Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Ijumaa Tukufu na nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza uko kwenye ukurasa wa 14 juu ya suala zima la uwezeshaji wananchi kiuchumi. Napenda kuipongeza Serikali kwa kutenga fedha za Mfuko wa Maendeleo kwa ajili ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, lakini niseme bado kuna changamoto kubwa kwa sababu hela inayotengwa haijaweza kuwanufaisha wananchi waliokuwa wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali iwe na jicho pana zaidi juu ya huu Mfuko wa Maendeleo kuhusiana na hii asilimia 10 kwa maana asilimia nne vijana, asilimia nne wanawake na asilimia mbili walemavu. Changamoto kubwa hapa asilimia 10 hii upatikanaji wake tunategemea vyanzo vya ndani vya Halmashauri zetu na Halmashauri nyingi zina changamoto kubwa mara baada ya kupokonywa baadhi ya vyanzo vyao kwenda Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na changamoto ya matamko ama maagizo ya Waheshimiwa Mawaziri pengine asubuhi ama wakisimama hapa Bungeni kwa kuagiza mambo kadha wa kadha, Halmashauri zifanye pasipo kuwatengea bajeti. Kwa hiyo, hilo ni tatizo kwani ile dhana nzima iyotafutwa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama hili jambo halijaangaliwa vizuri, haitakaa ifikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea hapohapo, tunawaambia Wakurugenzi kwamba wahahikishe wanatenga hizi hela ama baada ya kupokonywa hivi vyanzo tunawaambia wawe wabunifu, lakini wanapokuwa wabunifu wakianzisha vyanzo vipya Serikali Kuu mnawanyang’anya. Kwa hiyo, hili ni tatizo lazima Serikali tuliangalie kwa jicho pana kabisa. Pia, so long hii asilimia 10 hatujaiwekea utaratibu wa kisheria itakuwa kila siku ni hivihivi tunapiga dilly-dally hizi hela hazitakaa zitoke kwa ukamilifu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye ukurasa huohuo wa 14, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inaendelea kwa kusema kwamba, uwezeshaji wa wananchi wakiwemo vijana, wanawake na wazee. Hapa nitaomba kusaidiwa, nashindwa kufahamu Mfuko wa moja kwa moja ambao uko kwa ajili ya uwezeshaji wa wazee, nitaomba nije nisaidiwe ni Mfuko gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo niseme sioni namna wazee wanavyoweza kushiriki kwenye mchakato huu wa VICOBA, SACCOS ama huu Mfuko wa Maendeleo ambao tayari umeshajipambanua ni kwa ajili ya vijana, wanawake pamoja na watu wenye ulemavu. Kwa wazee napenda kuishauri Serikali, pengine muda umefika sasa ule mchakato wa universal pension (pensheni kwa wazee) mje nao ili tuweze kuwasaidia wazee wa Taifa hili. Sitaki kuzungumza sana, ni wazi tunafahamu mchango wa wazee kwenye Taifa letu. Kwa hiyo, nipende kuiambia Serikali…

T A A R I F A . . .

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda tu kuishauri Serikali iangalie namna bora ya kuanzisha mchakato wa universal pension (pensheni kwa wazee wote) ili tuweze kuwasidia wazee wa Taifa letu kwa mchango wao mkubwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili uko kwenye ukurasa wa 18 kuhusiana na suala zima la ajira. Nipende kuipongeza Serikali kwa kuanzisha miradi mikubwa ukiwemo wa Standard Gauge, Stiegler’s Gorge, bomba la mafuta, ujenzi wa viwanja vya ndege pamoja na ujenzi wa meli pamoja na vivuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba uanzishwaji wa miradi hii inaenda sambamba na upatikanaji wa ajira. Ninachopenda kuishauri Wizara isikae ikaishia ku-count kwamba Standard Gauge imetoa ajira ngapi, Stiegler’s Gorge itatoa ajira ngapi, napenda twende mbele zaidi ihakikishe inafuatilia huku kwenye hii miradi watu ama wananchi wanapata ajira zenye staha na job security. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu mikataba inayoingiwa kwa wananchi ambao wanapata ajira kwenye miradi hii imekuwa ina ukakasi ama imekuwa ikiwaminya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kwenye ujenzi wa feri ile ya Kigongo - Busisi, tulienda pale tumekuta ujenzi wa feri unaendelea, Watanzania wengi wako pale wameajiriwa, lakini changamoto inayojitokeza pale mikataba inakiukwa, ile mikataba ambayo imeingiwa haifuatwi. Kwa hiyo, nawaomba msiishie tu kuhesabu ajira zilizopatikana mwende mbele zaidi mkaangalie ajira hizi kama zina staha, mikataba inafuatwa na kama job security iko ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine uko ukurasa wa 44 kuhusiana na barabara. Asubuhi hapa wakati Mbunge wa Singida anauliza swali Wabunge wengi walisimama hapa kuhusiana na suala zima la barabara. Sote tutakubaliana Mikoa, Wilaya ama Majimbo ambayo yamepata ujenzi wa kuunganishwa kwa barabara ya lami uchumi wao unaenda haraka ukilinganisha na yale maeneno mengine. Tunakubaliana kabisa upatikanaji wa barabara ya lami kuunganisha mkoa mmoja na mkoa mwingine unapeleka maendeleo ya kiuchumi haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa nataka niiombe Serikali ikae chini na iangalie jambo moja. Kiukweli ujenzi wa barabara una gharama kubwa mno, kilometa mbili tu unakuta ni billions of money. Sitaki kuamini kama kwenye Wizara kuna kushindanishwa kwamba Wizara gani imekusanya kwa kiasi gani kwa sababu nature ya Wizara zingine ziko kwa ajili ya kutoa huduma tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu kwenye ujenzi wa barabara kumekuwa kuna tozo nyingi sana. Ukiacha hii ya fidia (compensation) ambayo hiyo kwa namna moja ama nyingine itakuwepo tu kuna hii fidia ya mrabaha au royalty ambayo barabara zetu zinajengwa kwa kutumia changarawe, kokoto, mawe, mchanga, maji, chokaa na kadhalika. Mradi wowote wa barabara huwa unai-include hivi vitu pamoja na hizi tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, vumbi la kokoto kwenye ujenzi wa barabara kwa mita moja ya ujazo Wizara ya Nishati na Madini inatoza Sh.25,000, mawe inatoza Sh.16,000 lakini kokoto kwa mita moja ya ujazo inatoza Sh.80,000, kuna tozo nyingi ambazo zinaingia inapelekea miradi ya barabara kuwa ya gharama sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali ama kuiomba hebu wakae chini waangalie kwamba endapo wakiondoa hizi tozo watakuwa wamepunguza gharama ya barabara kwa asilimia ngapi ama wamepunguza kwa kiasi gani, pengine inaweza ikasaidia. Niwaombe wakafanye hiyo analysis waone kama itaweza kuwa na mchango tukijaribu kuziondoa hizi tozo. Kwa sababu kuna ile Sheria ya Ardhi wanasema kwamba Serikali inapotwaa ardhi yake haiwezi kulipa, sasa inakuwaje hapa Wizara ya Ujenzi inaenda inalipa hela nyingi kwenye Wizara ya Madini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwa sababu kila Wilaya, kila Jimbo na kila Mkoa unasuburi kuunganishwa kwa barabara ya lami, ni vema sasa wakapitia sheria hii kama kuna uwezekano wa kupunguza hizi tozo zikapunguzwe ili suala zima la ujenzi wa barabara liende haraka haraka ili ziweze ku-boost uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumzia barabara kuna Kisiwa Mafia. Kisiwa kile ili uweze kufika kwenye Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani hakuna usafiri zaidi ya maji na kwa wale waliojaliwa ndege, lakini wananchi wengi wanasafiri kwa njia ya maji. Hatuna kivuko cha kuwavusha wananchi kutoka Mafia kuja Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani ambayo ni Kibaha Maili Moja. Sisi kule hatuhitaji barabara, tunahitaji kivuko. Kwa hiyo, niombe Serikali iwasaidie wananchi wa Mafia ili kuweza kupata kivuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa mwisho utakuwa kwenye ukurasa wa 44 kuhusiana na TARURA. TARURA ina changamoto kwamba kile kiasi cha 30% ambacho wanapewa hapohapo kinatumika kwa administration cost lakini nyingine kwa ajili ya maendeleo. Kwa hiyo, kile kiasi cha 30% kiongezwe ifike angalau 50%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu tuna barabara ya Vigwaza – Kwala – Dutumi - Kimalamasale ambayo inaunganisha Wilaya tatu za Mkoa wa Pwani, Bagamoyo, Kisarawe na Kibaha Vijijini. Tuna barabara pale ambapo unapita mradi wa bandari kavu, barabara ile TARURA wanasema hawana uwezo nayo, TANROADS wanasema iko kwa TARURA, wamekuwa wanatupiana mpira kati ya TARURA na TANROADS. Naamini kama TARURA wataongezewa hela ya kutosha pengine wanaweza wakaijenga barabara ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu Serikali tusisubiri mpaka ule mradi wa bandari kavu ukamilike ndipo tuweze kuipitisha ile barabara ya lami. Nadhani ni vema tungeitengeneza sasa hata kuvutia wawekezaji waende wakajenge kule hoteli. Pia wakati mradi unaendelea vifaa vinavyotumika kujengea mradi ule wa bandari kavu viweze kupita kwenye barabara ambayo inapitika vizuri. Kwa sasa hivi ile barabara haipitiki vizuri. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali iangalie namna bora aidha, kuichukua hiyo barabara kwa upande wa TANROADS…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.