Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii adhimu kabisa na mimi kuwa sehemu ya wazungumzaji siku ya leo. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia uzima wa afya njema na kuwepo kwenye Bunge hili Tukufu nikapata fursa ya kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge nimeapishwa juzi tu hapa, nimeingia kupitia dirisha dogo na mara nyingi wachezaji wanaosajiliwa katika dirisha dogo ni wachezaji wazuri sana. Nikishukuru Chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kunipa fursa hii adhimu kabisa hatimaye kuwagaragaza jamaa zetu kule na kupata ushindi wa kishindo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano Dokta John Pombe Magufuli, mimi namuita field marshal. Niliwaambia kuwa nampenda balaa na nampenda kweli kweli kwa namna anavyochapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijafanya sawa nisipomshukuru mama yetu, Mheshimiwa Samia, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyomsaidia Rais wetu kutekeleza majukumu yake. Pia sasa nikushukuru wewe Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri sana ambayo imetoa mwelekeo wa namna gani Serikali yetu katika mwaka wetu huu mambo yatakavyokuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wana Kinondoni wana matumaini makubwa sana na bajeti hii ya mwaka huu. Wana Kinondoni tuliwaeleza kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli ni Serikali ambayo imedhamiria kuleta maendeleo kwa Watanzania wote na wao ikiwa ni sehemu ya Watanzania. Niwaahidi wana Kinondoni kwamba uchaguzi umeshakwisha, tumepata ushindi unatosha na wote wawe kitu kimoja kushirikiana na Mbunge wao kuhakikisha wanaleta maendeleo katika Jimbo lao la Kinondoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaeleze tu ndugu zangu wa kipande cha kule kwamba uamuzi nilioufanya Katiba ya Chama nilichokuwa nipo kule unaruhusu na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu. Kwa sababu na wao siku hizi wamekuwa waumini wakubwa wa kutaka Katiba basi jambo hili wasilionee, usichokila usikitie hila, kwa maana kwamba, tumefanya kwa mujibu wa Katiba na siye ni waumini wa Katiba tusiwe na maneno maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine watazungumzia gharama hapa, uchaguzi umegharimu bilioni sita lakini siye au nyie siyo ndiyo mnataka twende kwenye Katiba Mpya, hivi Katiba Mpya tukiiingia kwenye hiyo kura ya maoni hatutotumia gharama? Hivi gharama yake itakuwa ndogo kuliko hiyo bilioni sita? Kama tunataka kweli kuwa waumini wa Katiba tuanze kuishi kwa mujibu wa Katiba tusianze kusemana kwa mtu ambaye amefanya maamuzi ambayo yanatekelezwa kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri tu, ushauri wa kwanza kwa chama changu kile kilichonilea kwamba kibaya chako chema kina wenyewe. Ushauri wa pili kwa Chama Kikuu cha Upinzani, CHADEMA waache kulialia wagangamale, kulonda kazi ya Jeshi kugangamala. Kama umeingia kwenye uchaguzi umepigwa unafanya tathmini unajipanga kwa ajili ya uchaguzi ujao. Mwisho wa uchaguzi ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwingine, tuonane 2020 na Inshallah Maulid Mtulia mtamkuta pale pale Kinondoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu chapa kazi. Chama cha Mapinduzi ndiyo chama chenye Serikali na ndiyo chenye jukumu la kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wa Tanzania na wengine jukumu lao ni kukosoa, kushauri, lakini bahati mbaya sana hili la kukosoa ndiyo wanalipenda, kwa hiyo usishangae wakija na maneno ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jamaa yangu mmoja mtani wangu anatoka hapa Ifakara, anakebehi kununuliwa ndege, basi okay wewe watu wako hutarajii kupanda ndege basi hata Daraja la Kilombelo hujaliona? Hata ile barabara inayojengwa kutoka Ifakara - Kidatu nayo hujaiona? Kwa hiyo, watu kama hawa wasimtoe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye lengo la kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kinondoni katika kuhakikisha tunatunza mazingira, tunainua uchumi wa wana Kinondoni na kuhakikisha tunashirikiana na Serikali kuleta ustawi tumekuja na mradi mkakati wa kuhakikisha Coco Beach tunaiendeleza. Tunahitaji Serikali itupatie pesa shilingi bilioni 7.2 ambayo tuna uwezo wa kuirejesha ndani ya mwaka mmoja. Tafsiri yake nini? Tafsiri yake ni kwamba kila baada ya mwaka mmoja tuna uwezo wa kutumia hicho kama chanzo cha ndani cha kuingiza shilingi bilioni 7.2. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuliahidi kwamba tunataka kujenga barabara na sisi Dar es Salaam na hasa Kinondoni tunatarajia sana kwamba barabara zetu zitajengwa. Tuna magari mengi na tunapojenga barabara na kuondoa foleni kiuchumi magari haya yanaweka mafuta na tozo ya mafuta sasa hivi ndiyo inaingia moja kwa moja kama kodi, maana yake magari yatakapotembea sana mafuta yatatumika sana na tutapata kodi sana. Kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha tunaondoa foleni katika Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna suala la masoko. Niishukuru Serikali imetutengea shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya soko letu la kisasa la Magomeni, lakini vilevile itenge pesa kwa ajili ya soko la Tandale ambalo ndiyo soko kubwa la chakula Dar es Salaam, pia na soko la Makumbusho na Mapinduzi ambayo ni masoko makubwa Dar es Salaam. Tukiyafanya haya yote, tutaongeza ajira kwa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Rais amehimiza kwamba wawekezaji wetu wa ndani na hasa katika masuala ya dawa na vifaa tiba wapewe kipaumbele. Mimi nina mwekezaji pale Jimboni kwangu, mpiga kura wangu ana kiwanda cha vifaa tiba pale Mwananyamala kinatengeneza gozi, hakijapata kupewa kipaumbele na badala yake MSD bado wanaendelea kununua kutoka nje. Sasa hii ndoto ya Mheshimiwa Rais tutaifika lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.