Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumbawanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia Mheshimiwa Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurudi salama na kuja kuwatumikia wananchi wa Jamhuri wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii tena kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kuwatumikia wananchi hawa. Nisiwe mchoyo wa fadhila kutoa shukrani kwa Wabunge wote walio humu ndani kwa heshima kubwa waliyonayo mbele ya Waziri Mkuu ndiyo maana unaona Bunge letu hili sasa hivi liko salama salmini. Laiti isingekuwa mahusiano mazuri na Waziri Mkuu leo hii Mawaziri wengine tungeshikana mashati humu ndani ngumi zingeruka, lakini haijawahi tokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongee mambo machache sana lakini yanayohusiana na Mkoa wangu wa Rukwa. Kama inavyojulikana sisi tunatoka Nyanda za Juu Kusini lakini zao letu kubwa ni mahindi. Nimeiona bajeti NFRA waliomba shilingi bilioni 86 lakini Wizara ya Fedha imetenga shilingi bilioni 15. Ni nini dhamira ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhusiana na hawa wakulima wanaolima zao la mahindi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa wakiongelea mambo mengi, nimeona wakiongelea kilimo cha pamba, korosho, katani, tumbaku lakini bila kulima mahindi hawa wanaolima tumbaku watakula nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli NFRA wametengewa shilingi bilioni 15 na naamini shilingi bilioni 15 zinatosha tu kwenye Wilaya moja tena Wilaya ya Sumbawanga Mjini kwa mahindi ambayo tunalima kwa wingi. Sasa ombi langu ni kwamba, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ananisikiliza, endapo Serikali haitakuwa na uwezo wa kununua mahindi haya ambayo wakulima wameyalima basi Serikali isifunge mipaka, iache mahindi yawe huru kila mtu akauze anapotaka kwa sababu mwaka jana mlifunga mipaka mlikuja kufungua mipaka dakika za mwisho kwa masharti makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilimfuata Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na kumweleza kuna wakulima au wafanyabiashara wadogo wadogo wenye gunia 10 au 15 wanataka kuvuka kwenda Congo, Kigoma leo hii mwambao wa Lake Tanganyika imekuwa ni rushwa kwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ananisikiliza; kama hawana uwezo wa kununua mahindi wawaachie wakulima wakauze mahindi wanapotaka. Watakuja hapa kama alivyosema Mheshimiwa Bashe mwaka huu, watazuia tena mahindi tusipeleke nje ili waweze kusingizia kwamba, hakuna mfumuko wa bei, wanawaumiza wakulima, hawana soko la kuuza mahindi yao, matokeo yake wamemweka mkulima ndiyo ngao ya kuhakikisha wananchi wa Tanzania hawafi na njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii si kazi ya mkulima, ni kazi ya Serikali kuhakikisha mkulima au mwananchi wa Tanzania hawezi kufa na njaa, mkulima mnambania kila eneo, kila sehemu na vikwazo juu ya vikwazo. Nimwombe tu Mheshimiwa Waziri kwa kweli mwaka huu kama itatokea wanafunga mipaka mimi nitakuwa wa kwanza kushikana mashati humu ndani ya Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sambamba na kilimo kuna mateso mengine yanawapata wavuvi wa Ziwa Tanganyika. Hawa Mawaziri mimi sijui Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Ulega tulimtegemea sana kama Mbunge kijana na Naibu Waziri kwamba atakuwa kimbilio la wavuvi; matokeo yake amekwenda kule amekutana na Waziri mwingine kazi yao imekuwa kuwaadhibu tu wavuvi, choma nyavu na mitumbwi, nyanga’anya huyu, piga faini huyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu niambie huyu mkulima anateseka, mvuvi anateseka nani kimbilio letu sisi wakati wa uchaguzi? Semeni tu maana imekuwa ni matamko tu, nafikiri kuna kasoro au tatizo ndani ya Wizara zetu na nafikiri labda kuna baadhi ya Mawaziri wanataka kumhujumu Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ana dhamira njema sana lakini kila kukicha nyavu zimechomwa, maboti yamechomwa, faini kubwa, mkulima hana pa kuuza mahindi, Mheshimiwa Tizeba ameinuka mbolea hakuna, yaani tabu juu ya tabu, vitu vinapandana siku hadi siku hakuna unafuu wowote kwenye hizi Wizara mbili, ni mateso juu ya mateso mpaka hata ngo’mbe wenyewe wanateswa sasa hivi wanapigwa mihuri siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Tizeba na Waziri wa Mifugo, hebu watupe afueni kidogo, tupumue sisi huko tunakotoka, matokeo yake sisi ndiyo tunaotakiwa kuwatetea, sasa tunakuwa tukiongea siku hadi siku na hawatusikilizi, matokeo yake tunakuwa kama tunaimba nyimbo bila sababu yoyote ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee barabara ya kutoka Sumbawanga – Tunduma, haijawahi tokea, ina kilometa 234 lakini ina matuta 240, matuta ni mengi kuliko kilomita tulizokuwa nazo kutoka Tunduma - Sumbawanga. Nataka nitoe mfano tu, Mheshimiwa Mipata alitoka India kufanyiwa operesheni ya mgongo ametua na ndege pale Airport Songwe kapanda gari kufika Sumbawanga mgongo umemrudia tena kutokana na matuta yalivyokuwa mengi kupita kiasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu ananisikiliza, Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu sijui ananisikia au wanaongea, sijajua; matuta yamekuwa mengi, tumwombe sana Mheshimiwa Waziri wajaribu kupunguza matuta haya, ni kero kubwa kuliko ambavyo tulitegemea kupata barabara ya lami yenye manufaa na wananchi. Sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hilo alichukue na alifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni kuhusiana na meli, Lake Tanganyika. Kila nikisikia hapa nasikia Mwanza meli mpya, tishali jipya, hivi Lake Tanganyika tumerogwa? Tuna meli toka uhuru mpaka leo hatuna meli nyingine yoyote ile. Wananchi hawa wanateseka mno na ukiangalia ile meli kwa kweli hata ng’ombe hatakiwi kupanda kwenye ile meli lakini leo kila kitu kinaachwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu afanye ziara siku moja aende akaitembelee ile meli aone athari zake na uchakavu wake ulivyokuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kiwanja cha ndege. Tumekuwa na mvutano wa muda mrefu sana lakini uwanja wetu wa ndege naamini ukikamilika utaleta tija kubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa hususan Jimbo la Sumbawanga Mjini. Tunapokuwa na kiwanja cha ndege na ndege zetu ambazo sasa hivi zimepatikana zikifika Sumbawanga tutarahisisha hata wawekezaji kufika ndani ya mikoa yetu na hata watalii kuja kwenye mikoa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka juzi tumepitisha bajeti ya kujenga uwanja, bajeti ya mwaka jana tumepitisha tutajenga uwanja, bajeti ya mwaka huu nimeona tunajenga uwanja, sasa sijajua labda ni uwanja mkubwa sana kuliko wa Dar es Salaam au ni uwanja mkubwa kuliko Dodoma kwa sababu kila mwaka tunapitisha bajeti, ifike wakati iwe mwisho. Kama bajeti ya mwaka huu itapita watuambie sasa wananchi wetu wasubirie uwanja wa ndege kama utajengwa au hautajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa kubwa tunalolililia sisi, wale wananchi wanaozunguka uwanja wa ndege toka wamefanyiwa tathmini ya malipo huu ni mwaka wa kumi wakati huo bei ilikuwa iko chini leo hii vifaa vya ujenzi vimepanda, viwanja vimepanda, sasa sijui fidia hii tutawalipa kiasi gani. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ifike mahali wananchi hawa ni wa kwetu sisi na sisi ndiyo tunaowatetea. Tuwe na moyo wa imani jamani, Mungu ametufundisha tuwe na upendo, tusali, tuombe Mungu, tuwasaidie na wale wasiokuwa na uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya wanapokuwa Mawaziri wanajisahau na bahati mbaya sana wakiwa huko sijui huwa kuna kitu gani kinapita, huwa wanajisahau kabisa kama na nyie ni Wabunge kama sisi. Wakirudi nyuma huku ndiyo wanaanza kuomba miongozo na kadhalika, lakini wakiwa huko wanajisahau kabisa, Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aangalie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nitawazungumzia watumishi hawa wa darasa la saba kama walivyosema Waheshimiwa Waunge wenzangu. Sumbawanga tuna dereva anaitwa Mapugilo ambaye alishawahi kumwendesha Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Injinia Stella Manyanya, kamwendesha vizuri, kaendesha Mawaziri wengine vizuri, kamwendesha Mkuu wa Mkoa, Waziri Mkuu Mstaafu, akija Sumbawanga gari la Mkuu wa Mkoa analotumia anayemwendesha ni Mapugilo, darasa la saba, lakini leo wameenda kuwatumbua, leo hii wamefukuza madereva wengi wa darasa la saba ambapo naamini kabisa udereva sio elimu, udereva ni ujuzi. Dereva anaweza kukuendesha hata kama hajui kuandika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, naamini kwa hili wanalisikiliza, warudisheni watu hawa. Warudisheni Watendaji wa Vijiji ambao wenyewe tuliwaajiri kwa cheo cha darasa la saba. Jamani tuwe na imani, hawa tunaowaonea ni binadamu kama sisi, inawezekana kwa njia moja au nyingine hatujui au hatuna ndugu ambao wanateseka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukimwangalia Mapugilo hana nyuma hana mbele, kafanya kazi leo mwaka wa 50 bado miaka mitano astaafu leo hii tunamfukuza, hivi kweli utu uko wapi? Wakulima shida, wafanyabiashara shida, madereva wa darasa la saba shida…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.