Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii . Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukurudisha salama na afya yako inaendelea kuimarika, hakika neno la Bwana lihimidiwe siku zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nichangie katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha hotuba yake vizuri kwa sababu inaeleweka. Nimeisoma na nimeielewa vizuri. Sasa naomba nianze kuchangia katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zote ambazo zinafanywa na Serikali yetu, lakini bado katika suala zima la afya, changamoto ni kubwa, wauguzi wamekuwa ni changamoto kubwa. Katika maeneo ambayo natokea, Mkoa wa Kigoma hospitali nyingi hazina wauguzi. Hata hivyo, pamoja na kwamba hazina wauguzi hata miundombinu ya hospitali hizo bado ni changamoto. Waganga wanaishi katika mazingira magumu, nyumba za Waganga hakuna. Niiombe sana Serikali ijitahidi kuzingatia hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya Mkoa wangu wa Kigoma tuna Hospitali ya Mkoa ambayo inaitwa Maweni. Hii ni hospitali kubwa ambayo inahudumia wananchi wengi na ukizingatia Kigoma tuko mpakani ambako tunapokea wakimbizi kutoka Burundi na Congo bado wanakwenda wanatibiwa mahali pale. Niiombe sana Serikali ituletee ma- specialist ndani ya Mkoa wetu wa Kigoma katika hospitali hii ya mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa uchunguzi ambao nimeufanya, mpaka sasa tuna-specialists watatu. Specialist wa akinamama, wa upasuaji na watoto. Niiombe sana Serikali mtuongezee ma-specialist katika hospitali yetu ya mkoa. Kwa sababu leo unapoweka specialist mmoja katika upasuaji naye ni mwanadamu ana dharura, kesho asipokuwepo kazini maana yake unawaambia watu wa Kigoma hamtakiwi kufanyiwa upasuaji. Niiombe sana Serikali ituletee wauguzi, ituletee waganga katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Spika, nimetembelea katika vijiji mbalimbali ndani ya Wilaya yangu ya Kigoma Vijijini. Nimekwenda Vijiji vya Kiziba, Mwamgongo na Bugamba, kuna changamoto kubwa. Usafiri wanaoutumia ni kupita na boti ndani ya maji. Tuangalie katika maisha ya kawaida mama huyu mjamzito anahitaji operation ya haraka, lakini hakuna boti ya haraka ya kuweza kumtoa Bugamba au Mwamgongo kumpekea hospitali ya Maweni. Niiombe sana Serikali iwaangalie watu wa pale angalau tupate boti ambayo litawasaidia wananchi wa maeneo haya kuwasafirisha kwenda katika hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, niiombe tena Serikali; natokea katika Wilaya ya Kigoma Vijijini, lakini mpaka sasa hatuna hospitali ya Rufaa; tuna vituo viwili vya afya ambavyo ni; Bitale, Nyamasovu ambacho ni cha mission na kingine kinajengwa Mwamgongo ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya amekifungua mwezi uliokwisha. Niombe sana Serikali mtuangalie Wilaya ya Kigoma Vijijini tuweze kupata hospitali hii ya wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala zima la vifaa. Hospitali ya Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine yote ya Tanzania, hospitali hizi zinakabiliwa na kukosa vifaa. Leo unapokwenda katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma hakuna CT-Scan machine inalazimu mtu apewe rufaa kutoka Kigoma kwenda Bugando, kutoka Kigoma kwenda Muhimbili; hali hii inasababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi. Niiombe Serikali tupate vifaa hivyo katika hospitali zetu na tuweze kuwasaidia wananchi wetu wapate huduma ndani ya mikoa yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala zima la barabara. Maeneo mengi ndani ya nchi yetu barabara bado ni changamoto kubwa. Nirudi kule kule katika Mkoa wangu wa Kigoma tuna barabara ambayo inatoka Mwandiga – Bubango – Chankele inakwenda Kagunga ambayo tunasema ni Kagunga Road.

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali itusaidie barabara hii iingie katika Mpango, iwekwe kiwango cha lami iweze kuwasaidia wananchi hawa ambao maisha ya yamekuwa ni kupita katika maji, wanahatarisha maisha yao na wao waweze kutumia usafiri wa barabara. Kwa hiyo niiombe sana Serikali, barabara hii muweze kuisaidia tuipate. Itatusaidia sana na wananchi hawa na wataweza kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine pasipokuwa na wasiwasi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la TARURA. Wananchi wengi hawana uelewa kuhusu TARURA. Natokea katika Kijiji cha Mwandiga, wengi hawaelewi TARURA wanafanya kazi gani na hata mimi nilikuwa nashangaa, kwa nini barabara hizi za mitaa hazifanyiwi kazi, nikajua ni TANROADS lakini nikaambiwa sasa zimekwenda kwa TARURA. Niiombe sana Serikali iwasaidie TARURA bajeti ipatikane, barabara hizi zitengenezwe.

Mheshimiwa Spika, vile vile nishauri TARURA washirikiane na watu kama Waheshimiwa Madiwani ili waweze kuwapa vipaumbele wajue ni barabara gani wanatakiwa wazianze, ni barabara gani za vipaumbele wazifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana Serikali ifanyie kazi hilo. Pia niongelee barabara ya kutoka Kidahu – Nyakanazi. Hii barabara ni potential, ni barabara muhimu sana. Kwa taarifa nilizonazo mkandarasi yuko pale lakini barabara hii inasuasua. Nimeipita nilikuwa nikitembea katika Vijiji vya Pamila, nimepita barabara ile, unakuta hapa pamechimbwa, hapa pamechimbwa, inaonekana mkandarasi yuko slow. Niiombe sana Serikali itusaidie barabara ile imalizike kwa wakati na kazi ziendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee tena katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Katika ukurasa wa 14 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu anasema kwamba kuna pesa ambazo zimetengwa katika SACCOS lakini pia katika vikundi vya akina mama zaidi ya bilioni 3.4 katika Halmashauri 53. Ningeomba ufafanuzi; hizi halmashauri ambazo hizi pesa zimekwenda ni zipi? Kwa sababu leo katika Halmashauri yangu ya Kigoma Vijijini kuna vikundi vya akinamama, kuna vikundi vya walemavu, kuna vikundi vya vijana lakini bado hawajapatiwa pesa hizo. Niombe kufahamu, halmashauri hii haijapata na kama pesa zimefika zimetumikaje au wanapewa akinamama wa mjini tu na sio akinamama vijijini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niiombe sana Serikali iwaangalie akinamama, vijana na walemavu, kwa sababu naamini ukimwezesha mama umeikomboa jamii; na vijana wa Kitanzania wanataka ajira, ajira imekuwa ni changamoto. Tuwawezeshe mitaji waweze kufanya kazi ili wasikae vijiweni ambako matokeo yake ni kuvuta bangi na kuingia katika biashara ya kujiuza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine niongelee suala zima la reli. Nimefurahishwa sana na Serikali kwamba, inakwenda kuanzisha huu mradi wa standard gauge. Ni mradi mzuri, tuuunge mkono, lakini ningeomba sana usiishie katika Mkoa wa Tabora, ufike mpaka Kigoma, tunahitaji standard gauge ndani ya Kigoma. Kwa sababu, naamini kabisa ikifika Kigoma tutakuza uchumi wa nchi, tutakuza uchumi wa Kigoma. Leo Kigoma tayari tumepata bandari kavu ya Katosho, naamini kama standard gauge itafika Kigoma, Wakongo, Warundi, magari ambayo watayaleta katika bandari ile ya Kigoma watatumia reli hii ya standard gauge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba, Kigoma na sisi tupate hii standard gauge ningeomba sana hii metre gauge, reli hii ya kati, Serikali iboreshe miundombinu. Changamoto ni kubwa, asilimia 90 ya wananchi wa Kigoma tunategemea usafiri wa reli ya kati. Wengi hawana uwezo wa kupanda ndege, wengi hawana uwezo wa kupanda mabasi haya kwa Sh.60,000/= wanakimbilia huku kwenye treni ya Sh.18,000/= lakini miundombinu ni mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Kigoma unaambiwa terni itaondoka saa 2.00 asubuhi, lakini unakuja kuondoka saa
8.00 usiku. Wale walioko pale abiria ni akinamama, watoto, kuna wagonjwa, kuna wajawazito. Wengine wametoka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono.