Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Madaba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa naomba niungene na wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na Watanzania kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kukurejesha salama na kuendelea na majukumu yako ya kulijenga Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, naomba kutumia nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo wametupa kipaumbele wananchi wa Madaba. Wizara ya Afya, Maji, Elimu, Miundombinu, Umeme na TAMISEMI hawajakauka katika Jimbo la Madaba. Kwa kweli, katika maeneo hayo tumepiga hatua kubwa sana na wananchi wa Madaba hawataridhi kama nitaanza hotuba yangu bila kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Wizara hizo pamoja na watumishi wote wa Wizara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, sitawatendea haki Mashujaa wa Vita ya Majimaji ambao tunawakumbuka tarehe 27 Februari, kila mwaka kwa sababu nisiposema baadhi ya maneno yamepotoshwa ndani ya Bunge lako Tukufu. Wiki iliyopita Mheshimiwa Ngombale aliilalamikia Serikali kana kwamba makumbusho tunayoyafanya Majimaji ni upendeleo.
Mheshimiwa Spika, tutatafuta nafasi ya kulifafanua, lakini kwa kifupi tu ni kwamba, historia ya makumbusho ya Majimaji sisi wenyewe wakazi wa Mkoa wa Ruvuma tulianza kuchukua hatua kuwakumbuka mashujaa wale na Serikali imekuja kushirikiana na sisi karibu miaka 90 baadaye. Sheria na miongozo ya Serikali ipo, nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge afuatilie hatua mbalimbali za kufikia huko na sisi Wanaruvuma tunaunga mkono sana jitihada za Watanzania wenzetu waliopigana vita kulinda heshima ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa niende moja kwa moja kwenye hotuba yangu. Hotuba yangu nitaiweka kwenye eneo moja tu kubwa muhimu, juu ya namna gani Serikali ya Tanzania, Serikali ya Uchumi wa Viwanda inahitaji sana ushiriki kamili wa Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki kifupi Wizara hizi mbili, Wizara ya Viwanda na Wizara hii ya Nishati, wamepiga hatua kubwa sana, hatua ambayo Waheshimiwa Wabunge hatuwezi kuibeza. Upande wa viwanda na biashara idadi ya viwanda imeongezeka kutoka 454 ambayo ilikuwa mwaka 2015 na sasa tuna viwanda vipya tu katika kipindi hiki cha miaka mitatu, viwanda 3,306.
Mheshimiwa Spika, katika hili nitaweka nukta kidogo. Kuna watu wanaibeza Serikali wakisema kwamba, viwanda hivi 3,306 si viwanda vyenye hadhi ni mashine za kusaga, sijui mafundi chereheni. Watu wafanye kazi ya kutafuta takwimu. Idadi ya ajira katika kipindi hiki kifupi, kwenye sekta binafsi, sekta ambayo inatokana na viwanda, ilifika 137,054; ukigawanya kwa idadi ya viwanda unapata wastani wa kila kiwanda kimeajiri watu wasiopungua 40. Sasa watu 40,000 si kiwanda? Watu wafanye kazi ya kutafuta takwimu.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine kuhusu viwanda tumepiga hatua; mwaka 2015 sekta hii ilikuwa inakua kwa asilimia 7.9 na sasa inakua kwa asilimia 9.8. Huu ni ukuaji mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, sekta ya umeme nayo imepiga hatua ambazo hatuwezi kuzibeza. Moja, sekta hii imejiwekea malengo ya mwaka 2020 ya kuwa na megawatts 4,915 na 2025 megawatts 10,000. Kwa kipindi hiki kifupi kuanzia mwaka 2015 wakati Serikali ya Awamu ya Nne inamaliza kipindi chake cha madaraka, ilimaliza wakati Watanzania tuna umeme wa megawatts 1,308 tu; leo tuna megawatts zaidi ya 2,500. Katika kipindi hiki kifupi katika sekta ya umeme, umeme umeongezeka kwa asilimia 52, hili si jambo la kubeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, Wizara hii inayoshughulika na umeme imeweka mikakati madhubuti ya kufikia malengo ya kuwa na umeme wa megawatts 4,915. Ipo miradi mipya ambayo imeanzwa ikiwepo Stieglers Gorge, lakini unaona kwenye Kinyerezi I na Kinyerezi II tunaona kuna Kinyerezi I Extension ambayo itazalisha umeme wa megawatts karibu 250, lakini kuna Kinyerezi III ambayo itazalisha umeme megawatts 600. Hiyo ni mikakati mizuri itakayotupeleka kwenye malengo yetu ya mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naona kuna watu wemesema jimboni kwangu. Nichukue nafasi hii, kwa vile nimekumbushwa niishukuru sana Wizara ya Nishati. Leo katika historia ya Madaba, mwaka huu uliokwisha tarehe 25 Desemba, 2017 wananchi wa Madaba wameanza kupata umeme, tangu kupata uhuru. Hili ni jambo la historia na ni jambo la kujivunia sana, naomba niishukuru Wizara katika kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, sipendi kusema kwamba, kila penye mafanikio hapakosi fitina, lakini nataka niseme kila panye mafanikio hapakosi changamoto. Malengo ya megawatts 4,915 tuliyojiwekea kwa mwaka 2020 na malengo ya megawatts 10,000 tuliyojiwekea ukilinganisha na Tanzania ya uchumi tunaoutaka ni kiwango kidogo sana cha umeme.
Mheshimiwa Spika, nitatoa mifano kadhaa. Zipo nchi kadhaa ambazo zimepiga hatua ambayo sisi sasa tunaelekea, lakini huko nyuma zilifanana sana na sisi kiuchumi na kimikakati.
Mwaka 1970 nchi ya Afrika Kusini ilikuwa na umeme wa megawatts 14,000 sisi leo tuna megawatts 2,500 na tunakwenda kutengeneza Tanzania ya viwanda kwa mkakati wa kuwa na megawatts 4,915. Umeme huu hautoshi kabisa na haya malengo ni ya chini sana, hayatatupa Tanzania ya viwanda tunayoitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ipo mifano mingi. Mexico mwaka 1994 walikuwa na megawatts 35,000; lakini leo Afrika Kusini wanaongelea megawatts 44,000 wakati nchi nyingine kama za Korea Kusini wanaongelea megawatts 84,000 sisi tumejiwekea malengo ya megawatts 4,000. Pamoja na kupiga hatua kubwa katika hilo, lazima tukiri kwamba, mkakati wetu lazima tuubadilishe na lazima tutengeneze vipaumbele.
Mheshimiwa Spika, sasa nataka niishauri Serikali kwenye eneo hili. Natambua mikakati mikubwa ambayo Serikali imejiwekea kwenye umeme, tuna mikakati hiyo ambayo nilikwishaitaja. Hata hivyo, kadri ya utafiti wa Benki ya Maendeleo ya Afrika vyanzo vya umeme wa Tanzania vinavyotokana na maji haviwezi kutupatia umeme unaozidi megawatts 4,000. Tunataka tutafute megawatts 10,000 na tunataka tufike megawatts zaidi ya 40,000 ili kupata Tanzania ya viwanda. Hiki kiwango ni kidogo, ni lazima Serikali iangalie vyanzo vingine.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba zilizotangulia tumeongelea kuhusu umeme wa gesi, nadhani kwa bahati mbaya Mheshimiwa Waziri Mkuu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.