Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hotuba iliyopo mbele yetu. Niliwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, sasa huu ndiyo mchango wangu mimi kama Sakaya, Mbunge wa Jimbo la Kaliua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendeleze kilio cha zao la tumbaku kwa sababu mengine sikuweza kuandika kwenye hotuba. Makampuni ya tumbaku yamekuwa na urasimu mkubwa sana kwa wakulima wa tumbaku. Mwaka 2014/2015 tulikaa kwenye kikao cha wadau tukakubaliana kupanga bei ya tumbaku kila kampuni inunue kwa dola mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo makampuni matatu; tunayo TLTC, Alliance One na GTI. Makampuni mawili ya TLTC na Alliance One walikataa kununua tumbaku kwa bei tuliyokubaliana kwenye kikao cha wadau. Kampuni ya TLTC walinunua kwa dola za Kimarekani 1.73; Alliance One walinunua kwa dola za Kimarekani 1.78, na GTI peke yake ndiyo waliokubali kununua kwa dola za Kimarekani mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya mawili yamesababisha hasara kubwa sana kwa wakulima wa Mkoa wa Tabora. TLTC peke yake, kwa mwaka 2015 kwa msimu mmoja tu wamesababisha hasara ya dola 3,953,558.3; Kampuni ya Alliance One imesababisha hasara kwa wakulima kiasi cha dola 2,537,800.10. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa pamoja makampuni haya yamesababisha hasara ya dola 6,491,758.40, sawa sawa na shilingi bilioni 13,665,676,156. Tumekaa kwenye mkutano wa wadau Mkoa wa Tabora tukakubaliana, hatuwezi kuruhusu makampuni haya kununua tena tumbaku msimu huu kabla hawajalipa hasara hii kwa wakulima wa tumbaku. Tunaiomba Serikali itusaidie, hasara iliyosababishwa kwa wakulima wa tumbaku kwa msimu mmoja tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposimama hapa Bungeni kulia kilio cha Wanatabora na tumbaku kwa ujumla, mtusikilize Mheshimiwa Waziri. Kama kwa msimu mmoja, makampuni mawili yanasababisha hasara ya shilingi bilioni 13 na ushee, rudi nyuma miaka yote ambayo wakulima wanalima tumbaku, ni hasara kiasi gani wanasababishiwa na makampuni? Naiomba Serikali itusaidie, makampuni haya yalipe fedha hii kwa wakulima kabla ya kuruhusiwa kununua tumbaku kwa msimu huu wa mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaruhusu viwanda kujengwa ndani ya nchi yetu, kwa nia ya kuweza kusaidia mazao ya nchi yetu yaweze kupata masoko. Tunaomba kupata majibu kwa Serikali, tunavyo viwanda ndani ya nchi yetu; tukianzia na Kiwanda cha Mkoa wa Dodoma cha kutengeneza mvinyo ambapo hatumii zabibu ya Mkoa wa Dodoma, anatumia concentrate, anakwenda kuchukuwa juice toka nje anatengeneza mvinyo wakati Dodoma tunazo zabibu zinatembezwa mtaani na akina mama, hazina soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali inaruhusu? Tulijua kiwanda kile cha mvinyo kingesaidia kuweza kununua mazao ya zabibu, leo akina mama wanaleta mtaani, zabibu haina soko la maana, lakini tunacho kiwanda ambacho kinachukuwa juice kutoka nje. Ni hasara kwa Serikali, ni hasara kwa wakulima. Kwa nini Serikali inaruhusu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo viwanda vya maziwa, leo tunaruhusu viwanda vya maziwa vinaleta Powder, vinatengeneza maziwa vinakwenda kusambaza, Lita moja ya maziwa ya powder ni shilingi 4,000, lita ya maziwa ya kawaida ni shilingi 1,000, huu ni unyonyaji wa hali ya juu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo juice, leo tuna machungwa nchi hii yamejaa kila kona, nenda Mwanza, Muheza yamejaa, tunakubali juice za nje, viwanda viko ndani vina-pack juice ya concentrate kutoka nje, wanakwenda kuuza lita moja shilingi 4,000 huku machungwa yanaoza, hayana soko. Kwa nini tunashindwa kutumia viwanda vya ndani kuweza kununua mazao ya ndani?
Naomba kujua, nini hatima na Mheshimiwa Waziri? Atujibu hapo, ni kwa nini wanaruhusiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala linguine ni Serikali kuruhusu vipimo ambavyo siyo halali; kuruhusu mazao ya wakulima kununuliwa kwa vipimo ambavyo siyo halali kwa kutumia rumbesa. Wakulima wananyonywa kupita maelezo! Wafanyabiashara wanajinufaisha sana. Leo mkulima wa hapa Gairo, gunia moja la viazi linawekwa rumbesa, akifika Dar es Salaam anatoa magunia mawili wakati kanunua gunia moja! Kwa nini Serikali haina huruma na wakulima wa Tanzania? Kwa nini Serikali inaruhusu wafanyabiashara wanakwenda mashambani wanashindilia magunia mpaka wananulia gunia lingine wanafunika kwa juu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waziri wa biashara akiwa Mheshimiwa Mama Nagu, tulimuuliza maswali hapa Bungeni na akaja na mpango wa kuhakikisha kwamba tunazuia vipimo ambavyo siyo halali tuje na mizani halisi. Baada ya muda mfupi wakaleta mpango wa mizani, then wakaja hapa Bungeni kwa Azimio wakaondoa ule utaratibu. Leo ni kilio kwa Watanzania, wakulima wanaumia, Serikali ipo inaona. Naomba kujua ni kwa nini hatuji na mizani kwenye mazao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ng‟ombe wananunuliwa kwa kupapasa, hakuna mizani. Hatuwezi kwenda kwa namna hiyo! Pia naomba kujua, kwa nini Serikali haianzishi Tume ya Udhibiti wa Bei ili kila mazao ya wakulima yanunuliwe kwa bei ambayo ni halisi, mkulima anufaike na mfugaji anufaike! Hatuwezi kwenda kwa namna hii wakati 70 percent ya wananchi wetu wanategemea kilimo na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni matumizi ya viatilifu na madawa ya mifugo na mimea katika mazao. Hili ni tatizo kubwa. Tumekuwa tunaruhusu, sheria inasema baada ya ng‟ombe kuchomwa sindano, aidha, antibiotics au baada ya mazao ya mboga mboga kuwekewa dawa za kuzuia wadudu yakae siku 14 shambani au ng‟ombe akae siku 14 kabla ya kupelekwa butchery.
Sasa dawa inapulizwa leo, kesho mboga ziko sokoni; kesho nyanya ziko sokoni. Unanunua mboga zina dawa unaziona kwa macho huhitaji hata kutumia darubini. Tunaharibu afya za walaji wetu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua na Serikali itueleze, wameweka utaratibu gani kufuatilia kuhakikisha mazao yanayokwenda sokoni ni bora na salama kwa walaji? Vinginevyo mimi nimekuwa najiuliza kila leo cancer zinazuka kila kona, kila leo mara figo zinaathirika, afya za wananchi wetu mpaka watoto wadogo! Hatuoni tatizo ni kwamba tunashindwa kudhibiti ulaji? Hatuoni tunashindwa kudhibiti mazao kwenye masoko? Tunaruhusu wananchi wetu wanakula vyakula, ambavyo haviwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaporuhusu ng‟ombe aliyechomwa antibiotic jana, leo analiwa, ile sumu ya madawa bado iko ndani ya mwili wake, inakwenda straight kwa mlaji. Leo mwananchi anaugua, akitibiwa dawa hazifanyi kazi; UTI imejaa, malaria hazitibiki, typhoid imekuwa nyingi! Tunaomba Serikali itujibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala linguine kuhusu matumizi ya hormone kwa kuku wa kisasa wanaofugwa, nalo ni tatizo kubwa sana. Unaweza kufikiria labda Serikali haipo! Hivi kweli kifaranga day one (chick) analelewa kwa muda wa wiki nne, ameliwa! Wiki nne, kuku anapewa hormone ananenepa, ukimkuta ana kilo moja au robo tatu ndani ya wiki nne. Huyu kuku ni salama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watoto wetu, nenda Dar es Salaam, watoto wa kiume wanaota maziwa, akina baba wanaota maziwa, Serikali haioni! Wanaruhusiwa wanauza wale Kuku. Angalau kuku wawe wamemaliza miezi miwili au miezi miwili na nusu. Kiukweli suala la afya ya Watanzania kwenye ulaji wa vyakula vya kisasa ni tatizo kubwa na hakuna udhibiti wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kujua, nimezungumzia suala la Vyuo vya Kilimo hapa nchini. Tunacho Chuo kimoja tu Tanzania kinachotoa degree zote kuanzia ya kwanza mpaka ya mwisho kwenye masuala ya kilimo na Mifugo, ambacho ni Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro. Kwa miaka miwili Serikali imeshindwa kupeleka hata senti moja ya maendeleo, Chuo Kikuu kimoja tu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale vyuoni kuna watalaam wana mifugo ya mfano, kuna mashamba ya mfano, watoto wanasoma, watoto wanakosa mpaka practicals, watoto wanasoma theoretical; tunataka kuboresha kilimo, tunataka kuboresha mifugo, watoto wetu wanasoma mpaka vyuo vikuu ni theory, hakuna practical! How can we move? Hatuwezi kwenda! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua, chuo kimoja tu! Kama tumeshindwa kukiangalia chuo kimoja; bahati nzuri Bunge lililopita tulikuwa tunasafiri tulikwenda nchi mbalimbali. Tulikwenda Indonesia, unapozungumzia habari ya drip irrigation unakwenda kuangalia vyuo vikuu, wanaonyesha kwamba drip irrigation ikoje na watu wanakuja kule kujifunza. Leo hapa tunazunguza vitu havipo. Naomba kujua, kama Chuo kimoja tunashindwa, kwa miaka miwili, miundombinu ni ile ile! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Sokoine, mimi ni product… (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako.