Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Masasi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi ya mimi kuchangia kwa muda wa dakika tano, nitazitumia vizuri. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri pamoja na wasaidizi katika Ofisi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwa kifupi, nataka nichangie kwenye hifadhi ya jamii. Watumishi waliostaafu wa Jimboni kwangu Masasi wameniagiza niseme kwamba kutoka mwaka jana mwezi Juni mpaka leo hawajalipwa mafao yao lakini pia wananchi hawa ambao wamestaafu hawajapewa hata fedha za kuhamisha mizigo kurudi majumbani mwao. Jambo hili linahuzunisha sana kwa sababu watu hawa wamekwishatumikia nchi hii na wameshafikia umri wa kustaafu, Serikali inapaswa kuwalipa haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kidogo pia kwenye kilimo. Niishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuimarisha sekta hii lakini pia sisi watu wa Kusini tunazo changamoto ambazo lazima tuziseme. Moja, toka tumepata tatizo la wakulima wa mbaazi kwa kutokupata bei mpaka leo Serikali haijasema kama iko tayari na imeshatafuta soko la mbaazi. Mpaka sasa hatuna majibu kwa wakulima kwa sababu mbaazi ziko mashambani tena, mwaka huu utaratibu ukoje katika kupata soko la mbaazi zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tukumbuke Serikali katika msimu wa korosho uliopita ilitoa sulphur bure kwa wakulima na sisi tulifanya kazi kwenye mikutano kuwashawishi wakulima wapate sulphur hiyo na Serikali ipeleke. Sasa tumebadilishiwa utaratibu tunaambiwa wakulima wanatakiwa wanunue sulphur.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaiomba Serikali itoe kauli haraka ili wakulima wajue sulphur hiyo inapatikana vipi tena kwa kudhibiti bei ya soko la sulphur. Kwa sababu mpaka sasa hivi tunavyozungumza bei ya sulphur ni Sh.70,000, Sh.80,000 kwa mfuko ambao walikuwa wananunua kwa Sh.27,000. Kwa hiyo, Serikali ina utaratibu gani wa kudhibiti bei hii ili wakulima wetu wamudu kuinunua na ipatikane mapema? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kidogo kuhusu suala la maji. Tunalo tatizo kubwa katika nchi yetu na Serikali kweli inafanya kazi ya kuhakikisha kwamba maeneo yote yanapata maji. Hata hivyo, katika Mkoa wa Mtwara, Wilaya ya Masasi na Nachingwea tunategemea chanzo cha maji cha MANAWASA. Hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo haya ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema mbaya sana kwa sababu hata Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja tulimwambia kwamba, MANAWASA wana tatizo kubwa la kutokwepo chujio la kuchuja matope, kiasi kwamba katika kipindi hiki chote wanafunga maji kwa sababu maji yale yanakuja yakiwa machafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika randama tumeona mmepanga shilingi bilioni mbili kuwapa MANAWASA lakini kwa sababu mara nyingi bajeti ya MANAWASA inakuwa haitoki, tunaomba sasa Serikali kwa kipindi hiki kilichobaki bajeti hii ya shilingi hizo bilioni mbili ipelekwe kwa ajili ya kufanya usanifu wa chujio la kuchuja tope ili wananchi wetu wapate maji na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni umeme. Wabunge wengi wamezungumza, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali lakini bado Mkoa wa Mtwara tuna tatizo la umeme, umeme unawaka kama indicator ya gari, unawaka unazimika, unawaka unazimika. Tumekwishaambiwa juhudi zinazofanywa na Serikali kwamba sasa hivi wanataka kufunga mashine nyingine ambayo itaongeza kiwango cha umeme. Tungependa Serikali ifanye jambo hili haraka kwa sababu linaharibu utaratibu mzima wa wananchi wa Jimbo langu pamoja na Mkoa mzima wa Mtwara kutokana na kukatikakatika umeme bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni REA. Nimezungumza na Waziri, nimezungumza na viongozi wa TANESCO, Jimbo la Halmashauri ya Mji wa Masasi vijiji vingi vimesahaulika. Tunaomba Waziri atakapokuwa anahitimisha atoe kauli ni vijiji gani sasa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)