Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nianze kwa kuendelea kuwapa pole wananchi wangu wa Karagwe kwa pengo kubwa tulioachiwa na ajali ya City Boys, Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu waliofariki mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda mimi nina mambo mawili; nianze na suala la kahawa na katika hili niipongeze Serikali kwa kuja na mfumo wa stakabadhi ghalani, lengo la kuleta mfumo wa stakabadhi ghalani ni kumsaidia mkulima wa kahawa ili aweze kunufaika na zao la kahawa na zao hili limsaidie kumtoa kwenye umaskini. Sasa ili tuweze kutimiza hii dhamira nzuri ya Serikali mimi Serikali naishauri mambo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye suala la butura; namna pekee ya kupambana na changamoto ya butura ni Serikali chini ya Vyama vya Msingi kuanzisha SACCOS ambazo zitakuwa zinakopesha wakulima wakati kahawa iko mashambani inasubiri kukomaa kuiva basi Serikali chini ya Vyama vya Msingi ianzishwe SACCOS itoe mikopo ya bei nafuu ili mkulima aweze kukopa na pale vyama vya ushirika vitakapouza kahawa yake aweze kukatwa mikopo hii ya bei nafuu. Kwa hiyo, hiyo ndio namna ambayo itatusaidia kuondokana na changamoto ya Butura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili pamoja na nia njema ya Serikali huu mfumo wa stakabadhi ghalani ili iweze kuleta weledi na uweze kumsaidia mkulima wa kahawa inabidi tujipange. Sasa bahati mbaya mfumo huu umeletwa wakati tunaingia kwenye msimu wa kahawa mwaka huu. Ushauri wangu kwa Serikali ili tuweze kujipanga vizuri maana kahawa lazima tuhakikishe iwe na ubora na ubora huu ndio itausaidia kupata bei nzuri sokoni. Serikali itumie mwaka huu kujipanga ili msimu wa mwaka unaokuja ndipo twende kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani, tutumie mwaka huu kuhakikisha kahawa inapotoka mashambani kwenda kwenye mnada ubora unazingatiwa kuanzia shambani kuna mambo ya miundombinu ya maghala, vyama vya ushirika vina madeni sasa hatujui Serikali imejipangaje kukaa na hivi vyama vya ushirika kuhakikisha haya madeni hayahamii kwa mkulima wa kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mambo haya yanatakiwa atupate muda wa kujipanga ili tutakapohamia kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani basi mfumo umsaidie kweli kweli mkulima wa kahawa kumkwamua kutoka kwenye umasikini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kuzungumzia ni mfuko wa uwezeshaji wananchi chini ya ofisi ya Waziri Mkuu. Mfuko huu ni wa muhimu sana hasa hasa kipindi cha sasa hivi cha Serikali ya Awamu ya Tano ambapo tunalenga kwenda kwenye uchumi wa kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda na tumekuwa tukisisitiza kwamba Serikali ijikite kwenye kusaidia Watanzania wengi katika shughuli ambazo Watanzania wengi wanajishughulisha nazo kilimo, mifugo na biashara ndogondogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko huu na sisi Wabunge wote humu ndani kwenye Wilaya zetu tumehamasisha watanzania Serikali hawezi kumsaidia Mtanzania mmoja mmoja tumehamasisha Watanzania wajiunge katika vikundi vya akina mama na vijana ili kupitia mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi ofisi ya Waziri Mkuu Serikali iwapatie mikopo ya bei nafuu. Sasa mfuko huu una bilioni 1.6 peke yake na toka mwaka 2013 mfuko huu haujawahi kupewa hata shilingi moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali hii Mwananchi Empowerment Fund ipeni hela ya kutosha iweze kuwasaidia wananchi kupitia vikundi vya wakina mama na vijana hasa vijijini ambapo tayari tumeshahamasisha na programu ya shilingi milioni 50 najua Serikali huko miaka ya mbeleni itaileta lakini tukitumia mfuko huu utawasaidia wakinamama na vijana Tanzania kuendelea na biashara ili zile shilingi milioni 50 zitapokuja baadae ziwakute wako katika kuzalisha shughuli za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipende sana kuomba Serikali ilichukue hili Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi upewe hela ya kutosha; shilingi bilioni 1.6 ni hela ndogo...

(Hapa Kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)