Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimefurahi jinsi ulivyolipatia jina langu, limekuwa likiwapa shida sana watu hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza pia kuzungumza katika Bunge lako, nichukue fursa hii kuwashukuru sana wananchi wangu wa Arumeru Magharibi kwa kura nyingi za kishindo ambazo wamenipatia. Labda tu ili uweze kuweka rekodi zako, mimi ndiyo niliyeshinda kwa tofauti ya kura nyingi kuliko Mbunge mwingine yeyote, takribani kura 62,000; siyo kidogo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti nakwenda moja kwa moja kwenye mchango. Nimefurahia, hotuba ya Waziri ilikuwa nzuri kama ambavyo zimekuwa zikitolewa hotuba nyingi nzuri humu ndani, lakini kwa kweli nina mashaka sana na utekelezaji wake. Takribani miaka kumi iliyopita, Wizara yake ya Kilimo ilikuwa ndiyo wimbo wa Serikali iliyopita, Kilimo Kwanza, lakini mpaka sasa hivi tumeshindwa kujua kilimo hicho kimetufikisha wapi na sasa kwa Serikali hii ambayo hatuoni namna gani ina-incorporate Kilimo Kwanza na Serikali hii ya viwanda ambayo mnakwenda kuifanya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi pia katika hotuba ya Waziri unanijia ni jinsi gani, sijapata kuona ni kwa namna gani anakwenda kumaliza matatizo ya migogoro ya wakulima na wafugaji; na wafugaji kwa wafugaji wenyewe? Ni matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya yangu kuna triangle moja ambayo sisi Monduli na Longido, wafugaji ambao wote ni Wamasai wanajeruhiana kila kukicha, wanagombania mpaka, kwamba ng‟ombe akitoka Arumeru Magharibi akaenda upande wa Monduli ni tatizo; akitoka Monduli akaja Arumeru Magharibi ni tatizo; akitoka Longido akaingia kwenye mashamba, sasa tunashindwa kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii migogoro ya namna hii ni kweli kwamba Serikali imeshindwa namna ya kumaliza matatizo haya ya wafugaji? Inakuwa vipi ng‟ombe wanaweza kutoka Arusha kwenda mpaka Morogoro, wakazunguka mpaka Mkoa wa Pwani; ukiondoa ile migogoro yao na wakulima; wafugaji kwa wafugaji hawagombani kwenye maeneo hayo, lakini wale ambao wanakaa, wako settled wanagombania mipaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Serikali ingekuja na kauli kama ambavyo tulivyo sisi Watanzania ambao tunaweza kuingia kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kama ni maeneo ya wafugaji kwa wafugaji, hakuna sababu ya kupigana kugombania nyasi, nchi hii ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ambayo ina ukubwa kuzidi nchi karibu nne za Afrika Mashariki; Kenya, Uganda na Rwanda ukiziweka pamoja bado Tanzania ni kubwa kuliko hizo nchi. Hizo nchi zina watu karibu milioni 100, sisi tuna milioni 50 tu. Nchi hii ni kubwa, ni nzuri ina karibia kila kitu kinachotakiwa. Hii ndiyo nchi ile ambayo ni ya asali na maziwa, lakini Serikali imeshindwa kuwatenga wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kutenga maeneo ya wanyamapori, tumeweza kutenga maeneo ya misitu, lakini tumeshindwa kuwatengea wakulima maeneo yao, wafugaji maeneo yao. Ni masuala ya kutoa kauli tu, tutengeneze corridor. Tutengeneze corridor ambayo wafugaji watakuwa wanaitumia bila kujali ni wa asili gani; awe Mmasai, Msukuma, Mnyamwezi, nani, kama kuna malisho na hayo maeneo yawe kama ni ya Serikali vile. Maana ni vigumu sana kwa wafugaji kupata hatimiliki kwa ajili ya kulisha mifugo mingi ambayo wanaifuga. Kwanza mifugo yenyewe inakwenda kulingana na malisho yanavyopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungetengeza corridor, kama ambavyo tumetengeneza Game Reserves kama ilivyozungumzwa hapo awali, tutengeneze corridor ambayo itakua ni ya wafugaji. Kama alivyosema Mbunge mwenzangu ambaye alitangulia awali, maeneo hayo yawe ni maeneo ambayo kuna maji, watawekewa miundombinu ya majosho na pia kuwa na maeneo ya masoko pia ili wafanyabiashara waweze kupata access ya kununua mifugo hiyo. Hii nchi ni kubwa na ina kila kitu. Kwa hiyo, tunaomba mtusaidie kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kiukweli hotuba hii ya Waziri kama hataidadavua vizuri namna gani anakwenda kukabiliana na tatizo la migogoro kwa kushirikiana na mwenzake Waziri wa Ardhi na pengine na Waziri wa Maliasili, ili tuweze kupata maeneo sasa na kuhitimisha suala hili la migogoro ya ardhi ambayo inalitia Taifa letu aibu, Taifa hili ni kubwa lina kila kitu tunashindwa kuvigawa. Kwa hiyo, Mawaziri hawa wakae pamoja na watuletee mpango ambao utatuonyesha ni kwa namna gani wakulima wetu wanakuwa safe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna tatizo kubwa sana la upatikanaji wa hatimiliki za ardhi kwa ajili hata ya hawa wakulima. Mimi kama nilivyosema, wakati mwingine ni mkulima lakini pia mfugaji. Ni mkulima wa ukweli, nalima kweli kweli, lakini tumekuwa tukipata shida sana ya kupata hatimiliki ya maeneo ambayo tumeomba na pengine hata Serikali ilitoa kabisa kwa ajili ya kulima lakini kuipata hatimiliki inakuwa ni shida sana. Kwa hiyo, Mawaziri wahusika wakae na wakubaliane kwa sababu bila hati pia unashindwa kupata misaada kwenye mabenki.
Kwa hiyo, Mawaziri wahusika wakubaliane namna gani wanaweza kuharakisha wakulima waweze kumilikishwa ardhi ili waweze kupata pia access ya mikopo ambayo inatolewa na mabenki na taasisi nyingine za kifedha. Kwa hiyo, tungependa tupate hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye suala la mbegu bora kwa ajili ya mazao ambayo wenzangu wamezungumza sana. Labda niseme tu Mheshimiwa Waziri, hii picha uliyoipiga hapa kwenye cover yako; hii picha ya dume inanipandisha mori kidogo. Hii ndiyo mbegu ambayo nilikuwa nasema tunataka tuzipate; mbegu bora ya ng‟ombe wa nyama, ndiyo kama hii. Mbegu hizi kwa kweli kwenye taasisi zako zinazozalisha mbegu bora, wanaziuza ghali sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dume kama huyu akiwa mdogo tu na mwaka mmoja, anauzwa shilingi 800,000 au shilingi milioni moja na kuendelea. Hii ndiyo bei halisi iliyopo. Kwa dume kama hili lililopo kwenye picha yako Mheshimiwa Waziri, mimi nimetoka mnadani juzi tu, shilingi milioni moja, shilingi milioni moja na nusu unapata hili dume, lakini ninyi mbegu mnauza shilingi 800,000, shilingi milioni moja. Hii mbegu ni kubwa na haionyeshi ile commitment ya Serikali kuwasaidia wakulima kuweza kubadilisha mbegu zao ambazo ni zile tunaita katumani. Kama ni mahindi tuite katumani; unalisha miaka mingi sana haifikishi kilo 100.
Kwa hiyo tusaidie tena, ulinijibu juzi kwenye swali lakini nisisitize tu kwamba bei mnayouza bado ni ya juu sana, mtusaidie ili tupate ng‟ombe wa namna hii ikiwezekana nchi nzima. Kwa hiyo, hilo naliomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alizungumzia ushuru wa mazao kutozwa sokoni. Naomba kabisa kwamba ikiwezekana ushuru huu utozwe shambani inapotoka. Kwa sababu haiwezekani Maafisa wa Halmashauri zetu wawasaidie wakulima lakini wakati wa kuvuna tozo inakwenda kuchajiwa Kariakoo; itakuwa mmetupunja. Kwa hiyo, naomba ushuru uchajiwe mara moja tu; kama ni mashambani au kwenye road block zilizopo kwenye Halmashauri na sokoni wasitozwe tena; kwenda kuitoza sokoni utakuwa umewadhulumu Halmashauri ambayo imekuwa ikiwasaidia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chakula cha njaa; enzi za Mwalimu kulikuwa na ile programu ya kwamba kila mkulima ni lazima awe na akiba ya chakula anapokuwa amevuna. Hiyo imekwisha, siku hizi hakuna na Serikali inahangaika na vigaloni au vidumu, chakula kiasi kidogo ambacho inakwenda kuwadanganyia wananchi na tunaona kama hii ni siasa ya kura. Serikali ije na mpango kama ule wa Mwalimu, kwamba kila mtu anapovuna awe na kichanja cha kuhifadhi chakula ili wakati wa njaa aweze kukabiliana na njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wanavuna halafu wanauza yote, halafu kesho Serikali inaanza kuhangaika kuwagawia kilo mbili mbili au tatu tatu za mahindi, kitu ambacho hakiwasaidii. Kwa hiyo, tuwe na mpango wa kisera kwamba wakulima waweze kushawishiwa kuhifadhi chakula baada ya kulima na tuepukane na hii kusambaza chakula ambacho hakiwatoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyeikiti, kwa hiyo ningependa pia kuishauri Wizara, nilipata fursa, nilikuwa Diwani hapo awali, nikatembelea nchi moja ya jirani hapo, sitaitaja. Kwa kweli tuliona wana mpango mzuri sana wa kuwasaidia wakulima. Wakulima wanapovuna kwa fujo, wamebahatika kupata mazao, wanakwenda kuyahifadhi vizuri kwenye maghala ya Serikali; na yale maghala yanakuwa yanathaminisha kile chakula au yale mazao ambao mkulima ameyazalisha na anapewa hati. Nafikiri nilishasikia hapa, sijui mnasema sijui ghala sijui nini, kitu kama hicho. Ile hati inamwezesha mkulima kwenda kukopa benki wakati anasubiria bei ya mazao yake yaweze kupanda value. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inamsaidia yeye kuweza kusomesha watoto wake au kujiandaa kwa msimu mwingine wa kilimo na kwa maana hiyo halazimiki kuyauza kwa bei ya haraka haraka. Tena anakuwa ameweka sehemu ambayo ni salama kimatunzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alisema hapa kwamba kuna dawa ambazo unawanyunyizia wadudu lakini wanaogelea tu na kutokea upande wa pili. Sasa kwenye maghala ya Serikali watapata fursa ya kuweza kuyatunza vizuri na kwa maana hiyo anakuwa na uhakika wa uhifadhi wa chakula kile na wakati huo Serikali ikimtafutia bei nzuri ya mazao hayo. (Makofi)
Naishauri pia Serikali, kama ambavyo ina kitengo kinachoshughulikia kutafuta ajira ndani na nje ya nchi, kuwe na chombo, kuwe na bodi kama ilivyo Bodi ya Utalii ambayo itakwenda nje ya mipaka yetu kutafuta masoko ya bidhaa ambazo tunazizalisha hapa nchini ili tuweze ku-entertain wananchi wengi kuingia kwenye kilimo kwa maana ya kwamba masoko yatakuwa yanapatikana. MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa bahati mbaya siungi mkono hoja.