Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Asha Mshimba Jecha

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri aliyoiwasilisha kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/2019. Wanachama wa CCM tumeridhika nayo kwani imelenga nchi yetu kutoka katika uchumi mdogo na kwenda uchumi wa kati wenye kaulimbiu ya Tanzania ya Viwanda inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushiriki wa wananchi katika kukuza uchumi nashauri Mikoa, Wilaya, Kata, Vijiji na Vitongoji viwe na uratibu unaoeleweka kwa wananchi na uwe wa wazi ili mwananchi azione fursa na kumrahisishia ushiriki wake kwa shughuli na miradi wanayoifanya. Fursa zilizopo zilenge kuwafikia na kuwashirikisha wananchi wa jinsi na rika zote mfano, vijana wa elimu ya juu, wanawake na wanaume mjini na vijijini pamoja na walemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wenye elimu ya kawaida wasiobahatika kupata elimu mijini na vijijini, wanawake, wanaume na walemavu nao wanao mchango mkubwa kwani kufeli shule si kufeli maisha. Mwelekeo wa kuwafikia kiurahisi ni kuwa na vikundi, ushirika, SACCOS, VICOBA na kadhalika. Elimu ya ujasiriamali kwa shughuli na miradi wanayopanga kufanya ni muhimu sana kupatiwa kabla na wakiendelea kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa za masoko ndani na nje ya nchi zisimamiwe kikamilifu na kupunguza au kuondosha urasimu usio na lazima ili kuwapa moyo na kuthamini kazi wanazozifanya, kuwakutanisha na taasisi za fedha na mabenki kuweza kukopa na kuongeza mtaji kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kuwawezesha watoto wote wenye uwezo wa kuingia shule waruhusiwe bila ya malipo. Hali hii wananchi wameipokea na kuwapeleka watoto kwa wingi. Wananchi hasa wanyonge wameitumia kikamilifu fursa hii na watoto wengi walioshindwa kujiunga na shule kwa kukosa malipo sasa wameingia shule. Changamoto iliyopo ni uhaba wa majengo na Walimu. Hata hivyo naamini Serikali kupitia wadau mbalimbali na taasisi wanaungana pamoja kulipatia ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa vyuo vya VETA kwa kujifunza kazi za amali (kujitegemea) kwa vijana wengi ambao wameshindwa kuendelea na masomo ya juu. Ukosefu wa takwimu sahihi kwa vijana wanaomaliza vyuo ama elimu ya juu na fani zao walizosomea. Nashauri mikoa, wilaya tuanzishe utaratibu wa kuwatambua wasomi wetu na fani zao walizozihitimu ili iwe rahisi kuwatumia na kuwashajihisha kujiwekea pamoja na kutafuta fursa na kuzitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuzaliwa Tanzania unazidi kuimarika, wananchi wake wanaishi bila bugudha yoyote ili mradi havunji sheria. Kwa kuwa Muungano huu ni wa watu bila shaka zinaweza kuwepo changamoto za hapa na pale, lakini zisigeuzwe na wapinzani wetu kuwa chachu ya kuvunja Muungano wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu ni wa damu, hivyo changamoto chache zilizobaki tuzitafutie ufumbuzi ili uzidi kuimarika. Hotuba, mijadala, makongamano yaeleze kwa uwazi mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka 54 ya Muungano wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unyanyasaji wa wanawake na watoto. Pamoja na jitihada kubwa inayochukuliwa na Serikali yetu ya kuweka sheria na kuridhia mikataba ya Kimataifa kupiga vita unyanyasaji wa aina zote wa wanawake na watoto, mafanikio yameanza kuonekana. Wanawake wanaweza kujitetea na kudai haki zao na kufikiwa na fursa mbalimbali bila ubaguzi, tunapongeza na kushukuru. Kwa watoto kumezuka makundi maovu yanawabaka na kuwalawiti watoto wa kike/kiume, sheria kali zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.