Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hoja muhimu na mahsusi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Kwanza kabisa naunga mkono hoja hii. Ni hoja ambayo imesheheni mambo ya msingi kwa Watanzania na hivyo ninashangaa sana watu ambao wanabeza juhudi ambazo Mheshimiwa waziri Mkuu anazifanya. Hilo ni kusema tu kwamba washindwe na walegee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo mawili yanayohusu masuala ya mazingira. Kuna mambo mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyazungumzia yanayohusu uharibifu wa vyanzo vya maji, uchafuzi wa mazingira kwenye vyanzo vya maji likiwemo suala la ukataji miti hovyo na suala la mkaa. Nataka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge jambo moja ambalo wanadamu huwa tunajisahau. Mwanadamu anapomuona mwenzake anakufa hakumbuki kwamba na yeye ni marehemu mtarajiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanadamu anapomuona mwenzake ni mlemavu hakumbuki kwamba na yeye ni mlemavu mtarajiwa. Vivyo hivyo, wako Waheshimiwa Wabunge ambao wanadhani kwamba mazingira yanahusu tu wanyama watatoweka, miti itatoweka, ndege watatoweka, wanasahau kwamba hata sisi wanadamu vilevile tutatoweka endapo hatutalinda na kuhifadhi mazingira ya nchi yetu. Kwa hiyo, na sisi wanadamu ni watoweka watarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria yetu ya mazingira inazungumzia namna ambavyo tunatakiwa kutoa miongozo kwa Halmashauri zote nchini pamoja na wadau wengine wa mazingira kuhakikisha wanaorodhesha vyanzo vyote vya maji pamoja na milima na vilima wakionesha changamoto za vyanzo vya maji kwenye maeneo yao pamoja na milima na vilima.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongozo hii inatuhitaji sisi baada ya kupata orodha hizo tuweze kuona changamoto za kila vyanzo vya maji ili vyanzo hivi tuweze kuvitengenezea miongozo ya kuvilinda ikiwa ni pamoja na kuvitangaza kwenye Gazeti la Serikali. Sasa kuna baadhi ya Wakurugenzi katiaka nchi hii ambao tangu Ofisi ya Makamu wa Rais imetoa agizo hili la kuwasilisha orodha hizi, muda ulishapita na juzi nikiwa Morogoro nimetoa muda mwingine wa mwisho kwamba tarehe 20 Aprili, 2018 Wakurugenzi wote nchi nzima wawe wamewasilisha Ofisi ya Makamu wa Rais orodha za vyanzo vya maji kwenye maeneo yao, vilima pamoja na milima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakurugenzi ambao wataendelea kukaidi agizo hili na kutolitekeleza, Mheshimiwa Waziri Mkuu najua mamlaka ya uteuzi Mheshimiwa Rais, kazi yetu sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tutaorodhesha Wakurugenzi wote katika nchi nzima ambao wamekataa kutekeleza agizo hili ili mamlaka ya uteuzi itafakari na kuona kama vitumbua vya Wakurugenzi hawa vinastahili kutiwa mchanga ama laa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vya maji vina uhusiano mkubwa sana na ndoto yetu ya Tanzania ya viwanda. Vyanzo vya maji vina uhusiano mkubwa na suala la uzalishaji wa umeme. Niwape mfano mdogo Waheshimiwa Wabunge, Mtera inazalisha megawati 80, Kihansi inazalisha megawati 180, Kidatu inazalisha megawati 204 na vyote hivyo vinahitaji sisi tulinde na kuhifadhi vyanzo vya maji na hasa maeneo ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawataka Watanzania ambao wanalima kwenye bonde hilo wazingatie masharti ya kulima kilimo cha uhifadhi (conservation agriculture) na wasijihusishe na uharibifu wa Bonde la Mto Ruaha Mkuu. Hata wake rafiki zangu akina Mheshimiwa Mwamoto, akina Mheshimiwa Chumi, Mheshimiwa Ritta Kabati ambao wana kilimo maarufu kinaitwa vinyungu, kilimo hiki cha vinyungu lazima kiende sambamba na kuhifadhi mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala lililojitokeza la shule ama vyuo ama taasisi ambazo zinatoa mafunzo kutokuwa na matundu ya vyoo na hivyo kusababisha ama wanafunzi, ama wafanyakazi kujisaidia porini na hivyo kuchafua mazingira; pamoja na kwamba kuna baadhi ya shule ambazo hazina matundu ya vyoo lakini hata shule ambazo zina matundu ya vyoo vikiwemo na vyuo vya kati na vyuo vikuu wana tabia ya kutapisha vyoo na kupeleka kwenye mifumo ya mito ambayo wananchi wanatumia kwa kumwagilia mbogamboga pamoja na matunda. Nimeenda Dar es Salaam pale, kuna vyuo pale ambavyo vinatiririsha maji kwenda Makuburi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo natoa tahadhari, shule zote ambazo nimefanya ukaguzi na kuwaambia watoe mabomba yanayotiririsha kwenye vyanzo vya maji wayaelekeze DAWASCO, na tutafanya ukaguzi nchi nzima. Yale mabasi ambayo bado hawataki kutekeleza agizo la Mheshimiwa Mwakyembe la kuchimba dawa, tutaanza kuorodhesha kutumia maafisa mazingira wa wilaya mabasi ambayo wanachimba dawa porini na kuchafua mazingira ili na wao tuwapige faini kama wale wengine.