Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Ofisi yake ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniokoa kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea tarehe 6 Aprili, 2018 nikiwa katika utekelezaji wa mjukumu yangu, niliponea chupuchupu. Aidha, kwa mukhtadha huo naomba nimlilie kijana wangu Mhandisi Izengo Ngusa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, aliyefariki usiku wa kuamkia jana kwa ajali ya gari.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru familia yangu, hususan Mke wangu Bi Warda na watoto wetu wote nane, wakiwemo sita nilioachiwa na marehemu mke wangu kwa kunipa ushirikiano wa kifamilia.
Aidha, naomba sana niwashukuru wapiga kura wa Sikonge na Chama cha Mapinduzi kwa imani wanayoendelea kuwanayo kwangu pamoja na majukumu ya Kitaifa. Ninamshukuru Mheshimiwa Selemani Said Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa uongozi wake wenye nidhamu ya kazi, weledi, uaminifu na uadilifu. Sisi Naibu Mawaziri wake ametufunza mengi sana kuhusu namna bora ya kutimiza majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati niwashukuru Watumishi wote katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kazi za kujituma katika kutimiza majukumu yao, kipekee naomba nimpongeze na kumtambulisha Bungeni Mwalimu Magreth Lubelege, kama yupo asimame ambaye licha ya kufundisha katika shule ya kawaida huko katika Manispaa ya Ilala, alikuwa pia akienda kuwafundisha watoto watukutu kwenye mahabusu yao, Upanga. Aliwawezesha wengi kufaulu mitihani ya darasa la saba kabla hajastaafu tarehe 30 Julai, 2017. Wengi wa watoto hao wako sekondari, wako vyuoni, wako vyuo vikuu na wengine tayari wameajiriwa. Mwalimu Magreth Lubelege ni shujaa kwani amewabadilisha watoto watukutu kuwa watoto wazuri. Maneno yake ni mafunzo kwa wengine, anasema alipouliza na waandishi wa habari na nanukuu’ “Mtoto kuwa gerezani si kwamba, hafai anafundishika ikiwa ataelekezwa na kufundishwa kwa upendo.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa walimu wote nchini kwamba, tumieni maneno ya Mwalimu Magreth Lubelege, waelekezeni watoto na kuwafundisha kwa upendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mheshimiwa Waziri wetu alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imepata wachangiaji 71 waliozungumza Bungeni na wachangiaji 49 waliochangia kwa maandishi, nawashukuru sana Wabunge wote waliochangia. Wameonesha hisia zao za kutuunga mkono katika majukumu yetu yenye changamoto za mahitaji mengi yaliyopo kulinganisha na ukomo wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni na ushauri wote mlioutoa Waheshimiwa Wabunge tumeuchukua tukiamini kwamba, pale mlipokuwa wakali mlisukumwa na hisia za kutorodhishwa na utendaji wetu katika baadhi ya maeneo, tumewaelewa. Mnataka weledi, mnataka uaminifu, mnataka uadilifu, mnataka uzalendo na mnataka tuzingatie sheria, taratibu na kanuni za kazi, STK tutazingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika masuala mahsusi, ufafanuzi wangu katika masuala hayo utakuwa ni ufuatao:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Waheshimiwa Wabunge wengi ambao Mheshimiwa Waziri atakaposimama atawataja wamezungumza kuhusu umuhimu wa Serikali kujenga madarasa, vyoo, ofisi, nyumba za walimu, majengo ya utawala, mabweni, mabwalo, maktaba, maabara na kadhalika. Serikali ikiachiwa jukumu hilo peke yake tutachelewa mno, kwa mfano, kuanzia Julai, 2016 hadi Disemba, 2017 Serikali kupitia mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo pamoja na Mpango wa Equip, ilipeleka kwenye Halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 106.5 mipango miwili kwa pamoja kukamilisha miundombinu iliyoanzishwa na wananchi kwa mwaka 2017/2018. Katika mwaka 2018/2019 tumetenga shilingi bilioni 8.7 kwa ajili hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ni makubwa mno wakati bajeti za Serikali zina ukomo. Hivyo, tunahitaji kuendelea kushirikiana na wananchi, wadau wa elimu wa ndani na nje ya nchi, huku mhimili mkubwa ukiwa ni wananchi wenyewe. Waraka Namba Tatu wa Elimu wa mwaka 2006 unaoainisha majukumu ya wazazi, jamii na wananchi wa maeneo husika bado uko hai, kilichokatazwa ni kuwatumia walimu kulazimisha michango kwa kuwapa adhabu wanafunzi, kuwatoa darasani ambao wazazi wao hawajachanga michango, hicho ndicho kilichokatazwa. Adhabu hiyo, haikuwa halali kwa mtoto kwa sababu hana kosa lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia siku ulipositishwa utaratibu huo michango yote ya wananchi kwa ajili ya miundombinu, chakula na hata kambi maalum za kimasomo inatakiwa iratibiwe na Serikali za Vijiji kupitia mikutano yao ya kisheria na taarifa lazima zitolewe kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, kuhusu viwango vya michango vilivyokubaliwa na kiasi kilichochangwa ili Halmashauri iratibu utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili na la muhimu sana, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu tatizo la upungufu wa walimu kwenye shule za msingi, pamoja na shule za sekondari, hususan walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukiri kwamba tatizo hilo lipo kama ifuatavyo; mahitaji katika shule za msingi ni walimu 273,454 waliopo 175,946, kwa hiyo, upungufu ni walimu 97,508. Mahitaji ya walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika shule za sekondari ni 35,136 waliopo ni 19,459, kwa hiyo, upungufu ni walimu 15,677. Tuna ziada ya walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari ambao ni walimu 21,165 ambapo wengi wao wana vipindi vichache sana vya kufundisha. Serikali inaendelea kuchukua hatua zifuatazo kurekebisha tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kwanza, kwa kuwa walimu wa masomo ya sanaa waliozidi katika shule za sekondari ni rasilimali watu ya Serikali, ili rasilimali watu hiyo itumike vizuri na kwa kuzingatia upungufu mkubwa wa walimu uliopo katika shule za msingi, imeamuliwa walimu hao 21,165 wahamishiwe kwenye shule za msingi. Huo ni uhamisho wa kawaida kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kituo kingine cha kazi, kazi hiyo ni hiyo hiyo ya ualimu. Mshahara ni ule ule haubadilishwi, daraja ni lile lile, kipaumbele cha juu katika uhamisho huo ni kuanza na walimu ambao zamani walikuwa katika shule za msingi wakajiendeleza kwa kusoma diploma au shahada ya kwanza ambao umahiri wa saikolojia ya watoto wa shule za msingi tayari wanao na wanayafahamu mazingira yaliyoko katika shule za msingi, wakiisha hao tunaenda kwa walimu wenye diploma na wakiisha tunaenda kwa walimu wenye shahada ya kwanza. Walimu wenye shahada ya uzamili hawahusiki na uhamisho huo isipokuwa kwa kibali maalum au maombi binafsi ya mwalimu mwenyewe na hayo ni maelekezo sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa agizo hili hadi ilipofika tarehe 31 Machi, 2018 jumla ya walimu 8,834 wamehamishiwa katika shule za msingi. Tumeyasikia malalamiko, tatizo kubwa lililopo ni utayari wa wanaohamishwa. Kuhamisha bila kuzingatia maelekezo tumeona katika baadhi ya maeneo na pia mazingira yale ya wanakopokelewa, jinsi ambavyo wale wanaotakiwa kuwapokea jinsi wanavyowapokea, hilo nalo limekuwa ni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaagiza Wakurugenzi na Maofisa Elimu katika Halmashauri zote kutengeneza mazingira bora ya utayari wa wanaohamishwa na pia wanaowapokea kwa kuanzia na wao wenyewe Maafisa Elimu wa Wilaya na Wakurugenzi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi zinazotakiwa kuzingatiwa pale anapohamishwa mtumishi, standing orders, lazima zifuatwe. Mfano, kama mtumishi anahamishiwa mbali na kituo chake cha kazi, lazima kumlipa posho stahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mukhtadha huo natoa wito kwa walimu wa sanaa waliozidi katika sekondari wakubali uhamisho ili waendelee na kazi hadi watakapostaafu kwa umri. Serikali inatambua kuwa licha ya tofauti ya lugha ya kufundishia mafunzo ya msingi kuhusu zana za kufundishia na saikolojia ni yale yale hakuna tofauti kubwa. Mukhtadha wa masomo ni ule ule, kama ni somo la historia ni lile lile, jiografia ni ile ile, kiswahili ni kilekile na kiingereza ni kile kile. Mwalimu anapofika kwenye kituo kipya cha kazi anachotakiwa kufanya ni kuchambua zana za kufundishia na ndani ya muda mfupi atajenga umahiri na weledi unaotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika baadhi ya masomo Maafisa Elimu wanaweza kuandaa mafunzo elekezi kwa njia ya mikutano ili kuelimishana vizuri zaidi kuhusu utekelezaji wa agizo hili la Serikali linalolenga kupunguza upungufu wa Walimu kwenye shule za msingi kwa asilimia 21.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine ni kuwa Serikali itaendelea kuajiri walimu kama hivi, tumepanga ifikapo Juni tuwe tumeajiri walimu 16,130, mwaka ujao tutaajiri walimu wengine 15,000 lengo ni kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi katika shule za sekondari, ifikapo mwaka 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumzia ni umuhimu wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike. Suala hili ni muhimu sana, lakini linatakiwa kuandaliwa kwa umakini kwa kuzingatia sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kwanza ni tofauti zilizopo kati ya familia zinazoweza kuwanunulia watoto hao taulo hizo na familia maskini ambazo hazina uwezo huo.
Jambo la pili, ni tofauti za kimazingira zilizopo baina ya shule za mijini kwenye urahisi wa kupatikana taulo hizo na shule za vijijini hasa vijiji vya mbali sana na miji ambako hata kama mtu ana fedha anaweza asipate taulo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya tatu, tofauti za ubora wa taulo zenyewe kutokana na viwanda zilikotengenezwa ili kuwa na uamuzi sahihi wa taulo zipi ni muafaka kutumika kwa wanafunzi wote wa kike katika shule zetu.
Nne, tofauti za bei ya taulo hizo kutoka eneo moja hadi lingine ambayo inaweza ikasababisha ugumu wa kupanga bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuzingatia sababu hizo, Serikali imeichukua hoja hiyo, ili mwaka 2018/2019 utumike kufanya uchambuzi na tathmini ya kina, ambayo hatimaye itatushauri kuhusu namna bora zaidi ya kutekeleza pendekezo hilo. Hatua ambazo tumeshaanza kutekeleza kwa sasa ni pamoja na kutoa maelekezo yafuatayo:-
(i) Kila shule iwe na mradi wa maji ikiwemo uvunaji wa maji ya mvua kwenye maeneo ya vijijini na shule za mijini waunganishe huduma za maji kutoka mamlaka za maji mijini.
(ii) Vilevile katika ujenzi wa vyoo vya shule wahakikishe chumba maalum kinatengwa mahsusi kwa ajili ya watoto wa kike kujihifadhi; na
(iii) Mwisho Wakuu wa Shule waendelee kuwatambua wanafunzi wanaotoka katika familia maskini zisizo na uwezo wa kuwanunulia watoto wao wa kike taulo za kike, ambao kwa kawaida huwa ni wachache. Kwa kutumia mwongozo wa ruzuku ya uendeshaji wa shule za sekondari wanaolekeza kutumia asilimia 10 ya ruzuku kwa ajili ya dawa na mahitaji maalum kwa wanafunzi wa kike, wawe na utaratibu wa kuwanunulia taulo hizo wanafunzi hao maalum kwa utaratibu utakaoratibiwa na Mkuu wa Shule husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa na Wabunge ni wale ambao waliomba maombi maalum yanayohusu Majimbo yao, hususan kwa upande wa sekta za elimu na maji tumeyachukua kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na Wizara za sekta husika. Maombi hayo ni pamoja na usajili wa shule, kupandisha hadhi shule kuwa kidato cha tano na sita na wananchi kupatiwa huduma za maji na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi waliozungumzia ni kuhusu gharama ambazo hazimo katika fedha za elimu ya msingi bila malipo. Naomba kulihakikishia Bunge kuwa gharama za umeme na maji zimo ndani ya fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule. Suala la mahitaji ya walinzi wa shule, matron and patron, kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu na hata wale wa kike bado linafanyiwa uchambuzi wa kina ili hatimaye utekelezaji wake uwe mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ambalo Waheshimiwa Wabunge ningependa kufafanua hapa ni changamoto za miradi ya maji katika maeneo yao. Napenda nikiri kwamba zimekuwepo changamoto kadhaa ambazo tumekuwa tukizitatua kwa kusaidiana na Wizara ya Maji. Miradi ya maji ni miradi ya miundombinu ambayo kabla ya utekelezaji lazima kujua chanzo cha maji, uwezo wa chanzo cha maji, aina ya mradi utakayotumika kama ni kuchota maji kwa mashine ya kuendeshwa kwa mkono au kuendeshwa kwa nguvu za nishati ya jua au kwa umeme au kwa mafuta au maji yanayotiririshwa kwa mteremko na kadhalika. Hatua hii ni upembuzi yakinifu na hatua ya usanifu ndiyo huelekeza gharama zinazohitajika kutengeneza mradi. Tukishajua gharama za mradi fedha hutengwa kwenye bajeti na hatimaye mchakato wa kuwapata Wakandarasi wa ujenzi na wasimamizi wao hufanyika ambao hatimaye Mamlaka za Serikali za Mitaa husaini nao mikataba ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ipo miradi ambayo fedha nyingi zimetumika, miundombinu isiyozingatia viwango vilivyomo kwenye usanifu imejengwa chini ya kiwango, ikiwemo iliyojengwa bila ya kuzingatia uwezo wa chanzo, wakati mwingine wamefukuzwa wakandarasi katikati ya utekelezaji na hivyo miradi kuachwa bila kutimiza lengo lake la kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zilizopo zinaonesha moja kwa moja sababu ni Mkandarasi asiye na uwezo unaotakiwa ndiye aliyepewa mkataba. Kwa kuwa taratibu za kuingia mkataba na wakandarasi zinafahamika duniani kote, kwamba huwezi kuingia mkataba na Mkandarasi bila kwanza kumfania due diligence yaani upekuzi maalum ili kutathmini uwezo wake wa kutengeneza mradi kabla ya kusaini mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihitimishe kwamba, tutaendelea kuwa wakali sana dhidi ya taratibu ambazo hazifuatwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Ahsante.