Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Rais wangu wa Zanzibar kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue fursa hii nimpongeze Makamu wa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya hususani wakati huu amejikita kwenye suala la mazingira pamoja na Wizara yake, kazi inafanyika vizuri. Matumaini yangu kwamba baada ya hapo mtaendelea kuondosha kero ndogo ndogo za Muungano zilizobaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa jinsi ya pekee nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nampongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi na vitendo vikubwa na mambo mengi anayowafanyia Watanzania yenye tija, yenye muonekano na yenye faida kwa wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kumshukuru Waziri na Naibu wake kwa kitabu chao kizuri, chenye mwelekeo na mwonekano wa kutatua kero za Muungano hususani pale kaka yangu Mheshimiwa January alipomalizia kusema yupo tayari kupokea kasoro ndogo ndogo na kero ndogo ndogo za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi hiyo basi nafarijika kumwambia kwamba kero ndogo ndogo za Muungano zipo na kweli zinahitaji utatuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kwenda moja kwa moja kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa tisa ambapo amezungumzia suala la elimu juu ya la Muungano.

Mheshimiwa Waziri na Naibu wako suala la elimu kwa Muungano linahitajika na siyo kuhitajika nje tu kwa wananchi hata Bungeni kwa Wabunge sisi tuliokuwepo humu tunahitaji kujua faida za Muungano, tunahitaji kujua uwepo wa Muungano na tunahitaji kujua nini maana ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia kaka yangu Waziri inawezekana ukachukua muda mkubwa kuwaelimisha wananchi lakini wenyewe Wabunge hatukuelimika juu ya suala la muungano. Maana leo ukisimama Mbunge unazungumza suala la Muungano kana kwamba sio Mbunge inakuwa haina afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili kwangu ni ombi kwa Waziri naomba suala la elimu ya Muungano tupewe na sisi Wabunge, inawezekana Tauhida ninavyouangalia sivyo anavyouangalia mwingine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri niombe elimu hii atakapopata fursa atuletee Bungeni ili tunapotoa michango kama Wabunge tujue nini tunazungumza juu ya suala la Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kati ya hivyo vitu vidogo vilivyopo. Kaka yangu Mheshimiwa January anakuja kila siku Zanzibar na tunamwona, sasa hivi hata mtoto wa miaka mitatu anamjua. Tunachokiomba kwake sasa atumie boti aache kutumia ndege, atumie boti kwenda Zanzibar ili apate kuona kero za wananchi wanyonge, mnyonge hapandi ndege, mnyonge siku zote anapanda boti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia kaka yangu Mheshimiwa January kwa sababu akipanda boti atajua nini kinachowakabili wananchi wa Tanzania katika suala zima la Muungano. Leo kaka Mheshimiwa January kijana kuliko yeye, umri chini yake, anatoka Zanzibar kwenye sherehe za pasaka Mtanzania bara anabeba TV ya inchi 14 kafurahia pasaka anasema nakuja huku nipate hii TV ya inchi 14, anatozwa ushuru ambao hatuufahamu mpaka leo. TV kainunua 125,000 anaambiwa TV ile ilipiwe 100,000, kijana kwa jicho langu namwona anaipiga chini TV bandarini vitu ambavyo ni vya masikitiko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wakati anazindua mradi wa reliā€¦

T A A R I F A . . .

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa kaka yangu January zinapoongelewa kero achukulie mfano wa ndoa ya mtu mwingine yoyote, maana hata kero kwenye ndoa zetu huwa haziishi. Kwa hiyo, Mheshimiwa January hizi ni changamoto aziandike aone jinsi gani ataweza kuwasaidia Watanzania. Leo kijana anakwenda pale anaipiga TV , amini Mungu kuna baba amebeba viporo vitupu zaidi ya ishirini anaenda kutia dagaa anatoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar vitupu, anachajiwa kiporo kimoja kanunua shilingi 100 anaambiwa alipe elfu 50, gharama ya vipolo vile 20,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama nimwambie Mheshimiwa kaka yangu January, Rais alizungumza wakati anazindua mradi wa reli, alisema kuna watu wana hujumu Taifa hili kwa kusingizia Muungano, kwa kutupia tope Muungano na wanatumwa na baadhi ya viongozi wenzetu. Mheshimiwa January kaka yangu, naomba kama kuna watu tusimsubiri kila kitu afanye Rais, aende, apite bandarini, tukisema hili Mheshimiwa kaka yangu atoke Makamu wa Rais aende litatia aibu, atoke, aende, akaangalie nini kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unawatoza wananchi kodi? Hiki kinafanywa kaka yangu sio lengo la Serikali, baadhi yao hawajaagizwa na Serikali, wanafanya kusudi kuupaka tope Muungano wetu. Kaka amepewa dhamana kubwa, dhamana aliyopewa Rais alijua ataitendea haki nchi hii, atawasaidiaje Watanzania, atumike kwenye nafasi yake, atoke, aende kama kuna viongozi au watendaji anahisi ni wabovu awatoe, afute. Rais amewazungumza sio mara moja, mara mbili wala mara tatu, Rais kila siku anawakemea lakini hivi vilivyobaki vifaurongo ahakikishe anaviondosha yeye, hatuhitaji Rais aende akamalize kazi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia Mheshimiwa kaka yangu January leo kero iliyopo pale kwenye Muungano ndio tutazimaliza hapa, kuna kero kubwa. Unakuta mtoto anatoka shule hii Tanzania ni yetu, anatoka shule Tanzania Bara labda anasoma Morogoro, anakwenda zake Zanzibar, tumezoea tiketi ni Sh.25,000/= anafika pale mwanafunzi wa shule anaambiwa akate tiketi ya Sh.50,000/= au Sh.60,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai kuna biashara za watu binafsi tunajua hakuna uhuru usiokuwa na mipaka, uhuru wowote una mipaka. Ikiwa nchi watu wanataka kufanya kazi bila kuwa na mipaka hatutokwenda, lazima kama kuna wafanyabishara binafsi washughulike nao, wazungumze nao. Huwezi kumchukua mtoto wa miaka 15,12 au 13 kavaa sare zake za shule na begi yake anatoka shule likizo, simu haruhusiwi kwenda nayo shule, mzee wake kamtumia pesa kupanda boti ya Sh.20,000/=... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.