Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, kwanza nashukuru Mungu kwa kutujalia uhai na pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii lakini niwashukuru na kuwapongeza Wizara ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mambo ya Muungano kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nathamini juhudi zao kubwa ambazo wanazozifanya katika kuzitatua changamoto, siwezi kusema kero ni changamoto na kitu chochote kinachohitajika kuendelea ni lazima kitakuwa kina changamoto zake, sasa nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri January Makamba kwa hotuba yake nzuri na kwa ziara ambayo aliifanya kule Zanzibar. Sasa Mheshimiwa katika ziara yake alipokwenda kule Zanzibar alilalamikiwa na wafanyabiashara. Namshukuru kwa kukutana na wafanyabishara wale ambao walilalamikia double VAT ambayo wanapata, ile VAT wakati wananunua bidhaa zao Tanzania Bara na pia wanapofika Zanzibar wanapata tatizo lile lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo hilo lilizungumzwa mbele ya Rais wetu Mtukufu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wafanyabiashara kutoka Zanzibar walimlalamikia lakini tukisema kodi tunazungumza kodi gani? Kodi hii iko sehemu gani? Kwa hiyo, kodi hiyo, naitaja, Finance Act ya mwaka 2016 kifungu cha 94 ya mwaka 2016 iliweka kifungu kipya katika VAT cha 55A ambacho kinasema:
“A supply of locally manufactured goods by a local manufacturer shall be zero rated if the goods are supplied to a taxable person registered under the Value Added Tax Law administered in Zanzibar and such goods are removed from Mainland Tanzania without being affectively used or enjoyed in Mmainland Tanzania”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndipo palipoleta tatizo la hiyo kodi ambayo ilikuwa ikizungumzwa na nashukuru Mheshimiwa Waziri kifungu hiki alipoenda kuwauliza mwenyewe wafanyabiashara na kwa bahati aliweka vikao tofauti jinsi ya kuvishughulikia. Sasa tamaa au matumaini yetu kwamba Serikali itakapokuja kwenye Finance Act ina maana kwamba jambo hili ni lazima lishughulikiwe, vinginevyo sisi ni watunga sheria, kama hatujalisema wazi hapa tutaliacha na litakuwa linaendelea kututafuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kitu ambacho kinapatikana kutokana na kifungu hiki, kwamba mtu akinunua bidhaa zake kutoka Tanzania Bara akipeleka Visiwani ikiwa yule mtu hajawa-registered by ZRB ina maana kwamba atachajiwa hapa asilimia 18, akifika Zanzibar atachajiwa na ZRB asilimia 18, kwa maana hiyo atalipa asilimia 36. Kwa hiyo, kwa mfanyabiashara mwenye mfuko mdogo hapa msingi wake unakufa kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hasara nyingine tunayopata ni kwamba watu wako tayari kwenda kununua bidhaa zile Kenya na wakati sisi tumo ndani ya Tanzania hii moja, mtu mmoja analipa asilimia 36 mwingine analipa asilimia 18 ya VAT kutokana na kifungu hiki. Sababu ya kifungu hiki kwamba ametajwa mtu lazima awe ame-register na ZRB kama ni taxable person. Sasa kwa taxable person wengine sio taxable person.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano zipo NGO au mashirika mengine ya kijamii, yanahitaji kujenga shule, kununua saruji, mabati na vitu vingine. Wakija kununua hapa wanaanza kuchajiwa huku mwanzo asilimia 18 na akifika Zanzibar anachajiwa tena asilimia 18. Nashukuru Mheshimiwa Waziri kwa taarifa ambazo zipo kwamba kikao kimefanyika, lakini tunataka utekelezaji wake na utekelezaji wake tunaomba Mheshimiwa Waziri alete hapa sheria tuje tubadilishe ili hii kero/changamoto iondoke. Bila kuondoka changamoto hii ina maana kwamba hatutoweza kufikia mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Serikali mwanzo ilipoona kuna hili tatizo wakasema wabadilishe sheria. Walibadilisha sheria hii naamini kwa nia nzuri tu, lakini utekelezaji wake baada ya kuingizwa haya mambo mawili kwamba lazima iwe manufacturer na lazima awe taxable person ndipo penye tatizo. Kwa hiyo, hili tatizo litakapoondoshwa, whether tukarudi kulekule mwanzo tukatumia origin principal kwa sababu hapa imepelekwa katika destination principal na ukipeleka kwenye destination principal bila ya kuwa na refund scheme ina maana hicho kitu si rahisi kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nakuomba ulete sheria hiyo hapa tuje tufanye marekebisho katika Finance Act. Bila ya hivyo utekelezaji wa hili tunalosema humu tutakuwa tunapiga kelele na sheria yenyewe ni hiki kifungu 55A kilichoongezwa mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, napenda kuzungumzia biashara, tumesema Tanzania ya viwanda, hatujasema Zanzibar ya viwanda wala hatukusema Tanzania Bara ya viwanda, tulisema Tanzania ya viwanda. Sasa ninachokiomba katika hili, ikiwa tunasema Tanzania ya viwanda ina maana kwamba hii movement of goods kama mtu akiweka kiwanda chake Zanzibar ina maana kwamba hatopata soko la Bara na ikiwa hatopata soko la Bara ina maana investment itakuwa haiwezi kufanyika Zanzibar kwa sababu bidhaa zake mtu hawezi kuingia kwenye soko la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachoomba, kwa kuwa soko ni kubwa na mtu anapofanya biashara anatazama location yake kwa mujibu wa soko lilivyo anapima Tanzania, Zanzibar ikiwa location kuna tatizo gani huyu mtu kumpatia ufumbuzi, kuna matatizo gani kuweka soko hili free? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nijulikane wazi sipiganii suala la askari, katika suala la askari niko pamoja na msimamo wa Serikali, lakini bidhaa nyingine, tukisema kwamba kila kinachozalishwa Zanzibar hakiingii Tanzania Bara ina maana kwamba tuna-discourage investment Zanzibar. Hakuna investor atakayekubali kwenda kuwekeza kule ikiwa msimamo kila kinachotoka kule kitakuwa hakifai kuingia huku, mtu anatazama soko kubwa na sisi tuko katika Afrika Mashariki, tunapima soko la SADC, tunatazama na soko la Tanzania. Sasa tukianza kujikataa wenyewe nani atatukubali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kingine, endapo nitazungumza nje ya miko ya taasisi inayoniongoza kisiasa nitaitwa Msungo na kama atatokezea mtu kwamba hana miko katika kuzungumza na taasisi inayomwongoza jambo la ndani akalitoa nje au jambo la kusema ndani yeye akalifanya nje, mtu yule kisiasa anaitwa msungo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili jambo la usungo linafanyika humu. Inakuwaje mtu jambo kama hili inakuwa mtu unalifanya, kitu ambacho kwamba kinajulikana faida za Muungano au chama fulani ndiyo kina msimamo wa Muungano huu, lakini anatokezea mtu pengine umri mkubwa tu akaja akafanya mambo akacheza shere Muungano. Kwa maana hiyo huyo mtu yeye sasa ndio anabakia anakuwa ndio kero ya Muungano, Muungano hauna kero kama alivyo kero huyo mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, nina wasiwasi huenda ikawa kuna minazi ya mpakani humu la sharikia wala gharibia, maana huo mnazi hauko mashariki, hauko magharibi, hatuujui mnazi wa wapi. Kwa hiyo aseme mtu waziwazi, lakini asifanye usungo wa kisiasa katika Bunge lako hili tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.