Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nianze kusema naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge wakati wanachangia hoja hii, lilijitokeza suala la utekelezaji wa Mradi wa Rufiji Hydro Power maarufu kama Stiegler’s Gorge. Michango ile ilielezea wasiwasi wao kuhusu utekelezaji wa mradi huu na masuala ya mazingira. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kuwa utekelezaji ni kweli Serikali ya Awamu ya Tano itatekeleza Mradi huu wa Rufiji Hydro Power ambao utazalisha Megawati 2,100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia hata historia mbalimbali za mradi huu tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza mpaka ya Nne na mpaka hii ya Tano, tathmini mbalimbali juu ya mazingira zilifanyika. Katika taarifa zile za tathmini hakuna mahali popote ambapo ilionekana mradi huu usitekelezwe kwa sababu ya mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nilithibitishie Bunge lako tukufu kuwa mradi huu Serikali zote zilizopita zimefanya tathmini lakini Serikali hii ya Awamu ya Tano imeamua kuutekeleza kupitia mapato ya ndani kutokana na uhitaji mkubwa wa nishati ili kutekeleza uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali imejielekeza kuzalisha Megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020. Ni kweli mpango huu kabambe wa Power System Masterplan umeelekeza miradi midogomidogo ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji, lakini mradi huu na ukilinganisha na gharama ya kuzalisha umeme kwa unit moja kwa kilowati kwa kutumia maji ni Sh.36/=, kwa kutumia gesi ni Sh.147/=, kwa kutumia mafuta ni Sh.346/=, ni wazi utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji ni nafuu. Vile vile kwa kuwa lengo la Serikali ni kupata nishati ya umeme yenye unafuu na Watanzania waweze kuitumia majumbani, viwandani, kwa hiyo, lazima tutekeleze huu mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ambayo imetajwa kwa huu mradi kabambe wa kuzalisha umeme kwa mfano Rumakali, Luhuji, Mpanga, Songwe, Rusumo, Malagarasi, Kakono, ni kweli ipo, lakini hii itatekelezwa baina ya ubia binafsi na wadau mbalimbali. Kwa hiyo, nataka nilitaarifu Bunge lako kwamba kwa kweli naomba watuunge mkono, mahitaji ya umeme ni mengi na Serikali imethubutu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu wake na mradi huu unatekelezeka bila tatizo lolote. Hata sasa wataalam wa chuo kikuu wameshamaliza Environmental na Social Impact Assessment na wataiwasilisha Wizarani na NEMC baada ya wiki moja. Kwa hiyo, naomba tu Bunge lako Tukufu lituunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, lilijitokeza suala la upatikanaji wa nishati au deni la umeme kwa Shirika la ZECO Zanzibar. Naomba niwaarifu wenzetu upande wa Zanzibar kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo na tumeipa kazi EWURA ifanye study ya gharama mbalimbali za kuzalisha umeme ili tufikie muafaka. Naamini Kamati yetu ya Nishati na Madini ilitu-task hiyo kazi na tunaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu Zanzibar kupitia ZECO wanalipa lile deni kiwango ambacho tunakubaliana, lakini lile deni ambalo hatujafikia muafaka mazungumzo yanaendelea na baada ya miezi miwili utafikiwa muafaka na hili deni litakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wazara hii kwa kazi nzuri.