Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Dr. Adelardus Lubango Kilangi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja iliyoko mezani. Nitaanza kwa kuchangia kwa maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambayo ilizungumza mambo mawili yanayohusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Kamati imeshauri na kupendekeza kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahitaji kuimarisha Mfumo wa Uandishi wa Sheria pamoja na usimamizi wa mikataba kwa namna ambayo itaweza kusaidia kulinda maliasili zetu za Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba ushauri huo wa Kamati umepokelewa na kwamba hatua tayari zimeanza kuchukuliwa. Katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali sasa tunaanza kujenga uwezo mahsusi kuiwezesha ofisi hiyo iweze kushughulika na hii mikataba, kwa sababu hii mikataba ina mambo ambayo yako a bit complex, yanahitaji utaalam wa juu. Kuna sheria za mikataba huko ndani, kuna sheria za uwekezaji, kuna sheria za Kimataifa, kuna sheria za aina mbalimbali ambazo zinahusika humo. Tumeligundua hilo na tunalifanyia kazi tuweze kuwa na wanasheria waliobobea katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu, hata Mheshimiwa Rais amechukua hatua kadhaa za kuweza kuiboresha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kiasi kwamba sasa inaweza ikakabiliana na changamoto na technicalities zote zilizomo katika masuala ya mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imetoa ushauri kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iongezewe rasilimali ili iweze kufanya kazi zake vizuri. Naomba tu nikuhakikishie kwamba ombi hili limeshapokelewa tayari na Serikali, kwa maana ya kwamba bajeti ya mwaka huu nafikiri kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaongezeka kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna michango kadhaa ya Waheshimiwa Wabunge na baadhi imeelekezwa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, labda nitaomba niizungumzie kidogo. Mheshimiwa Zuberi - Mbunge wa Liwale ambaye mchango wake pia umeongezewa nguvu na Mheshimiwa Richard Ndassa ambaye amezungumzia uwezo wa Wanasheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa kuingia mikataba kwamba pengine imeonekana mikataba hiyo haikuwa na tija na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, hatua zinachukuliwa. Mheshimiwa Rais ameanza kutusaidia kwa kuchukua hatua kuirekebisha na kuibadilisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sisi huko ndani tumejipangia mikakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ndassa alisema ni vyema sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikawa na specializations kule ndani. Tunakubaliana naye kwa asilimia mia moja. Yanapokuja masuala ya ujenzi, ni vema ukawa na mtaalam wa sheria za ujenzi; yakija mambo ya kodi, uwe na mtaalam wa sheria za kodi; yakija mambo ya mipaka, migogoro ya mipaka na kadhalika uwe na mtaalam wa sheria hizo na ndiyo ofisi nyingine za Wanasheria Wakuu duniani zinavyofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa kwamba tumeona hatuhitaji tu kuwa na wanasheria ambao wako specialized, lakini kuna baadhi ya maeneo tunahitaji tulete ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hata wataalam wasio wanasheria. Kwa mfano, una mambo ya construction ya ujenzi wa barabara, kwa kweli inafaa sana mkawa na engineer wa mambo ya barabara. Kuna mambo labda ya afya, ni vema mkawa na mtaalam wa mambo ya afya ambaye sio mwanasheria, atatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia na michango mingine nitapenda nijielekeze kwa mchango wa Mheshimiwa Lema, amezungumza kwa kweli kwa hisia juu ya mwenendo wa kesi mbalimbali na ametaja kesi ya Mwale, Ringo Tenga, Kitillya na Sioi; ninafikiri kwa ujumla sekta ya sheria ina lengo moja la kuboresha utoaji wa haki. Hilo ndiyo lengo la sekta ya sheria. Nikisema sekta ya sheria ninachukua kwa ujumla wake Mahakama, Wizara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ni vema nikalisema hili kwa sababu mchango huo unazungumzia kwa kweli kusimamia utawala wa sheria na alikuwa akipata mashaka kidogo tunapozungumza kwamba kama kesi iko Mahakamani tusizungumzie hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitaka kuweka msisitizo katika kusimamia utawala wa sheria, ukitoa hoja ambayo inapingana na essence ya utawala wa sheria, inaleta matatizo kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana nyingine ni kwamba Mheshimiwa Mbunge nadhani alipenda kusema kwamba tusifungwe sana na taratibu zetu zinazosema tusilizungumzie suala linapokuwa liko Mahakamani. Hili liko katika Kanuni zetu za Kudumu za Bunge, kanuni ambazo Bunge lenyewe limetunga, Kanuni ya 64(1)(c) ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016 inasema kwamba tusijadili jambo ambalo Mahakama haijalitolea uamuzi; ni kanuni zetu. Hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi wazi kwamba Mahakama itafanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa wala kutiwa shinikizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatari ya kujadili mambo ambayo yako Mahakamani ni namna moja ya kuipa Mahakama shinikizo. Kwa hiyo, labda niseme tu kwamba wale wote tulioko katika sekta ya sheria, tunafanya kazi ya kuhakikisha kwamba mfumo wa sheria unakuwa bora zaidi. Mifumo yote duniani, hata ukienda Marekani, utakuta kuna matatizo yake. Watasema mfumo huu una shida na mfumo huu una shida. Siku zote kinachofanyika, ni kufanya juhudi ya kuuboresha. Basi tusipendekeze kuboresha mfumo wetu wa sheria kwa kuvunja sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo, huo ndio mchango wangu na ninaunga mkono hoja. Ahsante.