Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa dhati kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara hizi mbili; Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa kazi kubwa anayoifanya. Kiukweli amethibitisha kwamba anaweza, ingawa Wizara hii ina changamoto nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Wabunge wote hapa leo ukiwauliza kama kweli tunahudhuria kwenye vikao vyetu vile vya Halmashauri vya Madiwani, hakuna mtu ambaye halalamiki juu ya fedha kutoka Hazina kutopelekwa Halmashauri. Kama kuna Mbunge hapa leo anaweza akatuthibitishia kwamba fedha wanapelekewa kwa wakati na kadri zilivyopagwa basi labda hiyo ni Halmashauri ya nchi nyingine haipo Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo haliko kwingine, tatizo liko kwa Wizara ya Fedha, tatizo analo Mheshimiwa Dokta Mpango. Kwa nini fedha za miradi mikubwa yote, Mheshimiwa Dokta Mpango, anazo, kwa nini fedha za Halmashauri ambako ndiko waliko wananchi, ndiko wanakohudumiwa wananchi wa chini, fedha hana kwa nini? Tunapokwenda kwenye vikao vya Halmashauri, Wakurugenzi tukiwabana wanatuambia ninyi ndiyo mnatoka Bungeni na ninyi ndiyo mko na Waziri wa Fedha huko, muulizeni kwa nini haleti fedha. Kwa hiyo, mtu mmoja ambaye labda anaweza kukwamisha Wizara ya TAMISEMI isifanye kazi vizuri ni Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa sababu hapeleki fedha Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni suala la watumishi, Ofisi ya Utumishi, Mwenyekiti wangu wa Kamati ameeleza hapa kwamba mwaka huu Wizara inayoongozwa na Mzee wangu, Mheshimiwa Kapteni Mkuchika, bajeti yake imepungua kwa shilingi bilioni 152 kutoka kwenye bajeti ya mwaka jana na hii ndiyo Wizara inayoajiri, hii ndiyo Wizara inayosimamia Utumishi wa Umma nchi hii. Sasa tunataka Mheshimiwa Waziri atueleze, hiki kiasi kilichopungua cha bilioni 152 maana yake ni nini? Kwamba shughuli za kuajiri hazitafanyika tena, kwamba hakuna ajira mpya, kwamba hakuna promosheni? Maana suala la kuongezwa mshahara nadhani Watumishi wa Umma sasa hivi wameshalisahau, limeshaondoka kwenye utamaduni wa kawaida. Hata hivyo, hata kuajiri hamtaajiri kama shilingi bilioni 152 mnaiondoa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata shida nikisikiliza kwamba Rais anasema mwaka huu tutaajiri, napata shida ukisikia Viongozi wa Serikali wanasema tutaajiri watumishi wa afya, unapokuja kusoma vitabu vya bajeti unakutana na fedha zimepungua kwa bilioni 152, napata shida kuamini kwamba haya yanayosemwa kweli yatatekelezwa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye TAMISEMI, nizungumzie suala la zahanati. Kwenye Halmashauri zetu tumejenga zahanati nyingi. Mheshimiwa Waziri, zahanati zimekamilika na nyingine zinabomoka, zimechakaa, zimekaa miaka minne, mitano, hazifunguliwi kwa sababu hazina watumishi. Sasa naomba kujua, nini mpango wake wa kutafuta watumishi wa idara za afya ili waende wakafungue zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu kuna zahanati tano zimekamilika, mbili Mheshimiwa Rais alipokuja mwaka jana mwezi wa Tatu alitoa agizo kwa Mkuu wa Mkoa kwamba hakikisha ndani ya miezi miwili ziwe zimefunguliwa, mpaka sasa zile zahanati hazijafunguliwa. Naomba Mheshimiwa Waziri amfikishie salamu Mheshimiwa Rais kwamba zile zahanati mbili zilizojengwa na mfadhili pale Mchinga na Ruvu ambazo Mheshimiwa Rais alitoa order zifunguliwe ndani ya miezi miwili, hazijafunguliwa, naomba ampelekee salamu hizo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI, nimesikitishwa sana kuona kwamba Mawaziri wanatoa order kupeleka kwa Wakurugenzi na Wakurugenzi hawatekelezi, hili jambo linaumiza sana na wala siyo jambo la kushabikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi 2016 humu wakati tunachangia bajeti tulisema kitendo cha Wakurugenzi kuwa wateule wa Rais italeta contradiction kwenye Utumishi wa Umma, tulisema humu na mkichukua Hansard mtaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mkurugenzi hamuheshimu Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye aliyemteuwa ni Rais na Waziri kateuliwa na Rais na inawezekana ndani ya Chama yeye ni kada mkubwa anawadhifa mkubwa kuliko Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo anaona kwamba mimi ni kada mkubwa na mimi nimeteuliwa na Rais huyo huyo aliyemteua yeye inakuwaje katika mazingira ya kawaida Mkurugenzi anapelekewa order na Mheshimiwa Waziri na hatekelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa eti Mheshimiwa Waziri ambaye amedharauliwa kaka yangu Mheshimiwa Kigwangalla, sisi tunakutetea wewe ili ufanye kazi vizuri na wewe unakuja kutetea ulivyodharauliwa! Wabunge hatupendi kuona Waheshimiwa Mawaziri mnadhalilishwa hatupendi kuona mnatoa order ambazo Wakuu wa Mikoa ama Wakurugenzi hawataki kuzitii. (Makofi)
Najua kwamba najadili bajeti za Ofisi ya Rais, Mheshimiwa Mpango hili nalielekeza moja kwa moja, Waislamu mwezi huu tunaita mwezi wa Rajab, tuko kwenye mwezi wa mfungo kumi, tunakaribia kabisa kuingia kwenye mwezi Mtukufu wa Ramadhan kufunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuulize Mheshimiwa Mpango, hivi Serikali hii itashindwa kuongoza, mtashindwa kukusanya kodi ikiwa tu mmeachia tende ziingie bure ikiwa tu tende peke yake mtaziruhusu ziingie bila kodi mtashindwa kuongoza Serikali? Kenya tende zinaingia free, Mozambique tende zinaingia free, Zanzibar wana mwaka wa saba tende free, huku Bara tende zinatozwa kodi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme inawezekana hamtuelewi tukisema kwamba, moja ya nguzo kubwa kabisa za Uislam ni kufunga na tunapofunga kuna sunna na kuna mambo ya faradhi. Jambo kubwa katika sunna katika funga ya Ramadhan ni Muislam kufungua kwa kutumia tende, leo tende mnaitoza kodi, hivi Kenya na wenyewe hawatozi kodi tende, Mozambique hawatozi kodi tende, Zanzibar hawatozi kodi tende na ninyi hapa jamani hamuoni aibu au ndiyo yale aliyosema bwege Waislamu hawana wa kuwasemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.