Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia katika Wizara ya Afya. Kwanza nianze kuipongeza Serikali yote kwa ujumla wake, nimpongeze Rais kwa kuweka nguvu za makusudi kabisa kuboresha Wizara ya Afya. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Naibu wake, tunaona matunda yao wanayoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mambo yangu ya Mkoa wa Tabora kwanza. Kule Tabora tulikuwa tumejengewa Chuo cha Madaktari. Chuo kile kilikuwa kimekamilika kwa asilimia 90 kuanzia mwaka 2014 mpaka magodoro yamo ndani ya chuo hicho, lakini mpaka sasa chuo hicho kimebakiza asilimia 10 tu kumaliziwa toka mwaka 2014 mpaka sasa hakijamaliziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu kitu hiki sasa kinaenda chini ya Wizara yake, jengo lile linaharibika, pesa haionekani thamani yake kwa sababu jengo limeanza kupasuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumejengewa jengo la kisasa la upasuaji, jengo lile limekamilika kila kitu ndani toka mwaka 2014, mkandarasi hajalipwa pesa yake, amelifunga na kufuli jengo lile halitumiki, ukizingatia Hospitali ya Kitete ni Hospitali ya Rufaa, jengo letu la upasuaji ni la kizamani, halina vifaa vya kisasa. Jengo la kisasa tunalo, mkandarasi amelifunga.

Nawaomba Wizara wakae na mkandarasi waongee naye wampe ahadi, lifunguliwe jengo lile lianze kutumika, lina kila kitu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kuhusu madaktari; Tabora hatuna Madaktari Bingwa. Ikama yetu ya Mkoa wa Tabora, tunatakiwa tuwe na Madaktari Bingwa 21, lakini sasa tuna Madaktari Bingwa watano tu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie. Pia tuna madaktari watatu wa kujitolea, wanafanya kazi nzuri sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati wa kuajiri asisahau kutupa nafasi hawa madaktari wanaojitolea mpaka leo hii, wanatufanyia kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wauguzi tunatakiwa tuwe nao 185, tunao 120. Tunaomba sana wakati wa kuajiri wauguzi watukumbuke. Tunasomesha Madaktari Bingwa watano, tunaiomba Wizara, madaktari hawa wakitoka kusoma, msije tena mkawahamisha mkawapeleka sehemu nyingine. Tunaomba mtuachie na sisi waweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba pia kuongeza majengo kwenye Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa, majengo yake ni machache, population ya mkoa imeshakuwa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi tena kuipongeza Wizara ya Afya kwa kazi kubwa wanayofanya. Nashangaa tu mtu anaposema kwamba sisi tunajifanya kusaidia wanyonge, Serikali inajifanya ya wanyonge, lakini siyo kweli ya wanyonge. Hii Serikali ni ya wanyonge. Niwakumbushe kidogo tu, tulikuwa tuna bajeti ya shilingi bilioni 30 mwaka 2015; leo tuna bajeti ya shilingi bilioni 270 kwa ajili ya madawa. Yote hii ni juhudi za Mheshimiwa Rais kuhakikisha watu wake wanapata tiba za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunatibu watu bure. Wagonjwa wa UKIMWI wanatibiwa bure, wagonjwa wa TB wanatibiwa bure, wazee wanatibiwa bure, akina mama wajawazito wanatibiwa bure, watoto chini ya miaka mitano wanatibiwa bure. Zote hizi ni gharama kubwa zinazobebwa na Serikali ya Awamu ya Tano, watu wanasahau hivi vitu. Kila siku wanakuwa wanapenda kulaumu tu, hawapendi kuona mambo mazuri yanayofanywa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo kazi ndogo, tuna wagonjwa wa UKIMWI wangapi? Leo Serikali ikisema wagonjwa wote wa UKIMWI wanunue dawa, ndugu zetu wangapi wataangamia? Naomba sana kuipongeza Serikali na kuitia moyo iendelee kufanya kazi kama inavyoendelea kutufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Ruge alivyokuwa anasema kwamba vifo vya wajawazito takwimu zake ni za mwaka 2015/2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii imewekeza sana kwenye zahanati na vituo vya afya. Ninaamini taarifa itakayokuja haitakuja na vifo hivyo vya akina mama wajawazito na watoto, naamini taarifa itakuwa imeboreshwa. Tumesikia taarifa ya Mheshimiwa Waziri, tumesikia taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati jinsi Serikali ilivyowekeza kwenye Wizara ya Afya.

Kwa hiyo, nataka niwaambie kwamba hiki kitu hakitaendelea kuwa hivi, kazi iliyofanyika ni kubwa.

T A A R I F A . . .

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa siikubali kwa sababu mimi kwenye Mkoa wangu wa Tabora akina mama wanatibiwa bure. Mheshimiwa Waziri alisema yeyote anayetaka kujiboresha zaidi ile kit ilikuwa ni kubwa, ina vitu vingi, anaweza akachukua kwa shilingi 21,000 lakini siyo kusema kwamba watu hawatibiwi bure. Wajawazito wakienda Kitete Hospitali wanazaa bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sikubaliani na alilolisema Mheshimiwa Owenya. Kama yeye Kilimanjaro wanazaa kwa pesa na watoto wanatibiwa kwa pesa, basi ni kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Ruge aliongelea kuhusu Azimio la Abuja akisema kwamba pesa tulizozitenga ni chache. Nasema hivi ameangalia kwenye Fungu 52, lakini pesa za matibabu ziko pia kwenye fungu la TAMISEMI.

Ukichukua TAMISEMI, ukichukua na Wizara ya Afya ukajumlisha utapata pesa nyingi zilizotengwa kwa ajili ya Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona makelele, ujue jua limewapiga kichwani. Kwa hiyo, hata huwa hainisumbui kwanza.

T A A R I F A . . .

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Esther nakusheshimu na unajua nakuheshimu, tafadhali. Nimesema kwamba takwimu alizozitoa Mheshimiwa Ruge asilimia tatu siyo sawa. Ukichukua TAMISEMI, Afya, ukichukua na Fungu 52 huwezi kupata asilimia tatu, utapata zaidi ya asilimia tatu, ndicho nilichokisema, siyo kwamba nilichokisema sikijui. Nakijua na ninakifahamu. Narudia kusema, nakusheshimu sana Mheshimiwa Esther. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee tena jambo moja ambalo limekuwa sana kwenye mjadala. Binafsi kama Munde na ni Mbunge wa wanawake siliungi mkono, naomba niseme wazi. Kumekuwa na mjadala wa kuiomba Serikali igawe taulo za kike bure, mimi siungi mkono na sababu ninazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa, Mheshimiwa Rais anajenga barabara, anasomesha watoto bure, madawati bure, kila kitu bure, tunataka tupelekewe na pads bure! Kwa sasa bado nchi yetu haijafikia, tuache Serikali ijikite kwenye kazi inazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nitaunga mkono kama mkisema tupunguze kodi kwenye hizi taulo ili watu wazinunue kwa bei rahisi. Bado hatujafikia kugawa taulo hizi bure, uwezo huo hatuna. Tusitake kuijazia Serikali mambo mengi, kesho na kesho kutwa tukaanza kuja kuwahoji mbona hili hamjalitimiza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wale wote wenye kuwa na hiyo azma ya kupewa taulo bure, mimi nasema sitaunga mkono, naendelea kupinga na nitaendelea kupinga siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameshatusomeshea watoto wetu bure, nasi kama wazazi tuwajibike; tuna sababu ya kuwajibika. Hatuwezi kutegemea kila kitu kiwe bure kwa Serikali. Hata Uingereza hawatoi hizo taulo bure. Kwa nini sisi kila kitu tunataka bure? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kusema, naendelea kuipongeza Serikali.