Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Yosepher Ferdinand Komba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kwa kumkumbusha dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mbunge mwenzangu wa Mkoa wa Tanga, mwaka 2016/2017 kwenye bajeti aliahidi katika Wilaya ya Muheza, Hospitali Teule ametenga milioni 20 kwa ajili ya gari la wagonjwa, lakini mpaka hivi ninavyoongea halijafika. Sasa ningeomba atakapokuwa anahitimisha atuambie hilo gari limekwamia wapi kwa sababu Wilaya ya Muheza Teule tuna shida kubwa sana ya gari la wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu kwenye Wilaya ya Muheza, kuna upungufu wa watumishi wasiopungua 117 katika Wilaya ya Muheza, lakini pia kuna upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba. Tuna tatizo kubwa la dawa kuwa ghali, hasa dawa ya nyoka na dawa ya mbwa. Wananchi wanaopata matatizo haya wamekuwa wakitibiwa kwa sindano moja Sh.250,000 ya nyoka na inatakiwa sindano tatu na kama hauna kunakuwa hakuna msamaha katika hilo. Wameshapoteza maisha wananchi wasiopungua watano katika Hospitali Teule kwa sababu ya tatizo hili la kuumwa na nyoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri alione hili kama ni ajali kama ajali nyingine. Wananchi ambao wanapata tatizo la kuumwa na nyoka au na mbwa wawe wanatibiwa bure kwa sababu wanakuwa hawajajiandaa na hili tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine napenda kuongelea haki na maendeleo ya watoto. Tunajua watoto wana haki zao, tunajua watoto wanatakiwa watunzwe mpaka kufikia umri fulani ambao wanaweza kujitambua. Haki ya kwanza ni haki ya kiliniki. Tumeshuhudia na kama Waziri na Wizara yake wafanye utafiti waone, watoto wengi wanapoachishwa kunyonyeshwa kati ya miaka miwili mpaka miwili na nusu wanakosa haki ya kuendelea na kiliniki. Watoto wengi wanabaki nyumbani wakati Sheria ya Afya inataka waende kiliniki mpaka miaka mitano. Kwa hiyo nimwombe Waziri kupitia Wizara yake waandae mkakati wa kufumbua hili suala. Watoto wengi wanabakia nyumbani kati ya miaka miwili na mitano wanapata magonjwa ambayo mwisho wa siku yanawasumbua kutibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haki nyingine ya watoto hawa ni makao na vituo kwa wale ambao wamekosa malezi ya wazazi wao. Nimeangalia takwimu za kwenye taarifa yako ya leo, kuna vituo 157, kituo kimoja tu ndicho kinamilikiwa na Serikali. Kwa hiyo wanataka kusema Serikali hawako serious na hili suala? Kama wanawaachia watu binafsi ndio wawe wanahangaika na watoto ambao wanatelekezwa, watoto wenye matatizo kwenye jamii, Serikali wana kituo kimoja tu kiko Kurasini, vituo 156 vinamilikiwa na watu binafsi. Hata hivyo, hawa watu binafsi hawawapi nafasi ya kutosha na kuwa-support ili waweze kuanzisha hivi vituo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kusajili vituo vya watoto yatima na watoto wenye mahitaji ni mgumu kwa watu binafsi, ni mgumu sana. Una mahitaji mengi sana kiasi kwamba mwenye nia anaishia njiani. Kwa hiyo niombe haki hizo za watoto zizingatiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine nataka kuongelea hapa. Sisi katika Wilaya ya Muheza tuna ujenzi wa hospitali ya wilaya katika Kata ya Lusanga, wananchi mpaka dakika hii wamejitoa kwa nguvu zao na mali zao kwa kiasi kikubwa, tuna michango ya kila kata kwa ajili ya hii hospitali. Tumeona imetengwa 1.5 billion, its ok, tunaomba kutenga huku kusiishie kwenye kitabu. Tunaomba hizi hela zifike Muheza tukajenge hospitali ya wilaya kwa sababu hospitali tuliyokuwa nayo tunachangia na kanisa lakini pia bado haikidhi mahitaji. Kwa hiyo niombe 1.5 ifike kwa wakati isije ikapotelea njiani kama vile ambavyo tunatafuta 1.5 trillion kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kuzungumzia, tunao ujenzi wa Chuo cha Utafiti kule Amani, ilizungumzwa sana na viongozi wameahidi sana kipindi cha kampeni lakini mpaka sasa hivi na nimepitia humu sijaona chochote ambacho kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hiki Chuo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu. Tunayo NIMR iko kule lakini bado inashindwa kufanya kazi inavyotakiwa kwa sababu ya ufinyu wa maeneo. Waliahidi watajenga chuo kingine, tunaomba hilo suala Mheshimiwa Waziri atakuja kuniambia ni lini wtaanzisha ujenzi wa hiki chuo kwa sababu tunakihitaji sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine; kuna kituo cha wakoma narudi tena, Kituo cha Wakoma kule Tononoka Ngomeni. Ugonjwa ambao unaanza kuonekana kama vile haupo lakini unazidi kukithiri, ugonjwa ambao dalili zake zinaonekana kuanzia miaka mitatu mpaka thelathini, ugonjwa ambao ukikupata unapata ulemavu wa viungo unapata na upofu, ugonjwa ambao unaongoza kwa kutengwa na jamii. Tunacho kituo kule kina hali mbaya kina wazee, kina wanawake, kina watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara yake, kwanza, wale wanawake wanahitaji kuinuliwa kiuchumi, lakini pili, wale watoto wanahitaji kupata mahitaji yao ya muhimu ya afya, tatu, wale wagonjwa wanahitaji kupata tiba na huduma zingine za afya, kwa wakati na kwa usahihi, lakini lishe ni tatizo na matatizo mengine naomba ni…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)