Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia leo kusimama katika Bunge lako hili kupata fursa ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu naomba pia niwashukuru akinamama wenzangu walioniwezesha kuingia katika Bunge hili, naahidi kuendelea kushirikiana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, dada yangu Ummy, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara. Nawapongeza hawa nafahamu sana umuhimu wa Wizara ya Afya kwa Watanzania. Kazi inayofanyika na dada yangu Ummy na Naibu Waziri ni kazi nzuri sana inapashwa kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kwa kuzungumzia masuala muhimu ambayo nakusudia kuyasema kwa siku hii ya leo. Niendelee kutoa pongezi. Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 mnamo tarehe 6 Agosti, nilitembelea Wilaya yangu ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma. Nilishuhudia tukiwa tunapokea vifaa mbalimbali ikiwemo vitanda na vifaa vya upasuaji. Naomba sana nipongeze jitihada za Serikali hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Imepelekea kufikia sasa kupata akina mama waliofanyiwa upasuaji kufikia 87.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni jitihada nzuri ya kuonesha kwamba tunaokoa maisha ya akinamama na watoto. Hata hivyo, liko tatizo kubwa katika hospitali ile, tatizo la X-ray. Nimwombe dada yangu Ummy amefanya mambo mazuri sana, naamini x-ray ni jambo dogo tu atalikamilisha, atujalie tupate x-ray katika hospitali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la vifo vya akinamama wajawazito. Tunapozungumzia vifo vya akinamama wajawazito ziko changamoto nyingi ambazo zinapelekea kupatikana kwa vifo vya akinamama wajawazito. Mojawapo ya mambo ambayo yanayojitokeza ni umbali wa eneo la kujifungulia, vifaa tiba na wauguzi. Nafikiri hivyo ni miongoni mwa vitu ambavyo vinatakiwa viwepo kwenye hospitali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la umbali wa eneo la kujifungulia kama nitakuwa na kumbukumbu nzuri kupitia ahadi za Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi tuliahidi kuwa na zahanati kila kijiji na kuwa na kituo cha afya kila kata. Niombe dada Ummy atakapofika basi atueleze, mimi kama mwakilishi wa akinamama wa Mkoa wa Ruvuma napenda kujua tumefikia hatua gani katika kuhakikisha ahadi hizi zinatekelezwa ipasavyo; na kupitia hivyo vijiji pia nitapata fursa ya kuona ni vijiji gani sasa kwenye Mkoa wangu wa Ruvuma tumefanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la wauguzi. Wachangiaji wengi wamesema kwamba tunalo tatizo la Ikama ya watumishi. Ziko zahanati ambazo mpaka leo ukienda unaweza ukakuta mhudumu mmoja tu. Nesi afanye kazi ya kuandika huyo huyo, nesi aende akampime mama mjamzito, nesi aende akazalishe mama mjamzito, nesi aende akatoe dawa. Kwa hiyo jambo hili ni muhimu sana niombe tuangalie sana katika suala hili la Ikama ya watumishi. Kwa bahati nzuri kupitia vitabu hivi wameeleza, kitabu cha Waziri amesema, kupitia zoezi lile la vyeti feki na mambo mengine ambayo yamejitokeza watumishi wengi sasa hawapo kwenye zahanati zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kuna usemi unasema ukikata mti panda mti, kwa hiyo tumaini langu kwamba tumewatoa wale watumishi ambao tunafikiri kwamba wa likuwa na makosa kwa namna moja au nyingine, ni wajibu wetu sasa kuona nafasi zile tunazifidia katika kutoa huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la upatikanaji wa dawa. Wamezungumza kupitia kwenye vitabu lakini nishukuru maoni ya Kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii kupitia ukurasa wa 35, wamesema na wametoa mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye vitabu hivi unaona kabisa kwamba sasa suala la dawa si tatizo katika nchi yetu, lakini ukienda katika hali halisi yako maeneo mpaka hivi tunavyozungumza yana upungufu mkubwa sana. Wajumbe wa Kamati kupitia maoni ya Kamati wamesema ni vizuri sasa kama Wizara waweke utaratibu wa kuhakiki kuona hizi dawa zinaishia wapi kama kweli zinafika kwa watumiaji. Ni tatizo kubwa sana la upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili, Mheshimiwa Waziri Mkuu bahati nzuri alifanya ziara Mkoani kwetu Ruvuma, lakini miongoni mwa mambo ambayo alikumbana nayo ni upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kufanya mkutano katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilisikitisha sana pale alipomwomba Daktari aeleze dawa zilizopo. Vile alivyojaribu kumweleza wananchi walimzomea sana. Hii ni kuonesha kwamba hizi dawa tunazozungumza kwenye makabrasha pengine sio zile zinazofika moja kwa moja kwa wananchi. Niombe sasa Serikali yangu, naamini hii ni Serikali sikivu sana ione hivyo.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna njia nyingine yoyote, sisi uwepo wetu hapa umetegemea na afya zete; kama tusingekuwa na afya njema tusingekuwepo humu ndani leo. Sasa kuwepo na dawa itarahisisha sana kuona matibabu yanapatikana haraka sana. 0525

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala lingine la matibabu ya wazee. Naomba niseme; kwamba suala hili la matibabu ya wazee tumelisemea sana lakini mimi naweza nikaona halijasimamiwa ipasavyo. Hawa wazee tunaowazungumzia wanapokwenda kwenye hospitali si tu kuandikiwa dawa ni pamoja na kupata dawa. Kwa hiyo niombe huu mfumo ambao tunakusudia kutoa matibabu kwa wazee uzingatiwe vizuri ili wazee wale wafaidike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu naamini na sisi wote ni wazee watarajiwa. Kwa hiyo tukiweka misingi mizuri leo hata sisi Mwenyezi Mungu akitujalia tukafika huko uzeeni tutanufaika na hii mipango ambayo tumekuwa tukiiweka. Nimwombe sana dada Ummy kwa kazi nzuri anazozifanya anawapigania akinamama lakini anazungumza sana suala la wazee, basi tuhakikishe wazee hawa wanapata huduma ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la vituo vya afya. Sisi katika Halmashauri yetu ya Tunduru; naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru kupitia wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge; tumejitahidi pale katika kuhakikisha ujenzi wa kituo cha afya unaendelea. Hata hivyo, tuiombe sasa Serikali kuweka msukumo. Kama mnavyofahamu nguvu za wananchi peke yake zinaweza zisitoshe, kwa hiyo tunaiomba Serikali iangalie katika kuona tunaboresha kile kituo cha afya ili tuendelee kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kituo hicho cha afya ambacho nimekizungumzia kilichopo Kata ya Nakayaya pia naomba kituo cha afya kilichopo Kata ya Narasi. Pale tuliahidiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, naamini Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete hayupo lakini Serikali ya CCM ndiyo iliyopo madarakani. Tuliahidiwa pale kupata kituo cha afya; na kwa kweli ukiangalia na idadi ya watu waliopo pale tunastahili. Niombe sana katika kutekeleza jambo hili wakati utakapofika tunapoona umuhimu wa kuongeza vituo vya afya basi na kile kituo kipewe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la CHF; limezunguzwa kwenye vitabu na sisi sote tunalifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukihimiza sana wananchi wetu kujiunga na CHF, na bahati nzuri dada Ummy amelizungumza kupitia kitabu chake; kwamba wanakusudia kuwa na CHF ya pamoja ambapo mgonjwa itamwazesha kutibiwa kutoka kwenye kituo cha afya, atatibiwa hospitali ya wilaya na vile vile atakwenda kutibiwa mkoani. Naomba katika kutekeleza hili tuangalie na changamoto zilizojitokeza. Inawezekana tukawa tunaangalia tulipoanguka lakini tukasahau tumejikwaa wapi, hatimaye tumeanguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu watu wengi wamekuwa wakisita kujiunga na CHF kutokana na huduma zinazotolewa. Mtu anajiunga kwenye CHF anapopata tatizo akienda kwenye zahanati hakuna dawa, hilo limekuwa tatizo. Sasa kwa kuwa tunakusudia kuwa na CHF ya pamoja, basi ni vizuri tukaangalia changamoto ambazo zimejitokeza katika mfumo huu tulipoanza nao ili tuboreshe ili wananchi wetu waweze kupata huduma zinazostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo jema na wengi kwa kweli walikuwa wakikata tamaa. Kwa mfano sisi katika Halmashauri yetu ya Tunduru ni wakulima wa korosho. Mtu anaweza akatoka Nalasi anakuja Makao Makuu ya Wilaya kuja kupokea pesa yake, lakini akiwa pale anapata tatizo la ugonjwa, CHF inafanya kazi katika zahanati yake, makao makuu ya wilaya haifanyi kazi. Kwa hiyo tukiweka mfumo mzuri itawasaidia, kwamba wanapopata matatizo hata kwenye hospitali za wilaya wanapata kutibiwa lakini watakwenda pia kutibiwa hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kusisitiza suala la upatikanaji wa dawa kama nilivyosema, ni kitu muhimu sana, naomba Mheshimiwa Waziri dada Ummy akizingatie sana. Inawezekana pengine taarifa hizi wanazozipata kupitia ngazi za mkoa zisiwe sahihi. Tukija kule kwenye maeneo yanayohusika pengine ile hali sivyo ilivyo, kwa hiyo nasisitiza jambo hili...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.