Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya njema na kuweza kusimama Bungeni hapa leo na kuweza kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa hotuba yao nzuri ambayo wameiwasilisha leo. Napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutupatia gari la wagonjwa katika Kituo chetu cha Afya Nyang’hwale. Mwaka 2017 tulipata gari moja na nashukuru mwaka huu tumepata gari lingine, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nyang’hwale kituo cha Afya na Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale, ama Wilaya ya Nyang’hwale kwa ujumla tuna upungufu mwingi katika vituo vyetu vya afya na hospitali. Upungufu wenyewe ni kama ufuatao:-
Tuna upungufu wa dawa, Wauguzi, Madaktari na vifaa tiba. Vifaa tiba kama vile X-ray na Ultra Sound. Upungufu huu unasababisha wananchi wetu kupata usumbufu mkubwa kufuata huduma hizi Mkoani Geita. Kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia upungufu huu ili kuwapunguzia adha wananchi wetu kufuata matibabu Mkoani Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bima ya afya. Watu wengi wamekuwa hawaoni faida ya bima ya afya sababu ni ipi. Sisi Wabunge tunajitahidi sana kuwahimiza wananchi wajiunge na bima ya afya, lakini wanashindwa kujiunga kwenye bima ya afya kwa sababu kwa wananchi ambao wameshajiunga na bima ya afya hawaoni faida yake. Vipi hawaoni faida yake? Ni kwamba wanapokwenda hospitali wanapata huduma, lakini huduma ya dawa wanakuwa hawaipati wanaambiwa waende wakanunue dawa hakuna dawa. Kwa hiyo hii inawafanya wananchi wakate tamaa kubwa ya kujiunga na huduma hii ya bima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alifika katika jimbo letu na akaahidi Kituo cha Afya cha Kalumwa kiwe hospitali ya wilaya, lakini mpaka leo hii hatuoni mpango wowote wa Wizara kutupa hati ya kuipandisha hadhi kukipandisha hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa hospitali hii ipandishwe hadhi ili tuweze kupata dawa kulingana na wilaya; kwa sababu hospitali hiyo inahudumia vijiji zaidi ya 110, lakini pia wilaya za jirani zinakuja kupata huduma katika hospitali hiyo. Kwa hiyo kituo hicho kitakapopandishwa na kuwa hospitali ya wilaya naamini kabisa bajeti yake itakuwa ni kubwa na inaweza ikakidhi angalau kidogo kupunguza makali ya mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba wizara ijaribu kuangalia. Tuna wodi moja pale ambayo ilijengwa mwaka 1958. Wodi ile inalaza wagonjwa 10 tu na leo hii hospitali ile inapokea wagonjwa wengi sana. Kwa hiyo tunaomba sasa tuweze kujengewa wodi ambayo ni ya kisasa na inaweza kubeba wagonjwa walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa mikakati yake ya kupambana na ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi. Ukweli ni kwamba naipongeza Serikali kwa kuanza kutoa chanjo kwa ajili ya kukinga tatizo hilo. Pia naomba sasa Wizara ishuke kule chini iende kutoa elimu ili kuondoa ile imani potofu waliyonayo wananchi wetu, kwamba tutakapochomwa sindano hiyo huwezi ukapata tena mimba, wengi wanaelewa hivyo, kwa hiyo naomba elimu hiyo iende ikatolewe kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waswahili wanasema kinga ni bora kuliko kutibu. Kwa nini nasema hivyo; Wizara imeshagundua tatizo la chanzo cha ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi. Jana nilisikia kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri hapa alisema kwamba chanzo chake ni kwamba inatokana na kuambukizwa na wanaume ambao hawajakata govi zao. Kwa hiyo naiomba sasa Wizara iende ikatoe elimu kwa walio na govi hizo ili waweze angalau zitolewe kuwakinga hawa. Kwa lugha nyingine wanaume ambao hawajafanyiwa tohara. Kwa hiyo naomba itolewe elimu kule ili kuweza kuwakinga hawa akinamama na maambukizi haya ambayo yanatoka kwa akinababa ambao hawajafanya tohara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.