Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nachangia kwa niaba ya Mheshimiwa Selemani Zedi na jina langu lipo huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia Wizara hii ya Afya, napenda kuishukuru sana Serikali kwa Mkoa wangu wa Mwanza, wametupa shilingi bilioni tatu na tumeweza kufanyia ukarabati Vituo vya Afya zaidi ya saba kikiwemo Kituo cha Kahangara (Magu); Karume (Itemela), Kome (Buchosa); Kagunga (Serengema), Mallya (Kwimba), Lugeye (Magu) pamoja na Misungwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kwa kuweza kutoa fedha hizi ili kuweza kuboresha huduma ya afya katika Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kuchangia katika suala la saratani ya shingo ya uzazi. Ni jambo jema kwamba Serikali sasa imeleta chanjo ili kuwachanja watoto wenye umri wa miaka 14. Naomba kuishauri Serikali kwamba sasa iangalie kwenda kwenye phase II ambayo ni ya watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 15 mpaka miaka 25. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kuishauri Serikali kuangalia ni namna gani wanaweza wakaanza pia na watoto wenye umri wa miaka tisa, kumi na kuendelea mpaka hiyo 14. Kwa sababu gani naishauri Serikali kufanya hivyo? Umri wa miaka tisa mpaka 14 watoto wetu sasa hivi wameanza kuingia katika masuala ya kujamiiana mapema sana. Ni vyema sana kuwakinga ili kuwaepusha kupata saratani ya shingo ya uzazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, saratani ya shingo ya uzazi inaambukizwa kwa magonjwa ya kujamiiana. Kwa hiyo, nashauri sana watoto wetu kuanzia miaka 9 hadi 14 na wao pia Serikali iwaangalie ni namna gani wanaweza wakawapatia chanjo. Pia watoto wa kiume wanaweza wakapatiwa chanjo ya Gardasil pamoja na Gardasil 9 ambayo inaweza ikawasaidia kuwakinga watoto wa kike wasipate maambukizi ya kujiamiiana na hatimaye kupata saratani ya shingo ya uzazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuongelea suala la ugonjwa wa myoma. Ugonjwa wa myoma ni ugonjwa ambao unawapata akina mama, wanapata uvimbe katika kizazi na inapelekea wanawake kutolewa kizazi na hatimaye kukosa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kuweza kusaidia kufanya utafiti wa ugonjwa huu kwamba upo kwa ukubwa kiasi gani? Kuna siku utakumbuka katika Bunge hili wanawake wote walisimamia kuchachamaa kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya wa kipindi hicho alisema ugonjwa huu siyo mkubwa na siyo hatarishi. Wanawake wote humu ndani walishangaa na wakanyanyuka. Ninaomba Serikali iweze kufanya utafiti wa ugonjwa huu wa myoma kwa sababu ni ugonjwa ambao unawamaliza sana wanawake, wanakosa watoto katika umri mdogo sana kuanzia miaka 25 hadi 35. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuongelea suala la utoaji huduma wa afya kwa akina mama wajawazito kuhusiana na suala la delivery packs. Serikali ilizitoa delivery packs bure kwa mwaka mmoja tu na baada ya hapo wanawake wengi tumekuwa tukiuliza maswali ndani ya Bunge na kujibiwa kwamba delivery packs zinakuja. Serikali cha kusikitisha sana delievery packs sasa tumeambiwa kwamba zinauzwa na bahati mbaya sana zinauzwa shilingi 21,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake huko vijijini hawana uwezo wa kununua hizi delivery packs kwa bei hiyo. Ninaiomba Serikali irudie kuangalia upya gharama za bei ya delivery packs angalau basi zishuke bei hadi kufikia shilingi 10,000. Kwa sababu kwenye pharmacy nyingine huko mjini wanauza shilingi 10,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la delivery packs siyo la muhimu sana. Tunatarajia mama mjamzito anapofika hospitali, kuna delivery kit ambapo nurse anapotoka kwenda kumhudumia huyu mama wakati anajifungua, anapoenda kufanya ile procedure, anaondoa vifaa vinavyohotajika kutoka kwenye delivery kit ili apate delivery pack aende kumsaidia yule mama aweze kujifungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona hili suala la delivery packs sio la lazima sana Serikali kutoa bure, lakini waangalie ni namna gani wanaweza wakapunguza bei ili wale wanaoweza kununua waweze kununua.
Mheshimiwa Naibu naunga mkono hoja. Nashukuru.