Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na rehema kwa kutupa uhai, sisi wote hapa Bungeni ni wazima na tunasikiliza Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda kumpongeza Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa kazi nzuri wanayoifanya. Napenda kuwapongeza Mawaziri wote kwa kazi nzuri wanazozifanya kutumikia Taifa hili. Napenda kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya za kuwanyanyua wanyonge na kuleta heshima ya kazi ndani ya Taifa hili. Zamani kazi ya Serikali ilikuwa inadharaulika na Manesi hawa walikuwa na lugha mbaya lakini sasa hivi wana lugha nzuri, Mheshimiwa John Pombe Magufuli usi-change gear ongeza gear nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda niende kwenye Mkoa wangu wa Katavi, napenda nishukuru kwa pesa tulizopata kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mkoa, naomba muuangalie kwa jicho la pekee mkoa huu kwa sababu mkoa huu ni mpya, naomba mtuongezee pesa kwa sababu sisi ndiyo tunaanza kujenga hospitali. Mkoa huo ni mpya, miundombinu ni mibovu, kwa hiyo, watu wote wa Mkoa wa Katavi wanasubiri Hospitali ya Mkoa iweze kuisha ili iweze kuwasaidia maana yake Hospitali ya Rufaa iko mbali Mkoa wa Mbeya ni kilometa 500 kutoka Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo hitaji lingine la Mkoa wa Katavi tunaomba gari la chanjo kwa Manispaa ya Mpanda. Manispaa ya Mpanda haina gari la chanjo, Halmashauri zingine zipo, kwa hiyo, inawafanya watoto pale wadogo wale wanaozaliwa kwenye Manispaa ya Mpanda waweze kukosa huduma ya chanjo. Namuomba Mheshimiwa Waziri utupatie gari hilo la chanjo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine ni kile kituo cha afya ambacho kilikuwa kinafanyiwa marekebisho pale kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kiweze kufunguliwa, ninazo taarifa kwamba Mheshimiwa Ndugulile ulikwenda Kakuni ukakagua ile shule ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo amejenga pale Kakuni, ametupatia sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi ifunguliwe iwe kituo cha afya.
Nimuombe basi Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa sababu ulikwenda pale Kakuni na ukaiona hiyo shule, ufanye uharaka wa kukamilisha hili jambo ili kituo hicho cha afya kiweze kufunguliwa na kile kituo cha afya cha zamani kiweze kutumika kwa akina mama wa Mpanda pamoja na watoto kwa maana ya kuwa kliniki ya watoto. Naomba hilo Mheshimiwa Ndugulile kwa sababu jambo hili unalifahamu na Kakuni ulifika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu kwa kutupatia hiyo shule ambayo alikuwa ameijenga kijijini kwake, ahsante sana kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine la wananchi wa Mkoa wa Katavi kuhusu afya, tunaomba ile Hospitali ya Inyonga bado haijapewa hati ya kuwa Hospitali ya Wilaya, tunaomba ipewe hati ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wa Mlele.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine kwa sababu dakika ni tano naenda u upesi, ombi lingine la wananchi wa Mkoa wa Katavi wazee wa Mkoa wa Katavi wanaomba sana wapewe bima ya afya. Sasa hivi wale wazee huwa wanapigwa picha wanapewa vitambulisho wanakwenda kutibiwa kwenye dirisha la wazee lakini wanapokosa zile dawa pale hospitali hawawezi kuzipata zile dawa kwa sababu hawana bima ya afya. Nimeangalia pale Manispaa ya Mpanda mmewapatia shilingi milioni saba, kwa ajili ya wazee wa Manispaa ya Mpanda na wao waliomba shilingi milioni 17, lakini mimi nasemea wazee wote wa Mkoa wa Katavi muwaangalie kwa jicho la pekee. Mkoa ni mpya ndiyo unaanza, una mahitaji mengi na wale wazee wa kule hawajafaidika na hii bima ya afya, nawaombea wazee wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuiomba Wizara ya Afya ninaomba Mkoa wa Katavi mtupatie wadau wa afya. Tunaye mdau mmoja anaitwa Water Rid yeye ndio yuko Mkoa wa Katavi anatusaidia saidia tunamshukuru sana, tunaomba mnapopata wadau wa afya wengine huko Wizara ya Afya muwalete Mkoani kwetu Katavi ili waweze kutusaidia kwenye sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri wa Afya pia nizungumze suala dogo kuhusu usafi ambalo limezungumziwa pia na mwenzangu aliyepita Mheshimiwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja hundred percent.