Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi fursa ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma hotuba hii yote kwa ujumla imeonesha kama vile yaani Tanzania kwenye mambo ya barabara na nini hakutakuwa na tatizo lolote, ndiyo hotuba nzima ilivyokuwa imeonesha. Lakini nitatumia kama dakika mbili kuelezea Jimbo langu la Momba halafu mengine ntayazungumza ya kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza swali hapa Bungeni miaka yote kuhusu kupandishwa hadhi kwa barabara ya Jimboni kwangu Momba kutoka Kakozi – Kapele kwenda Ilonga, Sumbawanga na Serikali ikaniahdi hapa kwamba tutaipandisha hadhi, wakakiri imekidhi vigezo na nini, lakini mpaka leo ile barabara huu ni mwaka wa nne tangu ahadi ya Serikali ndani ya Bunge, haijatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna barabara ya kutoka Mlowo kwenda Kamsamba mpaka Kiliamatundu, barabara ile imekuwa kwenye ahadi ya kila mwaka ukosoma kwenye hotuba hii kila mwaka iko mle ndani kwamba tutaijenga kwa kiwango kinachoridhisha itakuwa na uhakika wa kiwango cha lami, lakini ile barabara imebaki kuwa story ambayo haikamiliki. Kwa hiyo, sasa ukiangalia haya mambo ndiyo inashindwa kuelewa kwa nini Serikali inashindwa kutekeleza kile inachokizungumza kila mwaka kwa sababu imekuwa ikichukua miaka mingi. Sasa hayo ndiyo maeneo makubwa ambayo sisi jimboni kwangu wakati wa sasa ndiyo yanayotusumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nizungumzie mambo ya kitaifa. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ina deal na Shirika letu la Ndege la Taifa. Hivi karibuni ndege yetu ya tatu ya Bombadier imewasili nchini na baada ya kuwasili kulikuwa na taarifa za kukamatwa kwa ile ndege ya tatu, ilikuwa inadaiwa. Hata hivyo pamoja na kwamba imewasili Serikali haijatueleza imelipa kiasi gani kwenye kuikomboa ile ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka majibu kwa sababu zile fedha ni kodi za Watanzania. Masuala kama haya yanapoachwa kimya sisi Watanzania tutaendelea kuyauliza bila kupatiwa majibu kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata taarifa, Mamlaka ya Anga Tanzania pamoja na Shirika la Ndege Tanzania limeondolewa kwenye yale mashirika ya anga (IATA) umesikia hiyo taarifa hivi karibuni, kwa sababu ya madeni na inashindwa kujiendeleza. Sasa haya tunahitaji majibu ili tujue hili shirika letu ni kweli linajiendesha vile inavyotakiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukisikia taarifa zinazotoka Serikali zinaeleza Shirika la Ndege la Taifa kwamba linapata faida; wao wanasema tumepata faida. Nakumbuka mara ya mwisho waliainisha kwamba wamekusanya karibu shilingi bilioni 20, lakini hawatuelezi running cost za ili shirika; hawaelezi wanaendeshaji; maana unatajiwa tu mapato ghafi. Atueleze kuhusu faida iliyopatikana baada ya kuondoa gharama za uendehaji wa shirika. Kwa hiyo tunahitaji kufahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye report ya Kamati ya wakati uliopita ilikuwa inaonesha kabisa kwamba Shirika la Ndege lina madeni makubwa, kuliendesha ni gharama kubwa. Sasa kumekuwa na contradiction kati ya kinachotolewa na Serikali na maelezo yanayokuwa yanatoka kwenye Kamati. Kwa hiyo, jambo hili tunahitaji kupatiwa ufafanuzi ili tuweze kufahamu hivi shirika letu lipo katika kile kiwango tunachohitaji, yaani ili liweze kuendelea na kulishauri vizuri. Kwa hiyo, tulikuwa tunahitaji kupata ufafanuzi kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu kwenye shirika hili la ndege, hatujawahi kuona taarifa ya ukaguzi ya CAG juu ya hili shirika la ndege. Sasa tunahitaji majibu; kuna usiri gani wa kushindwa kuleta taarifa ya CAG ya ukaguzi wa Shirika la Ndege ndani ya Bunge? Tunahitaji hayo ili tuweze kujua namna gani tunaweza tukawashauri, lakini pia tunahitaji kujua hizi kodi za Watanzania zisingekuwa zinapigwa huko kimya kimya halafu sisi watu hatujui; kama ambavyo leo Watanzania wote wanahoji kuhusu zilipo shilingi trilioni 1.5 hatutaki kufika huko na ndiyo maana, Mheshimiwa Waziri atakuja kutueleza hapo kwenye ku-wind up, atueleze kwa nini taarifa zake hazionekani? Yaani zinakuwa ni siri ilihali mradi huu ni kwa maslahi ya Taifa? Tunahitaji majibu juu ya jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka yote upande wa barabara (TANROADS). Wakala wa Barabara kwa miaka ya hivi karibuni tumeshindwa kupata ripoti ya ukaguzi ya TANROADS (Wakala wa Barabara wa Taifa). Tunazitaka hizo taarifa kwa sababu kuu mbili; kumekuwa na maneno uko mtaani watu wananon’gona nong’ona kwamba kulikuwepo na barabara hewa zenye thamani ya shilingi bilioni 252. Sasa unapoelezwa hizi taarifa halafu Serikali inakaa kimya; sisi kama Wabunge jukumu letu kuhoji tunahitaji kupata ufafanuzi ili tujue kweli hiki wanachokizungumza ni kweli ama ni uongo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini CAG haruhusiwi ama taarifa zake haziletwi kwa Wakala wa Barabara wa Taifa? Kwa sababu tunaziona barabara zetu, tunataka kujua value for money ya hizi barabara. Je, barabara inayojengwa thamani yake inalingana na pesa iliyokuwa imetolewa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo majibu ambayo Serikali inapaswa kutuletea sisi Wabunge ili tuweze kuishauri namna ya kuliendesha hili taifa. Kwa hiyo, hilo tunahitaji kufahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine; sasa hivi kuna TARURA. Najua TARURA inategemea Mfuko wa Barabara fedha zake nyingi zote, niseme fedha zote zinatoka kwenye Mfuko wa Barabara. Hata hivyo bado kumekuwa na mkanganyiko, fedha kule kwenye TARURA hazipelekwi. Kuna barabara ambazo kwa sasa TARURA haiwezi kuziendesha. Nataka kujua namna gani ambavyo watu wa TANROADS wanaweza yaani tunatafuta yaani kama ule ushirikiano wa namna kupandisha hadhi zile barabara ambazo TARURA hawawezi, lakini fedha nyingi zimekuwa zikipelekwa upande wa TANROADS kuliko upande wa fedha za miradi ya barabara vijijijini hususani kupitia TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimeona nilizungumzie, najua liko kwenye upande wa TAMISEMI zaidi, lakini wana deal na barabara kwa hiyo unazungumzia barabara lazima kuwepo na connections, kwamba huyu anakuleta kwenye ngazi ya Wilaya na Mkoa huyu anakupeleka kwenye ngazi ya kitaifa zaidi. Kwa hiyo, na hili nilikuwa nataka tupate ufafanuzi kutoka kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Simu la Taifa (TTCL), shirika hili lina miaka mingi lakini ukuaji wake, yaani linakua katika tunasema in a negative growth. Sasa hivi wanasema rudi nyumbani, lakini rudi nyumbani hawana uwezo wa kujiendesha, yaani kwenye Taifa hili wapo kwenye Mikoa kumi tu peke yake. Tuliwauliza hapa siku moja, Halotel amekuja ana muda usiopungua miaka miwili, lakini ndani ya muda mfupi Halotel ana wateja zaidi ya milioni moja. Lakini TTCL lenye miaka na miaka lina wateja hawafiki hata laki mbili, ukiwauliza Serikali wanakwambia hiki ndicho kitu cha kujivunia, hiyo ndiyo changamoto iliyopo kwenye Serikali yetu. Tunataka kuanzisha mambo mengi lakini hatuwezi ku- compete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaambia hapa kwa nini Serikali isikubali kushiriki kwenye ubia wa PPP juu ya namna ya ku-run hizi kampuni. Amekuja Waziri hapa anasema kwenye miradi ya PPP Serikali ya Awamu ya Tano haioni kama ni kipaumbele. Sasa unajiuliza, mtawezaje kuendesha kila kitu kwa gharama ya fedha za ndani? Sasa haya dunia ya sasa huwezi ku-run miradi mikubwa bila kuingia katika mfumo PPP haiwezekani, na bahati mbaya sana Awamu hii ya Tano inafiiri kila jambo linaweze kutekelezeka kwa fedha za ndani, kitu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)