Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo tu katika hizi dakika tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nianze moja kwa moja na usafiri katika Ziwa Victoria. Meli yetu ya MV Victoria iliharibika miaka mitano iliyopita na Serikali imekuwa ikiahidi kutengeneza meli hiyo. Ukitazama hata katika makadirio ya mwaka jana Serikali ilisema katika makisio kwamba ingetoa bilioni hamsini ili kuweza kununua meli mpya lakini pia kufanya matengenezo kwa meli hiyo ya MV Victoria. Pia mwaka huu wametoa bilioni tisa kwenda kutengeneza meli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize tu Mheshimiwa Waziri, hii meli ya MV Victoria ambayo inatengenezwa katika miaka mitano inatengenezwa kitu gani? Kwa sababu inashangaza kwamba meli ambayo inahitajika; kwa sababu sisi watu wa Mkoa wa Kagera ili uweze kusafiri kibiashara na hasa akinamama ambao wanasafirisha ndizi, Avocado na bidhaa nyingine za maharage, wanatumia njia ya barabara, kitu ambacho kwa kweli kinawa-cost na gharama za kuendesha biashara hiyo inakuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba majibu, tunaomba Waziri atuambie, ni lini atatutengenezea hiyo meli wakati tunasubiri meli ile ambayo wamesema kwamba itajengwa? Kujenga meli mpya kunachukua muda mrefu lakini matengenezo ya MV Victoria ni kwa nini yamechukua muda mrefu na kila mwaka wamekuwa wanatenga fedha kwa ajili ya meli hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kitabu cha hotuba cha Mheshimiwa Waziri cha mwaka jana hiki, ukurasa wa 81, alichokisema na hata mwaka huu ameongea lakini hakuna kitu chochote. Hata Watanzania wa Mkoa wa Kagera hawapewi taarifa ni kitu gani kinaendelea kuhusu meli yao ambayo ilikuwa inarahisisha usafiri kutoka Bukoba kwenda Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongelea hiyo nije kwenye TARURA. Japokuwa hii TARURA ipo chini ya TAMISEMI, lakini fedha zake zinatolewa na Serikali Kuu kutoka kwenye Mfuko wa Barabara. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiiomba Serikali, kwamba huu mgawanyo wa asilimia 30 ni mdogo na Halmashauri walikuwa wanashindwa kutengeneza barabara nzuri na zilizo imara. Sasa pesa hiyo hiyo asilimia 30 ndiyo inapelekwa kwa TARURA na huu ni Wakala ambao umeundwa au umeanzishwa ili kuweza kusaidia barabara za vijijini zilizo chini ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara haifikirii namna ya kuongeza pesa kutoka angalau asilimia 30 kwenda asilimia 40 ili TARURA waweze kujenga na kutengeneza barabara; na tukijua kwamba wana mtandao mkubwa wa barabara zilizo halmashauri na kuna maeneo mapya ya utawala ambayo yamekuwepo; tunaomba Serikali ifikirie namna ya kuongeza pesa kwa TARURA au mtindo utakuwa ni ule ule na TARURA watashindwa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi. Wamesema katika kitabu na hata cha mwaka jana wamesema kwamba wanataka hii Bodi ya Usajili wa Wahandisi iweze kusimamia kazi zote zinazofanywa za kihandisi, wahandisi watokane na umoja huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi zinazojengwa zinakuwa chini ya viwango; naomba nitoe mfano, barabara ya Biharamulo ambayo imetoka Rusaunga inakwenda mpaka Kasindaga. Ukienda kwenye barabara hiyo pale kwenye keep left ya Biharamulo barabara imebomoka kabisa. Kilomita mbili kabla hujafika Kasindaga barabara imekwisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiitazama baada ya lami kubanduka pale utaona kwamba ile barabara imetengenezwa chini ya kiwango. Kwa hiyo, naomba Wahandisi ambao tunawasifu kwamba wanafanya kazi wafanye kazi kulingana na taaluma zao. Kama Wahandisi hawawezi kusimamia miradi hii, basi hii miradi itajengwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kusisitiza kuhusu usafiri wa Ziwa Victoria, watuletee meli yetu. Nisiseme, labda niseme wana ajenda gani na watu wa Kagera pale ambapo wanatunyima meli, tunakosa usafiri.