Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda niishukuru Serikali yangu pamoja na Wizara kwa ujumla kwa namna ya pekee ambavyo wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kwamba wanachanganua changamoto ambazo zinatupelekea kupata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri na Serikali katika kutupatia pesa ya maendeleo ya barabara; milioni karibu mia tisa katika Mkoa wa Katavi, lakini bado ni chache. Naomba wafikirie namna ya kuongeza kutokana na namna ambavyo barabara zimeharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika jimbo langu; napenda kuongelea Daraja la Kavuu. Daraja la Kavuu lilikwisha, lakini pamoja na kwamba ni la muda naomba sasa barabara ya Majimoto-Inyonga ambayo wamenitengea karibu milioni mia moja sabini, sidhani kama zitatosha kutengeneza zile kilomita mia mbili na kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sasa ili daraja lile liweze kupitika niombe Mheshimiwa Waziri wanisimamie na waniongezee pesa katika barabara hii ya Majimoto-Inyonga ili tuweze kutumia lile daraja na tuweze kuwarahisishia wananchi kutoka katika Jimbo la Kavuu kufika Inyonga na hatimaye kuweza kufika Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwashukuru wameweza kunipatia hela ya matengenezo ya barabara ya Mamba- Kasansa ambayo ni karibu milioni tisini. Pia niwashukuru kwa kunipatia pesa kwa ajili Kibaoni-Majimoto-Kasansa ambayo ni milioni takriban mia moja hamsini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri asinichoke ninapokwenda kuendelea kuomba kuhusu maendeleo ya Jimbo langu la Kavuu kwa sababu mvua ni nyingi na hivi ninavyoongea bado zinaendelea kunyesha na barabara na madaraja mengi na makalavati mengi yameharibika. Kwa hiyo, naomba washirikiane na TARURA kwa karibu na najua pesa yao ni ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na Wabunge wengine, kama vile tunavyosema tuwaongezee pesa angalau sasa ifike asilimia 50 kwa sababu wamekuwa wakifanya kazi nyingi bila uwezo wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee daraja langu ya Mwamapuli-Chamalendi ambalo TARURA wameweza kunipa pesa ya dharura na sasa hivi linapitika na wananchi wangu wanaweza kupita kwenda kwenye matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa yale maombi yangu ya dharura niliyoleta TANROAD ambayo nataka kujenga daraja la kudumu basi wayafikirie ili tuweze kurahisisha wananchi wa Kata kuanzia ya Majimoto, Mbede, Chamalendi, Mwamapuli, Ikuba, wote waweze kufika katika hospitali ama Kituo cha Afya cha Usevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kuongelea suala la Mradi wa Kokoto wa Kongoro. Mradi huu kwa kweli kama tutausimamia vizuri tunaweza tukaingiza pesa za kutosha. Inawezekana tatizo ni makubaliano kati ya TAZARA upande wa Zambia na upande wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri aunde tume basi ambayo itaweza kusimamia na kuangalia mkataba huo ili huu mradi uweze kujiendesha kibiashara na Watanzania wengi waweze kufaidika katika mradi huo ili tuweze kuona ni namna gani wanaweza wakachangia maendeleo katika nchi ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee Gati la Karema. Gati la Karema limeshafanyiwa upembuzi yakinifu, lakini katika bajeti iliyopita walituambia kwamba Karema hakutajengwa tena gati patajengwa bandari. Sasa tulikuwa tunaomba tupate ufafanuzi ni gati litakalojengwa ama ni bandari ili wananchi waweze kuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wameshafanya upembuzi yakinifu tunataka tujue maendeleo ya Bandari hiyo ya Karema ikoje, kwa sababu ndio kiungo kinachotusaidia sisi kutoka Kavuu kuja Mpanda Mjini mpaka Karema kuvuka mpaka Congo ambako tunaweza kupeleka mazao kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Mpanda. Kiwanja cha Ndege cha Mpanda ni kizuri na kimekwisha. Naomba ule upungufu uliobaki, Mheshimiwa Waziri mwaka jana nimemweleza na naomba tena na narudia, ili kiweze kufanya kazi tuweze kupata na sisi watalii wanaoweza kuja katika Mbuga ya Katavi ili tuweze kuongeza uchumi, kwa sababu Mbuga ile ya Katavi ina wanyama ambao ni unique. Tuna Twiga ambao ni machotara ambao hawapatikani kokote, ni warefu kuliko kama wengine, ni wanyama walioshiba. Tuki- promote na sisi mbuga yetu upande wa kule angalau tunaweza tukaongeza kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi pia katika suala la mawasiliano, kwa ndugu yangu Mzee Kamwele Ilunde, bado mawasiliano ni shida katika Kata ya Inyonga- Ilunde. Niwaombe basi tuweze kuwasaidia ndugu zetu wa Ilunde ili waweze kupata mawasiliano hatimaye waweze kuongeza vipato vyao kwa sababu wako karibu na Tabora na wako karibu na Kavuu, kwa hiyo inaweza kuturahisishia sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watakapokuwa na mawasiliano mazuri wanaweza wakafika mpaka Mbeya na wakarudi wakaingia mpaka Tunduma, Zambia kuweza kufanya shughuli zao ambazo zinaweza kuwaletea vipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee kuhusu TBA. TBA wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana; tatizo ni kwamba inawezekana hawana mtaji. Kwa hiyo naomba Serikali iangalie namna ya kuwatumia TBA katika miradi mbalimbali ya ujenzi inayoendelea nchini ili waweze na wao kuweza kwenda mbele katika kuongeza pato la Taifa. Kwa hiyo lengo ni kwamba wawaongezee hawa watu ili waweze kupata nanii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri naomba niulize, katika maziwa makuu yanayotajwa sijasikia Ziwa Rukwa. Sasa nataka kujua Ziwa Rukwa wana mpango gani nalo, maana yake wavuvi wako kule; lakini nasikia Ziwa Tanganyika, Victoria na Ziwa Nyasa, lakini sijasikia Ziwa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa, kama walikuwa hawajaliweka katika mpango wa Maziwa Makuu, naomba wafahamu kwamba lile ziwa nalo lipo na naomba liingizwe katika mpango wa maendeleo namna ambavyo wataweza kulishughulikia tuone namna gani ambavyo wavuvi wa upande wa kule nao wanafaidika kutokana na miradi ambayo wanakuwa wameiweka kwenye Maziwa Makuu ambayo Ziwa Rukwa hawajaliweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo naomba nikumbushe barabara yangu ya Kibaoni kupita mpaka Muze mpaka Kilyamatundu ambayo waliahidi kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, lakini ipo kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi tangu awamu iliyopita mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tupate majibu, je, barabara hii itajengwa lini na itaanza lini na itakwisha lini? Kwa sababu ni zaidi ya miaka 15 ipo kwenye maandishi ambayo haijaweza kufanyiwa lolote. Ni kutoka Kibaoni kupita Majimoto–Kasansa-Mfinga- Muze mpaka Kilyamatundu. Kwa hiyo tunaomba kabisa tutake kujua hatma ya barabara hiyo ikoje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo napenda tu niwapongeze Wizara kwa namna ambavyo wamekuwa wasikivu, hasa Mheshimiwa Waziri ni msikivu sana tunaposema shida zetu anatusikiliza na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu, Rais wetu ni msikivu, napenda tu niwatie moyo, naomba wasikate tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua changamoto za hali ya hewa ni nyingi sana, tuangalie, tushirikiane na Ma-engineer kama walivyosema na watu wa hali ya hewa tuone tunajenga barabara za aina gani ili tuweze kukabiliana na majanga yanayotokana na hali ya hewa hasa mafuriko yanayoendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante.