Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Ujenzi, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, watendaji wote katika Wizara hii kwa kazi kubwa waliyoifanya chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Tanzania kwa jitihada za makusudi za kubadilisha maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie mambo machache yafuatayo nikianza na viwanja vya ndege, barabara za Mkoa wa Dar es Salaam na usafiri wa ndege za ATCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuhakikisha vifaa vyote muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya usalama wa anga na usalama wa ndege wakati inatua kwenye viwanja, kwa kuweka alama, taa ambazo rubani wa ndege anaweza kuziona wakati kunapokuwa na ukungu mkubwa kwenye viwanja vya ndege ili kuepusha athari kubwa (usalama kwanza).

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na upungufu wa viwanja vya ndege ambavyo havikidhi viwango vitakavyowezesha ndege kubwa kuweza kutua katika viwanja hivyo kwa sababu mbalimbali kama kiwanja cha ndege cha Musoma, kiwanja cha ndege cha Mugumu – Serengeti (kwa ajili ya hifadhi), kiwanja cha ndege cha Iringa na kiwanja cha ndege cha Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuboresha viwanja hivi kutasaidia maeneo hayo kujiimarisha kiuchumi na kiusalama, kutokana na kiwanja cha Musoma na Mugumu ni eneo la kiutalii na ndiyo kuna Makumbusho ya Muasisi wa nchi yetu Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere. Hivyo, wageni wengi kutoka nchi jirani na watalii wengi kupitia Musoma kwenda Serengeti National Park.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanja cha Iringa ni muhimu sana kuboreshwa kutokana na uhitaji wa uharaka wa watumiaji pia ni kiwanja ambacho kiko karibu na kiwanja cha ndege cha Dodoma ambacho inapotokea dharura mfano ndege kupungukiwa na mafuta inaweza kutua kiwanja cha karibu cha Iringa na Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara za Mkoa wa Dar es Salaam; katika sekta ya barabara kumekuwa na changamoto nyingi katika barabara za mitaani, hali hii imesababisha adha na kero kubwa kwa wakazi wa Mkoa huo. Barabara ya Tabata kuelekea Segerea - Kinyerezi - Malamba Mawili - Msigani mpaka Mbezi kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaohamia, kwa sababu hiyo kumekuwa na changamoto ya foleni kubwa ya magari ambayo huchukua masaa mawili mpaka matatu hali hiyo husababisha watu kuamka mapema sana kuwahi foleni isiwakute muda wa saa 11.30 alfajiri ndiyo muda mzuri wa kuwahi kwenda mjini ili kuepuka adha hiyo. Tunaomba Serikali itafute utaratibu wa kuipanua barabara hiyo ili iweze kusaidia kutatua kero hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya Mheshimiwa Rais ya barabara ya Segerea Seminary kuelekea Majumba Sita kupitia Kituo cha Polisi cha Stakishari Mheshimiwa Rais wa Tanzania aliahidi kuijenga kwa kiwango cha lami na daraja wakati akiwa kwenye mkutano wa kampeni mwaka 2015 katika viwanja vya Vingunguti. Naiomba Serikali itimize ahadi hiyo maana hali ya barabara hiyo ni mbaya sana, wananchi wanalalamika kwa kukosa barabara ya uhakika.