Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Kivuli, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miezi mitano jela, tunampa pole kwa anayopitia. Kambi ya Upinzani ikiungana na Watanzania ambao wanalitakia mema Taifa hili, wanaungana naye na wanasema kwamba yampasa apitie hayo anayopitia ili aweze kupata ukombozi kwa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza sana maoni ya Kamati ya Wizara hii ambayo inasema kwamba inashangazwa, tangu kuundwa kwa Sheria hii ya Huduma za Vyombo vya Habari, ni kwa nini mpaka sasa hivi Mheshimiwa Waziri anaona kigugumizi kutunga kanuni? Ili sheria iweze kufanya kazi yake vizuri ni lazima iwe na kanuni ambazo zitaongoza sheria ile iweze kufanya kazi. Matokeo yake hivi sasa kinachoendelea, Mheshimiwa Waziri anachokifanya sasa hivi ni kufungia magazeti kazi ambayo siyo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anafungia magazeti kwa kusema ni kosa la uchochezi. Tunaelewa kosa la uchochezi ni kosa la jinai na Mahakama pekee ndiyo ya kutoa hukumu hiyo. Tuliomba kanuni hizi ziundwe ili kuwe na yale mabaraza likiwemo la ithibati ambalo ndilo litakuwa na room ya kuzungumza na Mwandishi na kutoa adhabu inayostahili kulingana na alichokifanya. Siyo kama hivi sasa Mheshimiwa Waziri akilala, anaamka asubuhi ni kufungia gazeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha na wakati mwingine kunakuwa na double standard. Yale magazeti ambayo yanaandika habari mbaya za kupiga Upinzani, za kutukana viongozi wa Upinzani likiwemo Gazeti la Tanzanite, Mheshimiwa Waziri sijui halioni? Ikifika kwenye magazeti kama hayo, anavaa miwani ya mbao, lakini ikifika Tanzania Daima anavaa miwani yake ya kawaida na anayafungia magazeti. Tunasikitika sana kama kunakuwa na double standard katika matukio haya na tunataka atupe majibu ni kwa nini kanuni hazitengenezwi mpaka sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakumbukwa tuliambiwa hapa Bunge Live halitakiwi kwa sababu kutakuwa na msongamano wa waandishi na nini, hawataweza kufanya kazi yao vizuri, tukaambiwa mwarobaini itakuja Bunge TV na itakuwa na uwezo wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata habari, tukakubaliana na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, toka hiyo Bunge TV ianze mpaka sasa outreach yake ni wapi? Kwa sababu hata pale barabarani haifiki. Yaani hii Bunge TV inakuwa kama kioo cha ndani, tunakaa hapa ndani tunajitazama tukitoka nje hatuwezi kujiona. Hivi kwa nini hii Bunge TV isiunganishwe ikaingia mpaka kwenye ving’amuzi Watanzania wakaona kinachoendelea ndani ya Bunge lako? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni issue ya bajeti, tulitegemea hata Mheshimiwa Waziri angeizungumzia sasa hii Bunge TV iweze kupewa, ifanye kazi yake vizuri, iweze kufikisha habari kwa Watanzania. Kwa sababu walitupa mifano, wakatuambia angalia hata South Africa kuna channel ya Bunge. Ni sawa hatujakataa, lakini tunataka tuione kwenye frequency, watu wenye ving’amuzi waione. Hata ikiwezekana wale wenye TV za local wawe na uwezo wa ku-access, wakati mwingine wa-relay kwenye Bunge TV wawaoneshe Watanzania kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu waandishi kukosa access, pamoja na hii Bunge TV kuwepo. Tunaelewa kwamba lipo Kikanuni, Mbunge anapozungumza hapa yapaswa kila kitu kiingie kwenye Hansard, lakini Mbunge akiongea jambo ambalo lina ukakasi kwa Serikali linakuwa- edited.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwulize Mheshimiwa Waziri, ni vigezo vipi vinavyotumika? Kwa sababu ukienda kwenye written Hansard utakuta kila kitu kinaandikwa vizuri kabisa, lakini kile ambacho kinachukuliwa hapa kinarekodiwa, wanapewa waandishi huko, hawana access na baadhi ya information zinakatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi upo Mheshimiwa Waziri akitaka nitamwonesha.

TAARIFA . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mwandishi professional, siwezi kumjibu, naendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kuhusu suala la usajili wa magazeti. Wote tunaelewa usajili ni kitu ambacho ni permanent. Usajili wa magazeti hivi sasa kuna sheria eti kila mwaka magazeti lazima yasajiliwe, tumewahi kuona wapi? Katiba yetu Ibara ya 18 inasema, ni haki na ni uhuru kwamba kila mwananchi ana uwezo wa ku-access information. Sasa wanapokuja na vigezo kwamba kila gazeti, kila mwaka lisajiliwe upya tunaomba watuambie, hivi Serikali wakati inapitisha bajeti zake, TRA ilionesha kwamba moja ya vyanzo vyake ni usajili wa magazeti? Ina maana hapa kuna ukiukwaji wa Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua usajili ni permanent na hii tunajua ni makusudi tu. Yale magazeti ambayo hayataandika mapambio ya kuitukuza na kuisifu Serikali hii ya CCM baada ya mwaka yatafungiwa, hayatapewa usajili. Hali hii inasababisha wamiliki wa vyombo vya habari kuwa na uwoga. Watu ambao wanataka hata kuingia kwenye biashara hii ya vyombo vya habari, wanashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kuhoji, hii wamei- copy wapi? Nimejaribu kufuatilia nchi za Afrika Mashariki, nimeona ni Rwanda pekee yenye element ya namna hiyo, kwamba kila mwaka wanasajili magazeti. Ni kwa nini tunachukua utaratibu ambao siyo utamaduni wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata blogs nazo eti zinaambiwa zinatakiwa zisajiliwe na zilipe, tena kwa hela nyingi; kati ya laki moja mpaka laki mbili. Mtu kafungua blog yake ambayo anategemea Watanzania watapata taarifa, lakini shilingi 200,000/= anaipata wapi? Haya ni masharti ambayo wanawawekea watu, wananchi watakwenda kuumia kwa sababu hawatakuwa na access ya kupata information.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TCRA tulitegemea wangesaidia kusimamia sheria iliyopo ya kuhakikisha habari zinawafikia Watanzania, lakini TCRA imekuwa kama ni barrier sasa. Yaani kitu kidogo TCRA tayari ni kupiga faini magazeti, ni kupiga faini TV, ni kupiga faini redio, hali ambayo wakiangalia, na wao wana takwimu, waangalie tangu Serikali hii ya Awamu ya Tano, ni watu wangapi wameingia kwenye ku-invest kwenye media?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna kasi kubwa sana ya watu ku-invest kwenye media katika kipindi cha Awamu ya Nne, lakini siyo sasa hivi. Ni kwa nini? Masharti magumu, lakini tunajua behind ni kuangalia vile vyombo ambavyo haviimbi mapambio, ndiyo vipewe fursa ya kuhakikisha kwamba vinaendelea kufanya kazi, vile vinavyokosoa Serikali kuhakikisha kwamba havipati fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo tunajiuliza, nimemsikiliza sana Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake. Katika hotuba yake tulitegemea angetuambia ni nini kinachoendelea katika matukio haya ya Waandishi wa Habari kupotea, kutekwa, kunyanyaswa na waandishi wa habari wamekuwa kama vifaranga vya kuku ambavyo havina mchungaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, hata mwezi haujapita, Mwandishi wa Gazeti la The Guardian alitekwa, alipigwa, alinyanyaswa, lakini hata Mheshimiwa Waziri hana habari. Hawa ndiyo watu wake ambao anafanya nao kazi. Kwa nini hawasemei Waandishi? Serikali kwa nini haitoi matamko kuhusu matukio ambayo Waandishi wa Habari wanafanyiwa, ikiwemo Azory ambaye sasa hivi amepotea ni miezi mingi mpaka sasa hatujasikia hata tamko la Serikali. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri akizungumza habari za sanaa, za nini, lakini kuzungumza habari za Azory ambaye amepotea sijawahi kumsikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahoji haya matukio ambayo Waandishi wa Habari wamekuwa wakiyaripoti, Serikali inaendelea kukaa kimya. Tunashuhudia watu wanapigwa risasi mchana kweupe, media zinaripoti, lakini hakuna kinachoendelea. Tunashuhudia watu wanatolewa bastola, Waandishi wa Habari wamepiga picha zinaonekana kabisa, mpaka sasa hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maiti zinaokotwa tunaoneshwa kwenye media, kwenye kila namna ya magazeti, lakini hakuna chochote kinachoendelea. Sasa ifike mahali Mheshimiwa Waziri, Wizara yake itambue mchango mkubwa wa kazi ya Wanahabari ambao wana kazi ya kulielimisha Taifa hili, kazi ya kutoa taarifa za Taifa hili ili Serikali iweze kufanyia kazi na kutoa matamko ya mambo yanayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuhusu suala…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)