Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. KHADIJA H. ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali, Wizara ya Habari pamoja na Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake wote katika Wizara hii kwa jitihada zao wanazofanya kuhakikisha wanafikia malengo waliyojipangia katika kuendeleza sekta zote zilizomo ndani ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri yafuatayo:-

(i) Wizara iongezewe fedha ili iweze kutekeleza majukumu yake.

(ii) TBC inahitajika nchini kote hivyo Serikali iendelee na juhudi za kuwajengea uwezo wafanyakazi ili waendane na hali ya sasa ya teknolojia ya habari. Aidha, TBC ipatiwe mitambo ya kisasa na yenye nguvu ili iweze kusikika na kuonekana ndani na nje ya nchi kwa muda wote.

(iii) Wizara iweke msukumo na mkakati maalum katika kuiendeleza lugha ya Kiswahili ikiwemo shughuli zote za kiserikali itumike lugha ya Kiswahili, mikutano yote inayofanyika nchini itumie lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuongeza ajira kwa Watanzania, kuongeza idadi ya watumiaji wa Kiswahili na kuifanya lugha yetu hii itumike duniani kote.

(iv) Wizara kupitia taasisi zake zote iendelee na juhudi zake wanazochukua kuhakikisha maadili, mila na desturi za Watanzania zile zilizo bora zinalindwa na wasisite kuzuia au kufungia nyimbo, michezo, filamu na sanaa zote zinazokiuka maadili ya nchi yetu na Watanzania kwa ujumla.

(v) Wizara ihamasishe na kufufua michezo ya zamani ambayo imepotea ambayo inaweza kuongeza tija kwa Taifa na wananchi kwa kuongeza kipato na kulinda isipotee kabisa.

(vi) Sanaa na utamaduni ni vyombo vyenye nguvu sana katika kuitangaza nchi. Hivyo juhudi za Wizara za kuitangaza nchi yetu kupitia sanaa mbalimbali ziongezwe kwa lengo la kuitangaza zaidi nchi yetu ya Tanzania duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kupiga kazi kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.