Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia leo kusimama hapa na kwa kweli kutoa mchango wangu wa mawazo kwenye Wizara hii. Kwanza kabla sijaanza, niseme ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Shinyanga Mjini kwenye Jimbo letu la pale Shinyanga Mjini, Mheshimiwa Waziri naomba achukue hili suala na shida hii kubwa ambayo tunayo; tuna tatizo kubwa sana la uchakavu mkubwa wa Kituo chetu cha Polisi pale Shinyanga Mjini. Vilevile tuna tatizo kubwa sana la uhaba wa magari; kuna Wilaya mbili za Kipolisi, Ushetu pamoja na Msalala, hazina magari ya Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nianze. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza sana Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa sana ambayo amekuwa akiifanya. Nalipongeza sana Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya. Naomba niseme yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa IGP na Makamanda wake, watulie wala wasiwe na wasiwasi. Waendelee kuchapa kazi. Kazi wanazozifanya zinaonekana, mambo mema wanayoyafanya yanaonekana. Hatuwezi ku- compromise kwenye suala zima la usalama. Hii nchi watu walikuwa wamezoea kudeka, kufanya mambo ya ajabu na kuropoka maneno ya ajabu kila siku na kutukana hovyo kwenye mikutano. Lazima ifike wakati tushikishwe adabu. (Makofi)

Vyama vyote vya Siasa, ukiwa CCM, ukiwa chama chochote lazima ufike wakati ujue kwamba nchi lazima ifike wakati itawalike. Isiwe kwamba watu wanakuwa huru kiasi ambacho mtu anakaa ana uwezo wa kuamka leo asubuhi akafanya anachotaka, ana uwezo wa kukaa mchana akafanya anachotaka, lazima ajue kwamba nikifanya jambo lolote nikiwa na azma mbaya, nitashughulikiwa. Hiyo ndio Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu mpaka wamefikia kusema kwamba Jeshi la Polisi ni wapiga debe wa CCM; watu wanasahau. Ndiyo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge aliyetoka kuzungumza hapa kwamba yanapokuwa masuala mema, pale tunapokaa tunalindiwa mali zetu na usalama wetu, tunaona hivi vyombo vya ulinzi na usalama kwamba ni vizuri sana. Pale inapokuja sasa kwamba na sisi tunashughulikiwa kwa mambo yetu ambayo tumeyafanya mabaya, tunaanza kuona Jeshi la Polisi ni baya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi sio wote ni wabaya, sio wote wanafanya kazi zao kinyume na sheria na utaratibu, wapo watu wengine baadhi ambao tunaona na hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tusione kwamba Polisi wote hawafai, Polisi wote sijui wameoza. Kwanza hali ya usalama iliyopo sasa hivi, uhalifu ulivyopungua, sasa hivi inaonesha kabisa kwamba Jeshi letu la Polisi na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza RPC wa Dodoma, licha ya haya maneno ambayo watu wanasema sijui amesema hivi, lakini mimi nampongeza. Nampongeza RPC wangu wa Mkoa wangu wa Shinyanga, nampongeza pia sana RPC wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana. Kwa ujumla ni mfumo mzima ndani ya Jeshi la Polisi wanafanya kazi nzuri, lakini yote haya, lazima na sisi tukiwa kama Watanzania bila kujali itikadi zetu za kisiasa, tofauti zetu za kiitikadi, lazima tujiulize, kwa nini nchi yetu imekuwa na chokochoko namna hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini mambo mengi sana sasa hivi yamekuwa yakisemwa na kumekuwa na chokochoko namna hii? Tena mpaka imefikia kiwango watu wa nje sasa wanaanza kuingilia uhuru wetu na mwenendo wetu wa nchi. Lazima tujiulize, yote haya yanasababishwa na kazi nzuri ambayo anaifanya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ambayo anaifanya, kwa namna yoyote ile hakuna mtu ambaye anaweza akakaa akafurahia. Wawekezaji kwenye Sekta ya Madini huko watu wamebanwa, wameshikwa pabaya; wakiangalia sijui watumishi hewa, wameshikwa pabaya; mafisadi, watu walikuwa wamekaa wamejiachia, wanakula pesa, wanafanya mambo ya ajabu, wameshikwa pabaya. Kwa hiyo, lazima tujue kwamba vita hii tuliokuwa nayo ni vita kubwa kuliko ambavyo tunaweza kufikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tu asubuhi Mheshimiwa Lema hapa amezungumza, aliuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu suala zima la matatizo ya mafuta ghafi ambayo yamezuiliwa huko bandarini. Hilo suala lina makorokoro mengi sana huko ndani. Namshukuru Mheshimiwa Lema hata kwa kuuliza lile swali. Sasa watu kama hawa ambao wamekuwa wakishughulikiwa lazima wao wenyewe kwa wenyewe watakuwa wanapiga makelele. Mwaka jana Mheshimiwa Rais alisema, wewe ukiwa kama mwanaume, unafanya biashara halali, ikifika mwezi wa Sita wewe utakuwa ni mwanaume kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuwa anasema namna ile kwa sababu hawa watu ambao wameguswa pabaya na wengi wetu na hata hawa wengine wa upande wa pili wanawajua na wengine wengi wao ambao wanawajua, wanajua kwamba baadhi yao wafadhili wao. Lazima ifike wakati na wao wawe wazalendo kutoka mioyoni mwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiona kwamba jambo hili ni baya, tuangalie hatima zetu za huko mbele, tusiangalie tu leo; tuangalie wajukuu na watoto wetu na ndugu zetu hao wengine wa baadaye. Tusikae tu kuangalia kwamba eti tumekaa, mara mambo yamekuwa yanaibuka ovyo, mara sijui hivi na hivi na hivi; lazima tujue kabisa kwamba hawa wafadhili wetu itafika mwisho sisi tutaondoka, lakini maisha ya Watanzania yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wakiendelea kusema, mimi nimezoea. Waseme wee, wakichoka wananyamaza, mimi naendelea. Watulie misumari iingie. (Makofi)

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge kwa muda mrefu wamekuwa wakizungumzia kuhusu suala zima…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa mwenyekiti, licha ya changamoto nyingi ambazo Jeshi la Polisi limekuwa linazo, lakini kazi kubwa ambayo imekuwa ikifanyika imekuwa inaonesha kabisa kwamba nchi hii, kinachotakiwa kimsingi ni dhamira ambayo iko kwa viongozi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nataka nizungumzie, nataka nizungumzie Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Nailaumu Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Nampongeza sana Kamishna wa Uhamiaji, mwanamke, Kamishna Anna Makakala, anafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamishna wa Uhamiaji anafanya kazi kubwa na nzuri sana. Kamishna huyu amekuwa anashughulikia masuala ya uhamiaji haramu, lakini yako mambo na matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza. Kuna taarifa kwamba wapo wahamiaji ambao wamekuwa wakiingizwa hapa Tanzania na watu ambao hawana uzalendo na nchi yetu; wahamiaji hawa haramu wamekuwa wakifa kwenye magari; wahamiaji hawa haramu wamekuwa wakitupwa na wale watu ambao wanaingiza kinyume na sheria; wanawatupa kwenye mito, bahari na kadhalika, lakini Wizara hii ipo kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwigulu, matokeo yake sasa imekuwa ni kwamba Serikali na sisi ambao tupo Chama cha Mapinduzi tumekuwa tunalaumiwa kwamba watu hawa sijui wanakufa, sijui wanauawa na kadhalika. Kwa nini Serikali hamsemi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnapokaa mnanyamaza kimya inafanya kwamba kile ambacho kinaendelea kufanyika sasa hivi, watu wanatumia sana mitandao hii ya kijamii, taarifa ambazo zinapelekwa kule siyo zote ni za kweli.

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya CAG, naomba Mheshimiwa Waitara akaichukue, atulie kichwa chake kiwe sober, aisome yote ataelewa ninachokisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia kuhusu Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Naomba kuanzia sasa hivi Wizara hii iamke. Iwe inatoa taarifa bila kumwonea mtu aibu. Matukio ambayo yanatokea, changamoto ambazo zinaendelea; ninafahamu kwamba endapo kama mtu ameuawa aidha kisiasa au hata kama siyo kisiasa, kwa sababu yapo mambo mengi ambayo yanafanyika, jinsi mwendelezo wa huo uchunguzi unavyoendelea, wawe wanatoa taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nafahamu kwamba hawawezi kusema kila kitu, lakini wawe wanasema kwamba angalau tumemkamata mtu na mambo haya yanaendelea. Kwa sababu yapo mambo ambayo yanasemwa kisiasa wakati kiuhalisia hata kwenye vyama vyetu vya siasa kuna mambo mabaya tunafanyiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi, kuwa mwanachama wa CUF, kuwa mwanachama wa CHADEMA, kuwa mwanachama wa chama chochote haina maana ya kwamba huwezi kuwa na matatizo yako mengine ya kijamii. Haina maana kwamba wewe kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa au wewe kuwa kiongozi wa Chama cha Siasa, basi ni mtakatifu kwamba ikitokea kuna chochote ambacho kimetokea dhidi yako maana yake ni kwamba umefanywa au jambo hilo limefanywa na mpinzani wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara hii waamke. Wamekuwa wananyamazia sana haya matukio. Matokeo yake Serikali imekuwa ikisemwa na ikihusishwa kwa mambo mengine ambayo hata hayapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili Mheshimiwa Waziri kwa kweli endapo kama ataendelea kunyamaza namna hii wakati anajua kabisa kwamba haya mambo yapo mengine ambayo yanafanyika kinyume na utaratibu; naomba watu watajane na watu watajwe kwamba huyu amehusika na huyu amehusika kwa moja, mbili, tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.