Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuzungumza mbele ya Bunge lako tukufu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kunipatia afya na nguvu na kuweza kusimama leo hii mbele ya Bunge lako na kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuzungumzia suala zima la bajeti ya elimu. Bajeti ya elimu imeweza kufanyiwa kazi kwa mwaka 2017/2018 na kuweza kupatikana kwa asilimia 65 ndani ya matumizi ya kawaida na asilimia 68 katika miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini elimu ni kila kitu, bila kuwa na elimu huwezi kupata maendeleo yoyote katika maisha ya mwananchi, ni lazima apate elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ninaiomba Hazina ijipange kwa ukamilifu angalau kwa Wizara ya Elimu iweze kupata bajeti yake kwa asilimia 85 ili waweze kutekeleza mambo yao kwani wana changamoto nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Mkoa wetu wa Rukwa tuna mapungufu ya madarasa, tuna mapungufu ya matundu ya vyoo, tuna mapungufu ya nyumba za walimu na vilevile tuna mapungufu ya maabara pamoja na vifaa vya maabara. Ukiachia mbali suala zima la upandishaji wa vyeo vya walimu na hata kuhakikisha kwamba wanapata stahiki zao zilizo sahihi katika Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wanakosa hata ule motisha na kufanya kazi yao katika uweledi na kufanya kazi yao katika hali iliyo nzuri zaidi. Kwa hiyo, ninaiomba Hazina kuweza kutoa fedha za kutosha kutokana kufuatana na jinsi bajeti tutakavyoipitisha hapa leo ili kuhakikisha kwamba elimu waweze kutimiza malengo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nilikuwa naomba Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba inajikita sana katika elimu ya awali. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tuseme kwa kweli kabisa kwamba lugha yetu ya Tanzania ni kiswahili, lakini lugha ya kiingereza ni muhimu kwa watoto wetu. Kwa hiyo tunawaomba Wizara ya Elimu tujikite kuhakikisha kwamba haya masomo ya awali (chekechea) waanze na lugha ya kiswahili na lugha ya kiingereza mpaka kuendelea huko mbele. Kufikia hapo ndiyo kusema ya kwamba walimu wanafundisha shule za chekechea naomba wafanyiwe maandalizi mazuri ili waweze kwenda kuwaandaa watoto wetu katika elimu ya awali ambao ndiyo msingi wa kuibua elimu bora ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala zima lililozungumzwa katika ukurasa 143, kuhusu nyumba za walimu. Suala la nyumba za walimu ni tatizo la nchi nzima. Ninamshukuru Mheshimiwa Waziri na Wizara yake kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hakika Mama Ndalichako na timu yako mnafanyakazi pamoja na changamoto zilizopo hamyumbi na wala hamtikisiki ilhali kwamba mnafanyakazi kwa pamoja. Ninawaomba hizi nyumba 40 zimetajwa katika shule kadhaa na Rukwa tumetajiwa shule moja ya Kasanga. Lakini nilikuwa naomba, kwa kuwa bajeti hii tumechelewa kuwekewa zaidi ya shule mbili/tatu kwa Mkoa wa Rukwa ninaomba awamu ijayo Mkoa wa Rukwa uweze kuangaliwa katika kuhakikisha kwamba tunajenga nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesema mnajenga nyumba za walimu katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi, hata sisi kwetu Mkoa wa Rukwa ziko sehemu hizo; Milepa, Kaoze, Kipeta, Ninde, Wanpembe, Kala, Senga, Molo ni maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi. Ningeomba kwamba tuweze kupatiwa nasi vilevile ujenzi wa nyumba za walimu ili walimu wawepo wa kutosha ili watoto wetu waweze kupata elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, napenda kuzungumzia suala la usafi wa mazingira. Usafi wa mazingira shule zetu za msingi na sekondari katika upande wa vyoo kwa kweli hauridhishi, unasikisitisha sana na kwa kuwa Wizara imeamua kujenga madarasa 2,000 na matundu ya vyoo 2,000, hata wakijenga 10,000 lakini hayatakuwa bora zaidi ikiwa kwamba hatuna huduma za maji katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Hazina (Wizara ya Fedha) wahakikishe kwamba zile shilingi bilioni
17.033 ambazo wizara imeweka kama bajeti yao 2018/2019 fedha hii itoke kwa sababu imeshawekwa hapa, lakini ingeongezeka ikawa ni kubwa zaidi kwa sababu zoezi walilonalo kuhusu vyoo vya shule kwa kweli eneo ni kubwa zaidi na vyoo kwa sababu vinahitaji maji na maji hayapo shuleni wanahitaji kuweka miundombinu ya maji, aidha, ya kukinga maji ya mvua au kuhakikisha kwamba wanaweka mifereji na kufikisha maji katika shule zetu zote za nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni zoezi kubwa, kwa hizi shilingi bilioni 17 kwa kweli ni ndogo zingeweza zikaongezeka ili wakaweza kufanisha hili zoezi ambalo ni gumu na tete kwa watoto wetu; na hasa watoto wetu wa kike hawawezi kuzihifadhi kwa sababu zile siku zao tatu au siku zao tano wanakosa maji katika maeneo yao ya shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napenda vilevile kuzungumzia suala la ujenzi wa shule za mikoa. Imetajwa mikoa saba inayojengewa shule, ninawaomba kwamba hata Mkoa wa Rukwa nao unahitaji kuwa na shule. Tuna shule chache na hata shule za sekondari za wasichana hatuna. Tunayo sekondari ya wasichana moja ambayo ni ya dhehebu ya wenzetu wa kikristo iko pale Kizwite, lakini tunahitaji kupata shule za sekondari za wasichana hata mbili, tatu kwa Mkoa wetu wa Rukwa na mjue wazi kabisa kwamba Mkoa wa Rukwa ulikuwa uko pembezoni na imechelewa na mambo mengi. Kwa hiyo suala la elimu ni mojawapo.

Kwa hiyo, tunawaomba kipindi kijacho, naomba katika ujenzi wa sekondari hizo za mikoa na Mkoa wa Rukwa uwemo katika mipangilio hiyo ya kikao kinachokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya ukurasa wa 126 wa hotuba wamezungumzia suala la ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi. Ninashukuru kuona Mkoa wa Rukwa nao umo miongoni mwa hiyo mikoa, tunashukuru sana Wizara. Lakini je, hii shule ya ustadi inakwisha lini? Ni ndani ya mwaka huu wa 2018/2019 ama zaidi ya mwaka mmoja? Kwa hiyo, tunapenda kufahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naifahamu wazi kwamba ndugu zangu wa Wizara ya Elimu tulishazungumza mara nyingi sana ndani ya Bunge hili kwamba Mkoa wa Rukwa hatuna Chuo cha VETA. Tunaomba Chuo cha VETA nayo inaanza lini kujengwa pale katika Mkoa wetu wa Rukwa ili vijana wetu wa darasa la saba na darasa la kumi na mbili waweze kupata mahali pa kuweza kupata stadi na kuweza kujiajiri wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nililokuwa napenda kulizungumzia ni kuhusiana suala ya walimu. Walimu wanahitajika kupata motisha. Lakini pamoja na hivyo Wizara imeelekeza katika ukurasa wa 123 kwamba kuna fedha zimetengwa, takribani trilioni moja ambazo watazitumia kwa kuhusu na kutoa na motisha kwa Halmashauri na kwa shule mbalimbali ili waweze kuonesha nguvu ya kuongeza elimu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, lakini tatizo linakuja ubora wa hizi Halmashauri na kupata motisha hizo na ubora wa hizi shule kupata motisha hizo kwa walimu wale kutaendelea na kuwezekana kuwepo kuwa na bora zaidi ikiwa Idara ya Ukaguzi ikiwezeshwa. Hawana magari, hawana mafungu ya kujiendesha wao wenyewe katika suala zima la ukaguzi. Ukaguzi si maafisa wanaokaa ofisini, ukaguzi ni watu ambao wanakwenda field si kwa ratiba maalum hata wakati mwingine kuvamia zile shule na kuona zinaendelea namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba hiyo motisha iliyokuwa imetengwa ninaomba Hazina itoke ili kwamba wale watakaoshinda na wale watakaoshindwa waweze kuhamasika ili na wao pia kipindi kichokuja waweze kufanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusiana na ubora wa elimu. Ubora wa elimu ni mambo mawili; wale wanaoandaliwa na wale wanaowaandaa hao wanaoandaliwa. Kwa hiyo tunaomba elimu waweze kuangalia kitu hicho wale wanaowaandalia hawa wanaoandaliwa wawe katika ubora zaidi na katika ukamilifu zaidi. Na hawa watu wapo tunao walimu walimaliza kusoma vyuoni wako mitaani hawajapata bado ajira, tunaomba hao walimu wato…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima nashukuru kwa kunipa nafasi hivyo, naunga mkono hoja.