Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia hii hoja iliyo mbele yetu ambayo ni hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze zaidi kwenye udhibiti wa ubora wa elimu. Nikianzia ukurasa wa 63 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri amebainisha kwamba Wizara imeandaa michoro kwa ajili ya kujenga ofisi 50 za Wadhibiti wa Ubora wa elimu. Naomba tu niishauri Serikali kwamba iharakishe ujenzi wa Ofisi hizi za Wadhibiti Ubora wa Elimu na ikiwezekana basi kwa kuwa Dodoma ni makao makuu na kwenye kitabu chake hiki hakubainisha kwamba ni Wilaya zipi ambazo zitajengewa, basi angetupa kipaumbele sisi Mkoa wa Dodoma kujengewa ofisi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili elimu iwe bora zaidi naamini kabisa masuala ya utendaji wa kazi kwa ajili ya hawa wenzetu wa udhibiti ubora wa elimu yanatakiwa yawe mazuri sana. Katika maeneo mengi ya nchi hii, Wadhibiti wa Ubora wa Elimu hawana kabisa ofisi za kutosha na kama zipo, zipo chache, lakini nyingi ya ofisi hizi ziko katika majengo ambayo ni au yamekodishwa au vipi, kwa hiyo, inawaletea kadhia sana wenzetu hawa. Nikichukulia kwa mfano katika Mkoa wa Dodoma kuna zile Wilaya mpya ambazo zimeanzishwa, katika Wilaya hizi zote hakuna ofisi za Wadhibiti wa Ubora wa Elimu. Kwa hiyo, naomba tu nisisitize juu ya umuhimu wa suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, hawa wenzetu wa Wadhibiti wa Ubora wa Elimu pia nyumba hawana. Sambamba na nyumba lakini pia suala la vitendea kazi, wanahitaji vitendea kazi ili kusudi waweze kutoa taarifa muhimu wanapokuwa wanakwenda kukagua hizi shule. Kwa hiyo, niitie shime Serikali kwamba lazima vitendea kazi vipatikane ili hawa Wadhibiti wa Ubora wa Elimu waweze kuleta mrejesho wanapokuwa wamekwenda kukagua katika hizi shule basi zile shule ambazo zinakaguliwa ziweze kujua wapi zinatakiwa zijirekebishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwenye suala la usafiri katika hizi Ofisi za Udhibiti wa Ubora wa Elimu. Naipongeza Serikali wametoa magari katika baadhi ya hizi Ofisi za Udhibiti wa Ubora wa Elimu lakini tatizo liko kwenye madereva. Bado madereva hawajaajiriwa kwa wingi, utakuta kwamba kuna baadhi ya ofisi inabidi waazime madereva kutoka idara nyingine. Inapotokea kwamba madereva hawa wakaazimwa na yule anajua kabisa kwamba ameazimwa, haoni ni muhimu kuitunza gari ile.

Kwa hiyo, kama imeshindikana basi kuwaajiri hawa madereva, Wizara ione utaratibu itawezaje kufanya itoe kibali maalum ili kusudi kuweza kuwapatia wale Maafisa Udhibiti wa Ubora wa Elimu waweze kuyaendesha wao wenyewe yale magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie kuhusu suala la OC. OC kwenye Ofisi za Udhibiti wa Ubora wa Elimu kwa kweli imekuwa ni tatizo na hivi ninavyozungumza hata OC ya kuanzia mwezi Januari mpaka hii leo bado hazijapatikana. Tumekuwa tukisema kwamba tunataka elimu iboreshwe, itaboreshwaje ikiwa hawa ndugu zetu ambao wanafanya udhibiti wa ubora wa elimu inakuwa ni mtihani kwao kupata OC? Kwa kweli naomba Wizara ilione hili jambo ili kusudi hawa Wadhibiti wa Elimu waweze kufanya kazi kwa kusimamia suala zima la elimu kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 76 wa hotuba hii imezungumzia kuhusu kuendeleza ujuzi kwa kuboresha vyuo vya ufundi. Naipongeza sana Serikali kwa sababu tutakapopata mafundi mbalimbali kama walivyozungumza wenzangu waliotangulia itasaidia nchi yetu inavyokwenda kwenye uchumi wa viwanda wa kati. Kwa hiyo, suala la ufundi stadi ni la muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri kwamba katika baadhi ya shule za msingi kuna vituo vya ufundi stadi, hebu Serikali ione jinsi ya kuviboresha vile vituo vya ufundi stadi ambavyo viko katika zile shule za msingi kwa sababu baadhi ya wazazi hawawezi kuwapeleka watoto wao VETA na utakuta vyuo vingi vya VETA viko mijini. Kwa hiyo, Serikali ione itashirikiana vipi na VETA kuweza kuhakikisha kwamba vile vituo ambavyo viko katika shule za msingi vinapatiwa walimu wenye ujuzi pamoja na vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niyapongeze sana taasisi na mashirika mbalimbali ya elimu katika kutekeleza majukumu yake. Niipongeze Serikali kwa kui-task TET iweze kuandaa masuala mbalimbali yanayohusiana na elimu kwa sababu tuliona kabisa kwamba siku za nyuma kumekuwa kukitokea malalamiko kwamba vitabu vya kiada, mihtasari na vinginevyo vimekuwa haviandaliwi kwa maudhui yaliyo sahihi. Kwa hiyo, naomba niipongeze sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi kubwa sana za Serikali katika kuboresha elimu bado tumeona kwamba suala la miundombinu ni changamoto hasa katika shule za Serikali. Mfano, makataba, maabara, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pamoja na samani havitoshelezi. Kwa kuwa Serikali inajitahidi sana kukabiliana na upungufu huu na bado Watanzania wengi wanajitahidi kuzaa kwa kupata watoto wengi, naomba nitoe ushauri kwa Serikali ione umuhimu wa kuhamasisha Halmashauri zote za Miji, Manispaa, Majiji na Wilaya waanzishe mifuko ya kuendeleza elimu katika maeneo yao. Kwa kuanzisha mifuko hii ina maana kwamba itasaidia sasa ku-supplement zile shughuli za Serikali ambazo inawezekana upungufu ni mkubwa ikasaidia kujenga baadhi ya miundombinu na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie kuhusu shule binafsi. Wenzangu wengi wamelizungumzia, lakini shule binafsi zinafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali siyo competitor, lakini kuna kodi nyingi sana kwa hizi shule za binafsi. Hebu Serikali ione kwamba hawa ni wadau ambao wanakwenda pamoja badala ya kuwawekea hizi kodi nyingi wazipunguze ili kusudi hizi shule za binafsi ziweze kutoa elimu inayotakiwa na tunajua kwamba zinatoa elimu ili wasije wakakwama, wakaona kwamba Serikali inatafuta mbinu ya kuwakwamisha ili wasifikie malengo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie kuhusu wahitimu wa Chuo cha Ukutubi Bagamoyo. Serikali imekuwa ikiingia gharama sana kwa kuwafundisha hawa wakutubi lakini wengi wao hawana kazi na tunasema kwamba vyuo vianzishe maktaba sasa kwa nini hawa wahitimu wasipate fursa hiyo kwa kuajiriwa ili kusudi sasa hizi maktaba ziendeshwe kitaalam? Kwa hiyo, naomba niishauri Serikali ione hilo hitaji kubwa kwamba hawa Wakutubi wanahitajika katika shule ili kusudi waweze kufanya kazi yao kwa jinsi inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba nitoe ushauri kwamba kwenye Ofisi za Udhibiti wa Ubora wa Elimu nako kuwe kuna maktaba maalum na nashauri katika maktaba hizo vitabu vyote vya marejeo, vitabu vya kiada na vitabu vya ziada viwepo ili kusudi viweze kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la vifaa vya kujifunzia na kufundishia bado ni changamoto kwenye mtaala mpya kuanzia darasa la tatu na kuendelea kwa ufundishaji ambao ulikuwa uanze tangu mwaka 2015. Wenzangu wengi wamelizungumzia, lakini kuna baadhi ya walimu wanatumia vitabu vya zamani. Mfano, hisabati darasa la nne havijafika mashuleni na walimu wanatumia vile vitabu vya zamani. Hebu Serikali itafute ufumbuzi wa kuhakikisha kwamba vitabu hivi vya mtaala mpya vinafika shuleni kwa wakati unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, suala la mgawanyo wa fedha bado hauzingatii mahitaji maalum ya shule ambazo zina matokeo mabaya. Tumeona kabisa kwamba kuna baadhi ya shule zina matokeo mabaya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.