Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
NCCR-Mageuzi
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubongo wa mtoto ni very delicate, ili nieleweke vizuri nitatumia mfano wa yai la kuku.
Yai la kuku ukiliwekea joto stahiki utapata kifaranga, kitakuwa kuku na baadae litataga, lakini ukiwekea joto ambalo ni la juu sana yai hilo litaiva na likiiva linaliwa na itakuwa mwisho wake, lakini ukiwekea joto lingine yai hilo hilo unaweza ukariharibu au kulidumaza. Huu ni mfumo unaokufa au unaodumaa utakuwa na deterioration or stagnation katika system. Naomba tusiue au kudumaza akili za watoto wetu, lulu zetu, zawadi ya mama Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na hilo kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba, tumeamua kupitia Wizara yetu ya Elimu kukumbatia ujinga ambao ndiyo umesababisha umaskini, maradhi, rushwa na mambo mengine katika jamii ya Tanzania. Imeandikwa kwamba watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa yaani mfumo endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema watu wanaagamia, ukichukua vitabu kwa mfano, nilikuwa nasoma hivi vitabu vilivyofanyiwa maboresho sasa. Ukisoma kitabu cha darasa la pili unaambiwa unganisha sauti za herufi, tangu lini ukaunganisha sauti za herufi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, consonant a, e, i, o, u hata kuiandika ni tatizo. Hivi vilivyofanyiwa maboresho vinavyosambazwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuimba kwenye Bunge hili, ukiangalia kitabu cha darasa la tatu cha Kiingereza vinavyosambazwa sasa kina makosa lukuki. Unawezaje ukaanza na alphabet unit ya tatu wakati unit ya kwanza unaanza na sentensi, nimetaja machache tu. Vitabu vyetu hivi havina majina ya Wahariri, vina maudhui mabovu na vinakiuka hata sheria na maadili vinaonesha ukatili, tangu lini polisi akawa ni mzungu na wanatesa watu, kwa nini vitabu hivi vilivyofanyiwa maboresho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule binafsi. Shule binafsi ni wadau muhimu sana katika elimu ya Taifa letu la Tanzania. Wengi wetu ni zao la shule binafsi hata Marais wastaafu Mzee Nyerere, Kikwete, Mkapa na Rais wa sasa Magufuli ni zao la shule binafsi na hasa mashirika ya dini. Mimi mwenyewe ni-declare ni zao la hizi shule binafsi. Leo hii kama siyo shule binafsi tuorodheshwe Wabunge humu ndani ya Bunge wangekuwa kwenye hali ya namna gani? Shule binafsi nyingi hata zilizotaifishwa kwa mfano shule ya Pugu, Ihungo, Umbwe, Peramiho, Masasi, Minaki, Weruweru, Kilakala nitaje chache tu na vyuo vya ualimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kilimanjaro una shule 314, mwaka jana kidato cha nne wamekuwa wa kwanza Kitaifa niwapongeze sana, niipongeze shule ya Anuarite ambayo ipo Jimboni Vunjo ambayo imekuwa ni shule ya tano kati ya shule kumi bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya vyuo vikuu inakuwa na ubaguzi wa hali ya juu sana. Ninapende kuuliza na Serikali inijibu vizuri student unit cost mfano mwanafunzi anayesoma Shahada ya Kwanza ya Udaktari pale KCMC Serikali inachangia kiasi gani na mzazi/mwanafunzi anachangia kiasi gani. TCU inalazimisha chuo kile waweze kuchangia shilingi 3,100,000; je, vyuo vingine vya tiba wanachangia kiasi gani ili kuwe na standard ambayo inaeleweka badala ya kupiga huku na kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matatizo mengi, Mzee Nyerere amesema nina kitabu chake hapa na nimesoma, ukisoma hotuba ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1967 anasema elimu yoyote iwe ya darasani au isiyo ya darasani ina shabaha yake, shabaha yenyewe ni kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine maarifa na mila za Taifa kwa kuandaa vijana wake tayari kuchukua nafasi zao katika kulitumikia na kuliendeleza Taifa. Mzee Mkapa amesema elimu yetu tunahitaji mjadala wa Kitaifa na Mzee Kikwete naye ametamka, nani atamke zaidi mpaka tuhakikishe kwamba tunaangamiza elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme the way forward, tukubali elimu yetu tupo kwenye janga ni maafa na ukiwa na maafa naomba tusiwe na tofauti za kiitikadi humu ndani, tusimame sote kwa pamoja na Mheshimiwa Waziri yote tunayoyasema uyachukulie very positive kwa ajili ya kujenga Taifa, Wizara, watoto wetu na kizazi chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu tuwe na mjadala mpana wa Kitaifa, hata urejee hoja yangu niliyoitoa humu Bungeni ya tarehe 31 mwaka 2013. Mjadala huu tukiwa nao tuwe na matokeo ya muda mfupi, kwa mfano matokeo ya muda mfupi.
Kuhusu shule binafsi kwa nini Wizara ya Fedha ianze kwenda kwenye majengo, mabwalo, mabweni, kumbi, waanze kutoza kodi ya majengo, kodi za ardhi na viwanja vya michezo. Hilo wala halihitaji mjadala ni suala la muda mfupi jadilini Serikalini ondoa zote wala usijadili, ada za mitihani ondoa wala msijadili masuala kama haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde suala la kusimamia ubora wa elimu Tanzania, tuwe na chombo kimoja cha kusimamia standard ya elimu Tanzania na hili lisichukue muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunaihitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania, tupende tusipende. Tuone kwa wenzetu karne hii ya sayansi na teknolojia, sayansi ni maarifa na teknolojia ni namna gani ya kutumia ya kutumia yale maarifa, duniani wenzetu wanafanya nini ili tuweze tukaondoka hapa Tanzania badala ya kila siku kulia. Lengo la nne la maendeleo endelevu ya dunia linasema elimu shirikishi, sawa, bora kwa wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni miundombinu ya binadamu, ukombozi wa mtoto wa kike ni elimu, lakini nimefanya utafiti miaka ya 1978 ndiyo tatizo la lishe lilianza Tanzania kwa kasi kubwa na zaidi ya asilimia 42 ya Watanzania walikuwa na tatizo la lishe kwenye shule zetu. Kwa hiyo, kunakuwa na intellectual disability ya hali ya juu sana. Unaweza kuona labda hata wengi walio madaktari, wahandisi na hata miongoni mwetu miaka ya 1978 hiyo hatujapata lishe vizuri labda ndiyo maana tunashindwa kufanya maamuzi yaliyo sahihi katika mazingira ya ajabu tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba chonde chonde walemavu wetu, kuna shule ya walemavu pale Moshi ya Kanisa Katoliki ipo Kimashuku ambapo Kanisa Katoliki wanajenga shule nzuri tu pale lakini wamewekewa vikwazo kwa kuwekewa vigezo vingi na ni shule kwa ajili ya walemavu, sasa tunafanya mambo gani ya namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisema kwa uangalifu kabisa, unajua Mzee Mwinyi alinifundisha namna ya kuhifadhi. Kwa mfano, nilivyosoma darasa la kwanza, Sister Benedicta na Sister Protasia walikuwa wananifundisha wananiambia ukitaka kumjua Yesu ni kujua elimu na tulikuwa tunaimba hivi tunasema: “Wa rohoni ndiye mwalimu kwake ni hunifumbulia, kukujua nipe elimu, Yesu mwema nijalie, eeh Yesu wataka nikupende.” Yaani mwanafunzi unahifadhi kwa sababu ya ubongo wa mtoto na unajua umuhimu wa elimu katika Taifa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtume Muhamad anasema nini ukitaka akhera usome, ukitaka dunia usome, elimu ni kitu chake kilichompotea muislam popote akipatapo na akichukue. Baba Askofu Mstaafu Dkt. Shoo anatuambia hivi: “Matendo yetu mema tunayoyafanya hapa duniani ni sauti huru na hai miili yetu ikiwa kaburini.” Leo hii tunamsikiliza sana Baba wa Taifa yupo kaburini lakini kazi nzuri aliyoifanya ya elimu kwa Taifa letu. Sasa nani tena aseme ili tuweze tukaelewa (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara chonde chonde, hapa tulipofika sasa kwa nini tusifundishe watoto wetu; “a, e, i, o, u hizi ni herufi kuu, tamka kwa sauti kuu, ndiyo a, e, i, o, u; na jicho eee, kama mpira ooo, ni kikombe uuu” tunakuwa very focused ili watoto wetu na bongo zao zilivyo delicate waweze kuelewa badala ya kuwarundikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, michezo na sanaa kwa sababu ya muda nitashindwa kurudia. Michezo na sanaa mtoto wa darasa la kwanza michezo na sanaa unamsaidia nini kwenye KKK! Anatakiwa kusoma, kuhesabu na kuandika. Sasa unamrundikia masomo yote na vitabu vyote hivi, huyu mtoto atafanyaje? Tumesema mara nyingi, angalia sera hii ya elimu ya mwaka 2014 iliyozinduliwa na Rais Kikwete ile siku ya Ijumaa tarehe 16 Februari, 2015 yapo mambo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachopenda kuomba baada ya kuizindua hii Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 haviendani vitu hivi. Sasa haya mambo ya kushindana huku shule binafsi huku hivi hapana. Hebu tuje pamoja kama Taifa na rai yangu kwa Bunge hili kwenye suala la elimu tuondoe itikadi... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)