Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwa kifupi sana juu ya Wizara hii ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi na maendeleo ya nchi yetu. Taifa lenye watu wasioelimika daima halitakaa liendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiendelea kushuhudia anguko la elimu licha ya Serikali kujitahidi kutoa elimu bure. Tumeendelea kushuhudia quantity na siyo quality kwenye elimu yetu. Kuzidi kuongeza usajili wa wanafunzi bila kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ni sawa na kazi bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeshuhudia upungufu wa walimu na kushuhudia uwiano wa wanafunzi kwa mwalimu ukiwa 1:50 na shule za awali 1:1159. Hata ije miujiza gani hapa hamna ufaulu. Vilevile uhaba ni mkubwa sana kwenye upungufu wa walimu na masomo ya sayansi hasa biology, physics, chemistry na mathematics na ukizingatia tunasema Tanzania ya viwanda bila kuwa na msingi imara ya sayansi tangu shule ya msingi na maabara ni kazi bure. Cha kusikitisha zaidi walimu tulionao wengi wamekata tamaa kwa sababu mbalimbali kama kutokuwepo kwa motisha, kutopandishwa madaraja, mishahara duni, mazingira duni ya kazi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nyingi za Serikali hazina miundombinu imara ya kufundishia mfano madarasa, vyoo, maabara, nyumba za walimu, ofisi za walimu na kadhalika. Hizi ndiyo sababu kubwa ukilinganisha na shule za binafsi ambapo wao uwiano kati ya mwanafunzi na mwalimu ni ya kuridhisha, idadi ya wanafunzi darasani ni chini ya 40, maabara za kisasa, maktaba na idadi ya walimu ni wa kutosha. Ni wakati muafaka sasa tuwe na mjadala mpana kama Taifa juu ya hatma ya elimu yetu na nini kifanyike na hili lifanyike mapema sana. Bila hivi tutaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu huku tukifurahia idadi kubwa ya kusajili wanafunzi na ufaulu duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa ufupi naomba kukarabatiwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tarime (TFDC) ili kiweze kutoa elimu yenye tija ikizingatiwa kinahudumia Tarime, Rorya na Serengeti na ikiwezekana kijengwe VETA. Katika bajeti ya mwaka huu imeainisha vyuo 20 vitakarabatiwa na ama kuongezewa majengo.

Naomba sana Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tarime nacho kiingie kwenye ukarabati wa majengo na karakana zake ambazo zimechoka na majengo mengine hayajakamilika. Hili nimekuwa nikiliulizia sana, hivyo, naomba sana katika hivyo vyuo 20 na cha Tarime kiwemo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu ukarabati wa shule kongwe ya Tarime ambayo ina michepuo zaidi ya saba na inachukua wanafunzi toka nchi nzima na ni shule ya A-Level tu kwani miundombinu yake imechakaa sana ni ya tangu mwaka 1973, hii siyo sawa kabisa. Vilevile tupewe gari la wagonjwa na ile Land Cruiser iliyochukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuboreshwa kwa Chuo cha Ualimu Tarime. Naomba pamoja na uboreshaji huo ikiwezekana kibadilishwe na kuwa chuo kikuu hasa ikizingatiwa ukanda ule hatuna chuo kikuu ili kuboresha elimu na kuweza kuchukua wanafunzi wengi wanaokosa udahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusu uhitaji wa shule ya wasichana Jimboni kwangu ukizingatia jamii ya Wakurya awali tulikuwa nyuma katika kusomesha watoto wa kike. Kwa kuzingatia pia Mkoa wa Mara tupo tano bora kwa idadi ya mimba za utotoni na kuacha shule kwa watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo langu (Halmashauri ya Mji wa Tarime) hatuna high school ya wasichana au hata mchanganyiko, bali tunayo high school moja tu ya Tarime ambayo ni wanaume tu siyo mchanganyiko, hivyo inatoa fursa kwa wavulana tu ambao wanatoka shule za kata mchanganyiko na hivyo kuacha wasichana. Kwa kuzingatia haya, naomba sana Serikali itupe fedha za kujenga high school ya wasichana maana tayari tuna uwanja pale Tagota, Kata ya Kenyamanyoni. Pia tunatarajia kupata fedha za Mogabiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba sana Halmashauri ya Mji, tunahitaji fedha kwa ajili ya high school ya wasichana tu ili tuwe na uwiano wa high school ya Tarime ambayo nayo ni chakavu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba majibu na utekelezaji.