Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri ya kuandaa hotuba hii na kuiwasilisha vizuri Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuelekea kwenye uchumi wa viwanda kwa hakika tunahitaji wanasayansi wengi zaidi Tanzania, tuna tatizo kubwa sana la upungufu wa walimu wa sayansi katika shule zote. Wanafunzi wanaochukua mchepuo wa sayansi wamekuwa wanakatishwa tamaa, pia wengi wamekuwa wanafanya vibaya kwenye mitihani ya mwisho. Tumejenga maabara hakuna walimu wa kufundisha practicals na theories pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kaliua karibu shule zote za sekondari za kata zina mwalimu mmoja tu na nyingine hakuna kabisa. Naomba Serikali isaidie upatikanaji wa mabweni ya wanafunzi katika shule ya Kiliua High School ambayo ndiyo shule pekee ya high school kwa Kaliua. Inawachukua wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali, lakini hakuna mabweni ya kutosha. Baadhi ya wanafunzi wanatumia madarasa kama mabweni kwa sababu ya shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo kubwa sana la kukosekana kwa nyumba za walimu hasa kwa shule za vijijini. Walimu wengi wanapangwa kufanya kazi, wanapokuta hakuna nyumba na mazingira magumu ya kufundishia wanaondoka kwenye vituo walipopangwa na wengine wanaacha kazi. Tunaomba Serikali ilete mpango maalum kuhakikisha miundombinu mashuleni inaboreshwa hasa nyumba za walimu, vyoo na maktaba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya vyuo vikuu vya umma ina hali mbaya, udahili wa wanafunzi unaongezeka kila mwaka lakini miundombinu yake haiboreshwi ikiwepo library, madarasa, maabara na kadhalika. Matokeo yake wanachuo wanasimama madarasani huku wakifundishwa pengine wanafanya shift ku-share lectures room.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke kipaumbele kwa Chuo Kikuu cha SUA, Morogoro, chuo pekee Tanzania kinachotoa elimu ya juu kwa masuala ya kilimo na mifugo. Asilimia 75 ya Watanzania wote ni wakulima, wafugaji, tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda, kilimo lazima kipewe kipaumbele. Waziri Profesa Ndalichako naomba utupe mkakati maalum kwa chuo hiki ili wanafunzi wanaotoka pale walete impact kubwa kwa wakulima na wafugaji Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ubora wa elimu wa vyuo wa elimu ya juu; TCU ina jukumu la kuhakikisha vyuo vikuu hapa nchini vinakidhi vigezo vya udahili wa wanafunzi kutoa ithibati, kuhakikisha ubora wa elimu na kuidhinisha programu zinazofundishwa vyuoni. Katika kutekeleza majukumu TCU imekuwa inachelewa ufuatiliaji wa vyuo vya private na matokeo yake wanashtuka baadae ambapo wanafunzi/wanavyuo wameshadahiliwa, wameanza masomo na hata wamefanya mitihani ya mwisho. TCU inachukua hatua too late wakati wanafunzi wameshalipa ada wanafunzi wamefanya mitihani ya mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata taarifa ya TCU kugundua madhaifu makubwa katika Chuo cha Mount Meru wanafunzi kupewa vyeti wakati walifeli, walimu zaidi ya asilimia 75 kuacha kazi kwa kutolipwa mishahara kwa miezi zaidi ya sita. TCU imeagiza wanafunzi wale warudi chuoni ndani ya miezi mitatu wafanye mitihani upya, hapa wazazi watalipa fedha nyingine. Hili ni tatizo kubwa, tunaomba maelezo ya kutosha wakati chuo hiki kinaendesha mitihani mpaka kutoa vyeti walikuwa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kila Wilaya kuna chuo cha VETA; vyuo vya VETA vipatiwe vitendea kazi vyote muhimu na walimu wenye ujuzi wa kutosha kusaidia kufundisha watoto wetu wapate stadi na ujuzi wa kuendesha maisha yao na kuendeleza Taifa. Fedha inayotolewa na waajiri kwa ajili ya kukuza vipaji na kutoa mafunzo ya vitendo, Skill Development Levy (SDL) itolewe iende VETA ifanye kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za Serikali kuongeza fedha za malipo ya vyuo vikuu na kufikia idadi ya wanafunzi 122,623 bado wanafunzi wanaopata mikopo ni michache na wanaohitaji ni wengi zaidi. Serikali iongeze zaidi fedha ya mikopo kwa wanafunzi ili kila mtoto wa Kitanzania aweze kupata elimu ya juu.