Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza sana Mawaziri wote, Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Naibu Waziri Mheshimiwa Ole Nasha, kwa usimamizi mzuri wa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ndiyo msingi muhimu sana wa maendeleo ya mwanadamu na uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. Pamoja na changamoto nyingi tunazopitia kama nchi, nimpongeze sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Hii inasaidia Watanzania wanyonge nchini kupata fursa ya kupata haki yao ya msingi yaani elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya nchi yetu sasa ni kujenga uchumi wa viwanda. Ili kufikia uchumi huo wa viwanda ni lazima sekta ya elimu iwaandae vijana wetu mashuleni kupata elimu ya ufundi yaani stadi au ujuzi mbalimbali. Ili kufikia azimio hilo nashauri Serikali yetu ianzishe utaratibu wa kuwa na somo la ufundi kuanzia shule ya msingi. Kila shule ya msingi na sekondari angalau kuwe na darasa, angalau kipindi kimoja ambapo watoto wetu walioko shule za msingi watajifunza stadi mbalimbali kama vile uashi, useremela, ushonaji, uhunzi au uungaji vyuma, umeme na kadhalika. Hii itasaidia watoto kupenda masomo ya ufundi na baadae kupata fursa ya ajira kwenye viwanda vidogo vidogo na vikubwa hata kujiajiri wenyewe. Katika kufanikisha jambo hili, tunaweza tukachagua shule moja ya msingi katika Kata na tukaanzisha darasa hilo la ufundi.
Mheshmiwa Mwenyekiti, lugha ya kufundishia na kujifunzia. Tumekuwa na mjadala kwa miaka mingi nchini juu ya lugha ipi itumike kwa kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wetu. Historia ya nchi nyingi ambazo uchumi wake umekua kwa haraka sana katika miongo hii ya karibuni ni kutokana na kuongezeka kwa ubora wa elimu. Ubora wa elimu unatokana na kutumia lugha inayoeleweka kwa wanafunzi na walimu wanaowawezesha wanafunzi kujifunza. Mfano, nchi za China, Korea, Malaysia na kadhalika. Watanzania tunapozaliwa tunaanza kujifunza lugha za kienyeji (mother tongue) tukiingia darasa la kwanza tunakutana na lugha ya kiswahili na tunatumia kujifunza kwa miaka saba. Baada ya miaka saba, Mtanzania akienda sekondari anakutana na lugha mpya ya kiingereza. Matokeo ya mchanganyiko huo, wanafunzi wetu wanakuwa wakishindwa kumudu masomo ya sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kwenye mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na nne, watoto wamekuwa wakiandika kwa lugha ya kiswahili katika kujibu maswali. Mtahiniwa anaweza akawa anajua kabisa hoja anayotakiwa kuieleza au kujibu, lakini kwa kuwa ameelewa kwa kiswahili wamekuwa wakishindwa kuandika kwa lugha ya kiingereza na badala yake anaandika kiswahili na kukosa alama kwa kuwa anatumia lugha isiyo rasmi kwenye somo husika. Hivyo nashauri ni muhimu Serikali iamue tufundishe masomo yote kwa kutumia lugha ya kiswahili ambayo ndiyo lugha mama na inaeleweka kwa Watanzania wote. Lakini kama tunadhani kiingereza ndiyo lugha bora zaidi, basi tufundishe kiingereza toka chekechea mpaka chuo kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udhibiti ubora wa elimu nchini; kitengo hiki ni muhimu sana katika kuangalia au kusimamia ufundishaji na ujifunzanji wa wanafunzi. Idara ya ukaguzi pamoja na umuhimu wake, lakini inakabiliwa na matatizo makubwa mawili, uhaba wa magari na kukosa fedha za kununulia mafuta ili waweze kuzifikia shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule zinakaa miaka mitatu mpaka minne bila kukaguliwa. Hii ni hatari kubwa sana kwa maendeleo ya elimu katika nchi yetu. Wizara ya Elimu ione umuhimu wa kuwawezesha wadhibiti ubora kufika mara kwa mara kwenye shule zetu ili kufanya ukaguzi na kujua kama walimu wanafuata miongozo vizuri, pia mikakati na njia za kufundishia zinatumika vizuri. Hii itasadia walimu kufundisha vizuri na kuwafanya walimu wawe mahiri katika masomo yao. Hili litaongeza ufaulu wa wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, naipongeza Serikali kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo hiyo. Pamoja na ongezeko hilo bado Wizara hasa Bodi ya Mikopo iwe makini katika kufanya tathmini ya wanafunzi wenye sifa ya kupata mikopo. Kuna baadhi ya watoto wanaotoka kwenye familia maskini wanakosa mikopo. Kigezo cha kwamba kipaumbele ni wale waliosoma shule za Serikali ndiyo hawana uwezo siyo sahihi sana, kuna watoto wamekuwa wakisomeshwa na Waheshimiwa Wabunge, Makanisa na watu wengine wasamaria wema baada ya kuona wazazi wao hawana uwezo au yatima, lakini wanapohitimu masomo yao na kuingia Chuo Kikuu hukosa mkopo kwa kuwa wamesoma shule zisizo za Serikali. Hivyo naomba sana Serikali itathmini kwa makini juu ya vigezo vya kupata mikopo kwa wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana na naunga mkono hoja.