Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Elimu, Sayansi na Technolojia. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri ya kuanza kuboresha elimu hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uboreshaji wa elimu kumekuwa na changamoto kubwa ya walimu kukosa ujuzi na mbinu za kufundishia, sambamba na walimu kutovutiwa na mazingira ya ufundishaji, jambo ambalo linawafanya kutofundisha kwa bidii na hivyo kusababisha kushuka kwa ubora wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hizi zimepelekea kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao ya kuhitimu. Uchambuzi wa matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha pili na cha nne mwaka 2017 unaonesha wastani wa asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mitihani hiyo walipata daraja la nne na sifuri. Nashauri Serikali ijikite katika kushughulika na changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa walimu, kwa mujibu wa takwimu za BEST za mwaka 2016 na 2017 idadi ya walimu kwa shule za msingi imeshuka kutoka walimu 191,772 mwaka 2016 hadi kufikia 179,291 mwaka 2017, ikiwa ni anguko la asilimia 6.5 na kufanya uwiano wa walimu na wanafunzi kuwa 1:50. Aidha, katika shule za awali, idadi iliyopungua ni walimu 1,948 na kufanya uwiano wa walimu na walimu na wanafunzi kuongezeka kutoka 1:135 mwaka 2016 hadi kufikia 1:159 mwaka 2017 badala ya 1:25 ambao ni uwiano unaokubalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule za sekondari kuna uhaba mkubwa wa walimu kwa baadhi ya masomo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hisabati kuna upungufu wa walimu 7,291, bailojia kuna upungufu wa walimu 5,181, kemia kuna upungufu wa walimu 5,373 na fizikia kuna upungufu wa walimu 6,873; hii ni kwa mujibu wa takwimu za BEST za mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu za Elimu ya Msingi za Mikoa (BEST Reginal Data 2017) walimu 7,743 wanatarajiwa kustaafu kati ya mwaka 2018 na 2019. Aidha, takribani walimu zaidi ya 30,000 wana umri wa zaidi ya miaka 51 ya kuzaliwa, hivyo na wao wanatarajiwa kustaafu muda mfupi ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa hakuna elimu bila walimu Serikali inatoa majibu gani katika maswali yafuatayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kitu gani kimesababisha upungufu wa walimu ukizingatia kwamba kuna idadi kubwa ya wahitimu wa fani ya ualimu katika vyuo vya ualimu vilivyopo nchini? Je, Serikali imeajiri walimu wangapi mpaka sasa ili kukabiliana na upungufu huo? Serikali ina mpango gani endelevu wa kuhakikisha kwamba tatizo la upungufu wa walimu linatoweka kabisa? Serikali imepanga kuajiri walimu wangapi katika mwaka wa fedha 2018/2019 kama sehemu ya mchakato wa kupunguza tatizo la upungufu wa walimu?