Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri kwa kazi nzuri pamoja na kuwasilisha bajeti yao ili tujadili. Yapo mambo ambayo nilikuwa nataka kupatia ufafanuzi na pia kutoa ushauri kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa usambazaji wa vifaa vya elimu kwa shule maalum za watoto wenye ulemavu. Nampongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Ndalichako kwa utaratibu wake wa kuvikagua kama vipo na kama vinatumika. Ni suala zuri sana kwa sababu kuna baadhi ya shule huwa zinapokea vifaa hivyo na kuviacha bila kutumika na wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kuwepo na utaratibu maalum wa kuwa na Mkaguzi Maalum wa vifaa hivi ili aweze kukagua na kuvifanyia ukarabati. Pia kuna baadhi hawana wataalam wa kufundisha, kwa wale wasiojua kuvitumia hasa walimu wao. Pia walimu katika shule hizi wote wangepatiwa elimu ya mawasiliano kwa watu wasiosikia. Shule hizi pia ziwekewe uzio kama Lugalo iliyopo Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ukarabati wa shule kongwe. Naipongeza Serikali kwa zoezi la ukarabati wa shule kongwe nchini, kwani shule hizi zilikuwa na miundombinu chakavu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu Bima ya Afya katika Vyuo Vikuu. Nilibahatika kukutana na Serikali za Vyuo Vikuu vilivyopo katika Mkoa wa Iringa. Changamoto yao kubwa ni kuhusiana na Bima ya Afya wanafunzi wanayochangia pesa ya matibabu lakini hawapewi kadi za matibabu kwa sababu vyuo vinakuwa havijapeleka pesa katika mfuko. Ushauri wangu kwa hili, ni vyema Bima ya Afya waweke dawati katika vyuo ili malipo yalipwe moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu chakavu katika vyuo, ni vyema pia Serikali ingekuwa na programu pia ya kuvifanyia ukarabati wa majengo shule hasa mabweni wanayoishi wanavyuo, mfano Chuo cha Mkwawa, mabweni yao hayajakarabatiwa kwa muda mrefu. Pia kuna upungufu wa madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuendelea kukopesha vijana wetu mikopo ya elimu ya juu. Naomba kigezo cha kupatiwa wanafunzi waliosoma katika shule za private, lingekuwa liondolewe kwa sababu kuna wanafunzi ambao ni yatima, wanasomeshwa katika shule hizo kwa ufadhili maalum au kuna wazazi waliokuwa wakati huo ni waajiriwa, lakini baadae wakastaafu uwezo wa kulipia vifaa, wao wanakosa. Pengine Serikali ingeangalia uwezekano wa mikopo hiyo kukopeshwa na taasisi za fedha ili hata kudai au kukusanya mkopo huo unakuwa rahisi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.