Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja hii ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Pia naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu kwa kuisimamia vizuri kuwa kiwango cha elimu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii ikiangalie Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Ulembwe. Chuo hiki kiko katika hali mbaya sana. Kwa kuwa miundombinu ni chakavu sana, naomba majengo yale yaboreshwe na kuezekwa kulingana na hali ya sasa. Wilaya ya Wanging’ombe haina Chuo cha VETA. Nimeomba majengo ya mhandisi mshauri yaliyopo pale Wanging’ombe yakubaliwe kutumike kwa kutoa elimu ya mafunzo ya ufundi VETA. Wizara ya ujenzi imeonesha nia ya kulikubali ombi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena Mheshimiwa Waziri kwa kunikubalia kukarabati shule mbili, moja ni shule ya msingi ya Dulamu na nyingine shule ya sekondari ya Usuka. Shule hizi miundombinu yake imekuwa modal kwa Wilaya yangu. Naomba mpango huo uendelezwe katika mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mpango mzuri wa kuendeleza elimu ya ualimu nchini. Tatizo lililopo hivi sasa ni upungufu mkubwa sana wa walimu na hasa shule ya msingi vijijini. Ziko shule zina walimu wawili tu kwa wanafunzi wa madarasa saba, hili ni janga. Ni vyema Wizara ijue namna ya kutatua janga hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeomba mfululizo kwa miaka mitano sasa kuanza kwa kidato cha tano na sita kwa shule za sekondari za Makoga na ile ya Wanike. Naomba majengo yaboreshwe na kukarabatiwa. Naomba sana zikubaliwe kupokea wanafunzi kwa mwaka huu 2018/2019.