Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mmoja wa wachangiaji katika Wizara yetu hii nyeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisimama mara nyingi sana kuchangia Wizara hii Wizara ya Maji. Pale Gairo pana mradi wa maji sasa hivi una muda mrefu, lakini kila nikisimama au kila Wizara ikileta bajeti ule mradi uko asilimia tu 84 na mwaka unaofuata unashuka unakuwa asilimia 75. Kwa hiyo, sasa sielewi mwaka mwingine unapanda bado haujaisha mwaka mwingine unashuka. Kwa leo sitaongelea sana huu mradi ila nitatoa ushauri kwa sababu nimeona kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 3 kwamba sasa hivi anatafutwa mzabuni wa kuweza ku-supply pump pamoja na mashine ya kuchuja chumvi ambayo ina uwezo wa kuchuja zaidi ya lita nafikiri kulingana na matenki zaidi ya mita milioni moja au zaidi kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa mpango huo nimeona kwenye gazeti la juzi hapa la terehe tatu, naomba iwe kweli kwa sababu huu mradi kwanza utakuwa ni mradi wa mfano kwa sehemu zingine za nchi yetu, kukuta maji mengi chini ya ardhi ni suala lingine na
kukuta maji salama ni suala lingine, unaweza ukachimba maji lakini ukakuta yana chumvi na ukienda kupima hayafai kwa matumizi ya binadamu. Kwa hiyo, siyo kila sehemu yenye maji mengi kwamba ni baraka unaweza ukakuta maji lakini yana chumvi ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule wa Gairo itakuwa ni mwanga kwa Wziara na sehemu zingine zote ambazo zina maji chini lakini hayafai kwa matumizi ya binadamu, nafiki ni mradi wa kwanza Tanzania ambao maji yatachunjwa sasa na kuwa maji salama na wananchi kutumia, naomba utekelezaji. Kwa sababu ule mradi ni wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na Wabunge wengine waliotangulia, siwezi nikasema Wizara ya Fedha haijaleta pesa haijaleta nini, tayari ule mradi wa shilingi 6,666,000,000 mkandarasi amechukua zaidi ya asilimia 80 ya pesa ameshachukua tayari, lakini haujakamilia sasa mimi siwezi kulaumu, siwezi kusema hapa pesa iko wapi haiwezekani! Hata huyo Waziri wa Fedha kama amezuia pesa bora azuie tu, kama asilimia 80 imechukuliwa na bado utekelezaji wake hata hauna dalili sasa hizo pesa zinakwenda wapi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wangu hapa amejitahidi sana pale Gairo na nushukuru tumemuomba aje pale Gairo na anakuja na nafikiri atakuja kwa ajili ya miradi ile ya maji kuja kuangalia. Atakuja Mvomero, atakwenda Gairo anaangalia miradi kwa sababu pesa tayari Kilosa, Mvomero, Turiani, Gairo, lakini kasi iko wapi ndugu zangu? Ingekuwa pesa haijatoka mngesema kweli hapa pesa haijatoka kuna matatizo, labda Wizara fulani haijaleta pesa hizo pesa zipo, maji yako wapi, tumekaa sasa hivi pale unajua kuna watu wengine duniani hawapo, mbinguni hawapo hawaelewi wanajua labda Mbunge huwa anapewa hela anaweka mfukoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu kabisa wanasimama pale wanakuambia Mbunge huyu wa Gairo amekula pesa zetu za maji, wanajua labda Wabunge tunapewa pesa kwa hiyo sisi ndiyo tunatoa toa pesa kwenye miradi. Wabunge hatupewi pesa, pesa ziko kwenu na ninyi ndiyo mnahudumia hizo au kama mmeshindwa mtu ukweli basi fedha zetu tuwe na account zetu za Mfuko wa Jimbo halafu tuweke watu muangalie nchi nzima kama haina maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa maji wa mradi huu maji hakuna, lakini ukiangalia hapa kwenye bajeti utaona usimamizi tu wa maji Gairo, Mvomero, Turiani na Kilosa ni shilingi milioni 490, usimamizi tu! Sasa si ulaji huu?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu namuomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Katibu Mkuu wamekuja pale, huu mradi wa Gairo utakuwa na gharama kubwa sana kwa wananchi. Nawakumbusha kwamba mradi huu wakati wa Waziri Maghembe alishasema ukiwa na gharama kubwa Serikali/Wizara italipia yenyewe gharama zile za pale siyo wananchi maana tuwekane sawa kabisa, muangalie kwenye Hansard. Ukiwa na gharama Wizara kama alivyosema Waziri aliyetangulia kwamba ninyi ndiyo mtakaowalipia gharama hizo wananchi wa Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewapa plan nyingi, tumewapeleka kwenye vyanzo vya Mserereko lakini kila watalaam wenu wakifika unasikia ooh! maji haya hayatoshi. Hivi maji haya ndiyo Mto Mkondoa yanasumbua watu kila siku yanaleta mafuriko pale Kilosa halafu unasema hayatoshi kusambaza Gairo? Tumewapeleka kwenye chanzo cha Mto Mkondoa unapotoka Gairo kila siku mafuriko pale Kilosa, Mto Ludewa, Mto Mvumi yote inatoka Gairo pale juu, kwa hiyo hata macho na sisi hatuoni kwa macho? siyo watalaam wa maji lakini hata kwa macho hatuoni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tumeomba pesa mtupe kile chanzo tunachotumia sasa hivi cha mserereko kina bomba za nchi tatu, tupeni bomba za plastic tu ambazo hazifiki hata shilingi bilioni moja tutoe pale kwenye chanzo cha Mserereko tulete pale. Mwaka jana mmetoa milioni 312 hazijatumika popote. Mnaweka tu hapa, litatumika bomba la chuma yaani mnapiga plan za ulaji ulaji, pesa ipo lakini plan za ulaji tu! Mwaka huu tena ukiangalia kuna shilingi milioni 300 eti hizi kufunga mita Mijini, kwanini msikusanye ile shilingi milioni 300 ya mwaka jana haijatumika na hii shilingi milioni 300 ongezeni hapo.

Waheshimiwa Wabunge, hatufuatilii tu mkiangalia, lakini kwenye Wilaya pesa za maji zinakuja nyingi, miradi ya utapeli mingi. Mimi mtu akiniambia hela haziji labda Wabunge wenyewe tu hatufuatilii tu, lakini ukifuatilia kwa makini, mimi pale Gairo naangalia pale na kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Saddiq na sehemu nyingine nyingi tu hata Mheshimiwa Mabula nimeongea nao hapa, kuna miradi mingi! Hata ya kwenye Halmashauri mnatoa hela, lakini Wizara hamsimamii siyo tuende mpaka TAMISEMI ile si mambo ya maji? Wizara ninyi mmetoa labda Gairo maji, kwa mfano pale Chakwale na Kibedi kuna mradi wa karibia shilingi milioni 500 lakini maji mpaka leo hayatoki na wakandarasi wameshakabidhi. Ukifungua yale maji mabomba yote yanapasuka, kwa hiyo mnataka sisi kama anavyokuja Mheshimiwa Magufuli hata haya mambo ya maji tukamlalamikie Rais? Sasa hawa wataalam wamewekwa kwa ajili ya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani, halafu mnajua kabisa Mji kama Gairo ni mji mkavu kama Dodoma, kwenye kutenga pesa mnatufananisha sisi na sehemu ambayo watu wakichimba hata na mkono kama panya hapa wanapata maji, huu utalaam unatoka wapi? Muwe mnaangalia, lazima muwe na usawa kwamba sehemu zingine maji hayapatikani kirahisi. Kwa hiyo Ndugu zangu tunaombeni sana... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)