Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima, ninayo machache katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitambue kazi nzuri sana inayofanywa na Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hii wamekuwa wakitusikiliza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninayo michango miwili, ama mitatu kutoka Jimboni kwangu. Kwanza ni mradi wa Kawa uko Nkundi. Mradi huu unasimamiwa na Wizara moja kwa moja na umeanza miaka minne, mitano iliyopita wananchi wanasubiri maji. Umetumia zaidi ya shilingi bilioni tatu, tangu ujenzi wa chanzo chake, wananchi tumewaaminisha kwamba mradi huu karibu wanapata maji, mpaka sasa Mheshimiwa Waziri bado hawajapata maji. Ujenzi wake umekamilika na nilifika ofisini kwako kukuelezea juu ya changamoto zinazojitokeza, leo hii nilikuwa naongea na wannchi bado maji katika kijiji cha Nkundi hawajapata maji, lakini Kalundi wamepata maji na wao wanasema maji yanachukua muda mrefu sana kujaa kwenye tank kwa hiyo kwa vyovyote vile kuna changamoto ama za kimfumo, mfumo wa kusukuma maji au njia yenyewe.

Kwa hiyo, ninaomba watalaam wa Wizara wausimamie huu mradi vizuri kwa sababu umetumia pesa nyingi na ikiwezekana mradi huu ukitoa maji vizuri upeleke na maji kijiji changu cha Miula itakuwa imesaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi mwingine wa mradi wa Isale. Mradi huu una changamoto ya fedha, mkandarasi amesha-raise certificate sasa hivi tunaomba pesa, nilikuja hapo Wizarani Mheshimiwa Waziri ukaniahidi kwamba hivi karibuni utatoa. Tunachotaka kuwaeleza ni kwamba huu mradi ni muhimu sana unabeba vijiji zaidi ya sita na kama mkiupa pesa maana yake ile asilimia ambayo tunatoa maji katika Wilaya yetu itapanda kidogo. Vijiji vya Nkata, Ntemba, Kitosi, Ifundwa na Ntuti vinakusudia kunufaika na mradi huu, shida yake ni pesa. Mtuharakishie pesa ili mkandarasi aweze kuendeleza ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni Mradi wa Mpasa mradi huu wa pia unaendelea vizuri. Mkandarasi sasa hivi amesimama kidogo kwa kukosa pesa lakini anadai vilevile certificate yake ili aweze kuendeleza mradi wenyewe. Mradi huu tunaomba utakapokamilika utapeleka maji King’ombe, Kilambo, Mlambo na tunaomba upeleke Kilambo upeleke na Kapumpuli utatusaidia sana. Maeneo haya ya mwambao huwa yanapata kipindipindu kila wakati, kwa hiyo utakuwa msaada sana na ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maombi pia mapya, niliwahi kuzungumza hapa Bungeni, katika Vijiji vya Kasu, Katani, Milundikwa na Kantawa ili ku-support pia sekondari mpya ya Milundikwa, mradi huu unahitaji watalaam na timu ya watalaam iende nimeandika na barua kwa Wizara, naomba itusaidie kupeleka timu iende ikachunguze, siyo huu tu wajaribu tena kunisaidia katika Kijiji cha Nkana, kijiji cha Sintali na kijiji cha Mkomachindo ambao wana sekondari pia hawana maji ya kutosha yanayoweza kusaidia. Kijiji cha Sintali muda mrefu sana wanatumia maji ya Madimbwi, wana chanzo kizuri lakini haijawahi kusaidiwa. Naomba Wizara iniangalie katika hilo na nimeandika barua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine muhimu ni mradi wa maji ya Mserereko wa Wampembe. Mji mdogo wa Wampende hauna maji na una kituo cha afya na watu wengi wa kutosha, lakini ndiyo maeneo ambayo chanzo cha magonjwa ya kipindupindu yanaanzia kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika. Mradi ule Halmashauri wameanza kuufanyia kazi, tunaomba support ya Wizara ya kitaalam na kifedha ili uweze kusaidia Vijiji vya Kizumbi, Ng’anga, Katenge, Wampembe na Ng’undwe unaweza ukatusaidia sana. Lakini vijiji kama Mwinza, Izinga, Lusembwa na Itanga hawana maji, naomba sana watusaidie. Vipo vijiji pia vya Kacheche na vijiji vingine vina visima ambavyo tunaomba pia mtusaidie katika uchimbaji na ukamilishaji wa visima vile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji Mdogo wa Chala una chanzo kizuri cha maji, kinatakiwa kiongezewe tu, kuna kisima kilichochimbwa muda mrefu kiongezewe kwenye chanzo kinachotoa maji sasa ili maji yaweze kutosheleza Mji wa Chala na jambo hili ni pesa kidogo tu itahitajika kwa sababu kisima tayari kimeshachimbwa na miundombinu ipo inayotumika mpaka sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho ni suala la umwagiliaji. Nimezungumza juu ya bonde la Mto Kate, bonde la Mto Namansi kuna vyanzo vya umwagiliaji na miundombinu yote na michoro na utaratibu wote wa kihandisi ulishafanywa na Halmashauri kwa gharama kubwa na kuletwa kwenye Kanda, tunachosubiri ni pesa ili tuanze ujenzi wa miundombinu. Nilitegemea kwenye bajeti hii nitaona huu mradi sasa sijui kwa nini. Ninaomba Wizara na watalaam wa Wizara wawe wanapitia michango ya Wabunge, haiwezekani mradi mmoja unazungumzwa mara kumi. Nazungumza kila wakati huu mradi kwamba Halmashauri imetumia gharama kubwa saa katika mradi huu lakini bado hatujaanza umwagiliaji katika maeneo yote mawili ya Kate pamoja na Wamanse.

Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise Wizara inafanya kazi vizuri, naunga mkono hoja na ninapongeza utendaji mkubwa sana wa Wizara na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.