Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shaurimoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Maji. La kwanza, niipongeze sana Wizara pamoja na watendaji wao wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni muhimu, maji ni uhai wa binadamu mpaka wanyama. Mimi nitachangia kwa kuanza na Mamlaka za Maji na madeni ya taasisi za Serikali. Taasisi za Serikali zinadaiwa fedha nyingi na Mamlaka zetu za Maji, inafika wakati hizi mamlaka zetu zinashindwa kujiendesha. Niiombe sana Serikali, la kwanza iweze kulipa pesa hizi za Mamlaka za Maji ili ziweze kujiendesha kwa ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi zetu za Serikali zinadaiwa fedha nyingi na Mamlaka za Maji inafika wakati mamlaka hizi haziwezi kujiendesha kabisa. Ni jambo la ajabu sana, mamlaka zinalalamika zinasema zikilipwa fedha na taasisi hizi zinaweza kujiendesha wao wenyewe. Ni jambo la ajabu sana ni kwa nini Serikali isiweze kulipa pesa hizi kwa Mamlaka za Maji ili hizi mamlaka ziweze kujiendesha kwa ufanisi zaidi na wakiweza kujiendesha maana yake ni kupunguza mzigo kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, leo nina mambo machache, ni suala la shilingi 50 kuongezwa katika petroli na dizeli. Suala hili tunaiomba sana Serikali, lazima ifanye jitihada zake zozote zihakikishe inaongeza shilingi 50 kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna muarobaini wa tatizo la maji kwenye nchi hii isipokuwa kuongeza shilingi 50. Nashangaa kwa nini Serikali haiwezi kukubaliana na maoni ya Wabunge wake. Sisi Wabunge tukisimama hapa kuchangia, siyo kama tumesimama Wabunge ni wananchi wa Tanzania ndiyo wamesimama hapa wanaishauri Serikali. Wametuleta hapa kazi yetu ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Mimi nashangaa sana, Serikali yetu hii kama Wabunge tunachangia, tunaishauri lakini haitaki kusikiliza mawazo yetu sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, suala la kuongeza shilingi 50 kwenye mafuta ya petroli na dizeli lipewe kipaumbele ili tuweze kufika hatua ambayo tunaitaka. Ukiangalia bajeti iliyopita, asilimia 80 ya miradi ya maendeleo imefanywa na Mfuko wa Maji, siyo pesa za Serikali ni Mfuko wa Maji. Tukiongeza shilingi 50, tukiwa tuna shilingi 100, tutafika mahali pazuri. Niiombe sana Serikali yangu, mimi naamini Serikali hii sikivu, Waziri wa Fedha yupo nimwombe aweze kulichukua hili jambo liweze kufanikiwa ili wananchi wetu waondokane na kadhia ya maji waliyo nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuligusia ni suala la DAWASCO kuunganishwa na DAWASA. Ni jambo zuri sana limefanywa, Serikali imewaza jambo zuri lakini je, wamefanya tathmini ya kina jinsi ya kuendesha maana ziko mamlaka mbili kwenda mamlaka moja? Je, Serikali imefanya tathmini ya kina kuhusu gharama za uendeshaji hasa katika suala la mishahara, lazima tuliangalie kwanza. Kama sisi Kamati hatukuletewa lolote na tumewaomba Wizara waweze kutuletea ili tujue, je, kuondoka kuwa mamlaka mbili na kuwa mamlaka moja kuna-benefit yoyote? Isijekuwa tunaondoa baadae tukawa tunapata hasara katika Serikali yetu tukaja tukataka turejeshe. Niiombe Wizara ikae chini iweze kufanya tathmini ili tujue tunakwenda kwenye faida au hasara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pesa za India. Hizi pesa hata na mimi kule Zanzibar kwa kuwa niko Mkoa wa Mjini nitafaidika nazo sana. Niiombe sana Serikali, sijui pana tatizo gani, hebu Serikali ituambie, hizi fedha zina tatizo gani? Huu mwaka wa tatu tunazichangia hizi fedha ndani ya Bunge hili. Fedha hizi hazipatikani, tunashindwa kusaini, sijui kuna tatizo gani? Kuna tatizo gani hapa ili hizi fedha ziweze kupatikana kwani zikipatikana tunaweza kutatua tatizo kubwa sana la maji kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni la Tume ya Umwagiliaji. Tume ya Umwagiliaji bado ni tatizo lakini ili kuondoa matatizo ya Tume naiomba Serikali leo hii iweze kunisikiliza kwa makini. Naishauri Tume hii iondoke kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji ipelekwe kwenye Wizara ya Kilimo. Hili ni jambo jema sana, tukiiondoa Tume hii kutoka katika Wizara ya Maji tukaenda nayo katika Wizara ya Kilimo ndiyo hasa yale mahitaji ya wananchi wetu yatafika mahali tunapotaka. Tume hii ikibakia kwenye Wizara ya Maji na Tume hii shida yetu ni wakulima na maendeleo kwa wakulima bado itakuwa ni shida. Tunaomba sana Serikali iiondoe Tume hii kutoka kwenye Wizara ya Maji ielekee kwenye Wizara ya Kilimo hapo ndipo tunaweza tukapata mafanikio katika nchi yetu kutokana na Tume hii ya Kilimo kwa sababu itafika pale ambapo wanataka iwaguse wananchi. Tukiibakiza katika Wizara hii tutakuwa tuna wakati wa kufanya zero na pasipo na Tume ya Umwagiliaji, ikafanya kazi vizuri kwenye nchi hii hapana kilimo wala hakuna maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.