Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa niweze kuchangia kwenye bajeti muhimu sana ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilio cha maji kwa Watanzania ni kilio kikubwa sana na ukiangalia hata siku ambayo maswali ya maji yanazungumziwa humu ndani ya Bunge hili almost karibu robo ya Bunge wanasimama kwa ajili ya kuuliza masuala ya maji. Hii inaonesha ni jinsi gani Taifa kwa ujumla tuna shida kubwa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jaribu kuangalia jinsi taratibu za kutatua changamoto ya maji na hii kampeni ya kwenda kumtua mama maji kichwani sioni kama inaenda sambamba na fedha zinazotolewa. Ukiangalia kwa kweli kwa asilimia 54 inayotengwa, tutenge shilingi bilioni karibu 623, tutoe shilingi bilioni 349 kwa speed hii kampeni itafanikiwa lini? Hili ni tatizo. Lazima Serikali iamue kwa uhakika kwamba tunataka sasa kuondoa tatizo la maji nchini, kama tulivyopanga kwa masuala ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumzia habari ya vijiji karibu zaidi ya asilimia 80 zinaenda kupata umeme, hivyo hivyo kwenye maji lakini speed ni ndogo leo na kila siku tunalia hapa Bungeni ni shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa speed tunayoenda nayo kama hatuna mkakati maalum kuja na Wakala kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wenzangu na naunga mkono Wabunge waliozungumza suala la wakala. Hatuwezi kuondokana na kero ya maji na akina mama wanateseka, hawaingii kwenye shughuli za maendeleo, hawaendi kulima hawaendi kwenye miradi yao midogo midogo, watoto wetu wa kike hawasomi kwa muda wanaenda kufata maji kisimani ndiyo waje waingie darasani, hatuwezi kuwatoa Watanzania mahali walipo kwa speed hii tunayoenda nayo ni ndogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la umwagiliaji. Serikali tumekuwa na malengo, almost karibu miaka mitano sasa kuweza kuwa na heka milioni moja kwa ajili ya umwagiliaji. Lakini nenda kwenye vitabu, leo mmeona vitabu vyote hapa karibu vinne vya miaka minne mfululizo angalia inayotengwa yaani kwa mwaka mmoja tuna hekta 6.7, 7.2 ni aibu, kwa nchi ambayo inategemea kilimo kwa hatua kubwa. Tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda, tunafahamu tunataka kwenda kwenye umwagiliaji kwa speed hii tunayoenda nayo itachukua muda wa miaka karibu, nilikuwa nafanya mahesabu ya haraka hapa, kwa speed tunayoenda nayo, ukiangalia 2016 hekta za umwagiliaji tunaenda 7000.02; mwaka 2017 ni hekta 6,712 kwa hiyo ukiangalia trend hiyo ili tuweze kufika milioni moja hekta tunahitaji karibu miaka 50, hivi tutakuwepo?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali lazima tuamue tunakwendaje kwenye uchumi wa viwanda wakati hatuwekezi vya kutosha kwenye umwagiliaji, bado ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la upotevu wa maji, ukiangalia speed ya upotevu wa maji wakati tunalia hatuna maji, hata mijini watu hawana maji, vijijini watu hawana maji asilimia 33 ya maji yanapotea, hayatumiki na mengine tumeshaingia gharama za walipa kodi. Kwa hiyo, naiomba Serikali lazima ije na mpango maalum, waweke utaratibu maalum wa kuboresha miundombinu mingi imechoka, miaka 20, miaka 30, miaka 50 leo ukienda baadhi ya maeneo unakuta maji yanamwagika barabarani. Inaumiza wananchi wako wanapokuwa hawana maji unafika maeneo unakuta maji yanamwagika barabarani hayatumiki, ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Waziri aje na mkakati, awe na utaratibu maalum, regularly mpango wa kurekebisha mabomba yaliyochakaa kuhakikisha kwamba maji hayapotei yanayopatikana yakatumike kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la charge za maji. Kwenye gharama za maji tumeweka kitu kinaitwa service charge kama ilivyokuwepo kwenye umeme hizi Mheshimiwa Waziri hazimsaidii Mtanzania, zinamuumiza. Hizi service charge kwenye maji wakati tayari bili analipa bili nzima na kama analipa maji taka yapo, leo mnaweka tena na service charge tunaomba iondolewe kama ilivyoondolewa kwenye umeme ili kupunguza gharama za maji kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la maji kutoka Mwanza kuja Mkoa wa Tabora. Tulifurahi sana tukajua kwamba sasa Mkoa wa Tabora japokuwa haifiki Kaliua na Urambo angalau shida kubwa ya maji inaondoka. Lakini jaribu kuangalia kwa miaka mitano tumetekeleza kwa asilimia 17 ya utekelezaji wake, ili mradi huu ukamilike utahitaji karibu miaka mingapi, karibu miaka labda kumi. Hivi kweli kama ni mpango mkakati, kama ni mradi wa kimkakati kwa speed hii ya asilimia 15 ya utekelezaji, nasikitika sana kwa kweli hii pengine hatutakuwepo wakati huo.

Naiomba Serikali kwa kuwa huu ni mradi ambao unaenda kulisha karibu Wilaya tano za Mkoa wa Tabora na kilometa 12 pande zote ambazo bomba linapita iwekewe fedha ya kutosha ili speed yake iongezeke na itengewe muda maalum, tuambiwe sasa kwamba mradi huu utakamilika lini? Lakini kwa asilimia inayokwenda nayo bado ni ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee Kaliua, mimi nasikitika na kiukweli natamani kupiga yowe hapa kwenye hili Bunge. Ninaongea kila siku habari ya Kaliua, nimesoma hiki kitabu page by page, line by line Kaliua huku haimo, Mheshimiwa Waziri huoni hata huruma, Kaliua haimo, hivi Kaliua hawaishi watu? Mradi pekee ambao umetoka Kaliua ambao hauonekani wanasema kwamba Mradi wa Maji Kaliua, kata mbili, Kaliua na Ushokora mradi unaotekelezwa na Mkoa. Fedha haionekani, kuptoka wapi haionekani, wala ni lini haijulikani.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na mradi Waziri mwaka jana alisema kutoa maji Malagarasi kuleta Kaliua na Urambo, ukiangalia imetengewa shilingi milioni 500 na nimeongea na Waziri akasema siyo mradi wa leo wala kesho. Sasa mpango wa kupatia maji wananchi wa Kaliua uko wapi? Leo kama unazungumzia habari ya kata mbili za Kaliua na Ushokora. Kaliua ina Kata 28, ina vijiji 101, ina vitongoji karibu 460, leo unazungumzia habari ya kata mbili na hakuna mradi mwingine wowote hatuko kokote, kwenye visima hatumo, kwenye mabwawa hatumo, kwenye miradi ya quickwins hatumo, kwenye miradi ya mkakati hatumo, miradi mikubwa hatumo, hivi Kaliua wanaishi watu wa aina gani?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ukija unijibu kwa nini kwenye kitabu hiki Kaliua umewasahau, kuna baadhi ya Wilaya nimeangalia huku mpaka inauma. Wilaya ina miradi yote kwenye visima wamo, kwenye mabwawa wamo kila mahali wamo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana walikuja mradi wa kuchimba visima pamoja na mabwawa, wakaainisha maeneo ya kimkakati kuweka mabwawa saba, nimeshangaa huku hamna hata bwawa moja, hii kwa kweli muone aibu Serikali. Naomba Mheshimiwa Waziri uniambie kwa habari ya Kaliua kama wanawake wa Kaliua wataendelea kuteseka na maji miaka mingapi nijue, hata kama mimi siyo Mbunge lakini wana Kaliua wana haki ya kupata maji, wanalipa kodi kama Watanzania wengine, akina mama wale wanataka wafanye shughuli za maendeleo, lakini kwa speed hii mimi nakataa kwamba Kaliua haijatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri na nikuombe bajeti ikiisha twenda Kaliua ukaone mateso wanayopata wale watu, kwa kweli ni maumivu makubwa sana, yaani hata bwawa jamani ni kweli kwamba ardhi yetu haina maji chini na hata visima vya Mradi wa World Bank hatukunufaika navyo kabisa kwa sababu hatuna maji chini. Hata kutuwekea mabwawa ili mvua zinaponyesha tukusanye tuyatumie, inasikitisha, inaumiza sana, sijui nitumie lugha gani!(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilijua kwa kilio changu miaka yote inakwenda kwa Waziri tungeangaliwa angalau mwaka huu lakini inasikitisha sana, kwa kweli inaumiza sana. Mradi wa Malagarasi haujulikani, Mheshimiwa Waziri ukija hapa Bungeni na mimi nang’ang’ania shilingi yako mpaka nijue wannchi wa Kaliua wanapatiwaje maji, karekebishe bajeti, haujatutendea haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.