Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii muhimu kwa maendeleo ya Watanzania. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Waziri wa Maji, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Naibu wake, Mheshimiwa Aweso na timu nzima kwa kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma muhimu ya maji. Nawapongeza sana na nawatia moyo waendelee kufanya kazi hiyo pamoja na changamoto zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu kusema kwamba maji ni uhai, shughuli nyingi zinategemea uwepo wa maji. Viwanda, kilimo, mifugo na binadamu wote uhai wake ni maji. Waathirika wakubwa wa ukosefu wa maji ni wanawake, wanawake hawa wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji na hivyo kutokushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na wakati mwingine kuhatarisha ndoa zao kwani hutoka usiku sana kutafuta maji hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Maji inamtaka mwananchi kutembea umbali wa mita 400 ili kuweza kuyapata maji. Kwa Mkoa wa Singida maeneo mengi ya vijijini imekuwa ni kinyume, wanatembea umbali mrefu hasa wanawake waishio maeneo ya vijijini kuyasaka maji. Kwa kuwa tunaelekea Tanzania ya viwanda, niombe sana maeneo haya ya vijijini yaweze kupatiwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo inakua kwa kasi, lakini inapata mvua kwa msimu mmoja kwa mwaka. Hivyo basi naiomba Serikali kuja na mkakati mahsusi wa kuchimba mabwawa ya kuweza kuhifadhi maji kwa mwaka mzima ili kuwawezesha wanawake ambao ni wakulima wazuri wa mazao ya biashara na chakula kuweza kulima kwa muda wa mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kwa kutupatia fedha katika miradi ya maji ya vijiji kumi vya Mbwasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Niiombe iongeze juhudi zaidi kupeleka fedha katika mpango wa pili wa ukamilishaji wa mradi huo.

Pia naishukuru sana Serikali kwa kutupelekea fedha katika Mradi wa Maji wa Uliyampichi uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, lakini changamoto iliyopo katika mradi huo ni kwamba hakuna pump na fedha za kuweza kuunganishwa na umeme ili uweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini kuna Mradi wa Maji wa Kijota, lakini mradi huo umekuwa ukitumia pump ya dizeli ambayo kwa sasa imeharibika. Niiombe sana Serikali iweze kupeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 94.6 ili basi waweze kutumia pump ambayo itatumia umeme na kwa kuwa kuna miundombinu ya umeme mradi huo uweze kuunganishwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi kilichopita nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya LAAC na kazi kubwa tuliyokuwa tukifanya ni kukagua miradi ya maendeleo na mingi ilikuwa ni ya maji, lakini changamoto kubwa tulizokuwa tukikutana nazo ni miradi mingi ya maji kutokukamilika kwa wakati au utakuta miradi mingine imekamilika lakini haifanyi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninao mfano hai kwa Mkoa wangu wa Singida wa Mradi wa Unyanga na Mradi wa Mchama B, ni miradi ambayo imetumia mamilioni ya fedha za walipa kodi lakini haifanyi kazi. Namuomba Waziri wakati wa majumuisho atuambie ni kwa nini miradi ya maji ambayo imetumia fedha nyingi za walipa kodi haifanyi kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Itigi unakua kwa kasi lakini hauna kabisa mtandao wa maji. Naiomba Serikali iangalie vile visima ambavyo tayari vimechimbwa basi ipeleke fedha za kutosha ili kuweza kuunganisha miundombinu na mji huo uweze kupata maji ya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, nakushukuru sana, mengine nitachangia kwa maandishi, ahsante sana.