Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninapenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Maji chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, kazi wanayofanya ni kubwa sana, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo naomba nieleze changamoto kadhaa wanazopitia wakazi wa Mkoa wa Manyara hasa wanawake kwa kuwa wao ndiyo wanaopata adha kubwa ya utafutaji wa maji kwa ajili ya familia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua juhudi kubwa zilizofanywa na Wizara ya Madini ya kujenga ukuta katika eneo la Simanjiro Kata ya Mererani kwa nia njema ya kuhifadhi madini yetu. Wananchi wa kata nne zinazozunguka ukuta huo ambazo ni Marerani, Naisanyai, Endiamtu na kadhalika walikuwa wanapata maji kutoka Tanzanite One lakini hivi sasa hayo maji yapo ndani ya ukuta ambako movement za kuingia ndani ya ukuta ziko monitored sana, hivyo ningeomba Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Halmashauri ili mabomba yatolewe nje ya ukuta na wananchi waweze kuendelea kupata maji kama ilivyokuwa mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia suala hili hali ni tete zaidi kwa vijiji vya Emishiye na maeneo ya jirani na vijiji hivyo kwani ukuta wa Mererani una kilometa za mraba 24.5 ili akinamama wa Emishiye wapate maji hayo yaliyoko ndani ya ukuta wanatembelea kilometa zaidi ya 30. Akinamama ndiyo gumzo ya uchumi wa familia yoyote, sasa kama mama anatumia saa 12 kutafuta maji? Maji yenyewe haya ninayozungumzia si kwamba ni maji mazuri kwa kiwango hicho, maji haya yana floride, mifugo na wanyama wanaotumia maji haya wamepinda miguu na kung’oka meno kabla ya umri wao.

Naiomba Serikali yangu sikivu iwaonee huruma wakazi hawa wa Simanjiro ili waweze kupatiwa maji kutoka West Kilimanjaro ili wapate ahueni ya maradhi yanayosababishwa na madini haya ya floride. Kwa sasa wakazi hawa wananunua ndoo moja ya lita 20 kwa shilingi 500 gharama hii ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya ukosefu wa maji ni kubwa Mkoani Manyara, Wilaya ya Kiteto ni moja ya Wilaya zinazoongoza kwa ukame zifanyike juhudi za makusudi ili kutega maji haya ya mvua yanayopotea ili kupata mabwawa yatakayosaidia watu na mifugo wakati wa kiangazi. Wilaya ya Babati, Kata ya Singu tuna shida kubwa ya maji tunaomba msaada wa Wizara yako kama tunaweza kupata maji kutoka BAWASA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naomba kuunga hoja mkono.