Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya kumtua mama ndoo kichwani. Nampongeza Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwa kazi kubwa anayoifanya akishirikiana na Naibu Waziri. Kwa kweli Mheshimiwa Kamwelwe (Waziri) na Mheshimiwa Aweso wamepewa Wizara stahiki na wanaitendea vema Wizara hii, ni imani yangu kuwa ifikapo mwaka 2020, vijiji vingine na mitaa mingi nchini itafikiwa na huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai lakini pia maji ni maendeleo. Shughuli zote za kibinadamu na uhai wetu unategemea sana uwepo wa maji. Akinamama nchini wanatumia muda mwingi kutafuta maji kwa ajili ya kupika na matumizi mengine ya nyumbani. Wanafunzi mashuleni wamekuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji na hii imekuwa ikiathiri taaluma. Kwa kuwa tulishakuwa na shilingi 50 kwenye kila lita ya mafuta na matokeo yake tumeyaona, bajeti ya maji imekuwa ikiongezeka na miradi ya maji mjini na vijijini ikiongezeka pia. Hivyo napendekeza tuongelee tozo toka shilingi 50 kwenda shilingi 100 ili bajeti iweze kuongezeka. Naamini tukiongeza shilingi 50 tena vijiji vingi na mitaa mingi itapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni nchi yenye baraka au imebarikiwa sana, tunapata mvua nyingi sana ambazo zimekuwa zikisababisha mafuriko na uharibifu mkubwa wa miundombinu na majengo. Kuna baadhi ya nchi, mvua nyingi ni fursa za kimaendeleo. Nashauri maeneo yenye mvua nyingi ufanyike utaratibu wa kuvuna maji haya ili yatumike wakati wa kiangazi. Maeneo kama Mkoa wa Dodoma, Singida, Tabora, ungeanzishwa mradi wa uvunaji wa maji ya mvua na ujenzi wa mabwawa makubwa kwenye mabonde kama ya Fufu na mabonde mengine. Maji haya yakivunwa yanaweza kutumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji au matumizi ya nyumbani wakakti wa ukame.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imekuwa ikipata fedha kidogo sana kwa ajili ya miradi ya maji ukilinganisha na Halmashauri nyingine nchini. Vijiji vingi vya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Vijijini haina maji ya bomba pamoja kuwa na vyanzo vingi vya maji. Mfano Vijiji vya Matiganyoro, Myombo, Kichiwa, Upani, Ilengititu, Taganende, Kivitu, Lima, Isitu, Havaiga, Isohivaye, Kanikelele, Igombole, Ikang’asi, Welela, Sovi na Iyembela. Lakini naishukuru Serikali kwa kutenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, naamini fedha hizi zikitoka zitapunguza kero kubwa ya maji katika Jimbo la Lupembe na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo kubwa la usimamizi wa miradi ya maji. Wakandarasi wengi wamekuwa wakitengeneza miradi hii chini ya kiwango na kwa kutumia gharama kubwa. Ni muhimu Wizara hasa Waziri wa Maji na wataalam wa Wizara kuwa jirani na miradi hii, kuwa na ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kusitokee ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya kandarasi wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kumpongeza Mheshimiwa Rais, Waziri wa Maji, Naibu Waziri na wataalam wa Wizara ya Maji kwa kusimamia na kufuatilia miradi ya maji. Hii itatusaidia kukua kwa uchumi wetu kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja iliyopo mezani.