Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Silvestry Fransis Koka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Nichukue nafasi hii kwanza kuishukuru sana Serikali yetu ya Chama cha MapinduzI kwa kazi nzuri inayofanya. Wizara ya Viwanda imekuwa ikijitahidi kwa hali mali ili kuhakikisha Sera yetu ya Viwanda inakua. Nichukue kweli nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kujitoa na kujitolea kwa ajili ya wananchi wa Tanzania kuhakikisha Watanzania wenyewe tunajenga viwanda na tunakwenda kushika hatamu za uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nitoe pongezi kwa kazi kubwa ya kujenga miundombinu mbalimbali kwa sababu kupitia miundombinu hii ndiyo tunaweza kujenga uchumi wa kati na hata uchumi mkubwa. Mifano iko wazi, ujenzi wa reli, ujenzi wa miundombinu ya umeme kama Stiegler’s Gorge ni jambo ambalo tunahitaji tumuunge Mheshimiwa Rais mkono kwa nguvu zetu zote.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mojawapo ya changamoto tuliyonayo katika uanzishaji wa viwanda ni pamoja na nguvu za kusukuma au kuendesha viwanda kwa maana ya umeme. Ndugu zangu wote tunafahamu kwamba umeme unaozalishwa kwa maji ni rahisi kuliko umeme mwingine wote. Kwa hiyo, tutakapopata umeme mkubwa unaozalishwa na maji kutoka Stiegler’s Gorge maana yake ni kwamba hata gharama za uzalishaji zitapungua, tutaweza kuzalisha kwa gharama nafuu na hatimaye kufikisha bidhaa kwa wananchi kwa gharama iliyo nafuu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndugu zangu wafanyabiashara wa Tanzania na Watanzania wote tumuunge mkono Rais, tujitokeze tujenge viwanda, tuunge mkono miradi ambayo ipo mbele yetu ili siku ya mwisho jihitada za kwenda kwenye uchumi wa kati ziweze kukamilika bila tatizo lolote.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ina sababu hasa ya kutazama sasa balance ya biashara ya ndani nje. Tuangalie na tuweze kuona ni namna gani tunapoanza sasa kulea viwanda vyetu tuna balance pamoja importation ya bidhaa muhimu kwa ajili wananchi. Kwa sababu lengo la biashara pamoja na kupata faida na kulipa kodi lakini ni kuwafikishia wananchi bidhaa kwa bei iliyo nzuri, nafuu na ubora. Sasa kama hatutarudi tukaangalia bado kuna watu wachache wata-take advantage na wananchi wataendelea kununua bidhaa kwa gharama kubwa na wao kujilimbikizia faida kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kuwepo na balance kati ya bidhaa zinazoletwa kutoka nje na zinazozalishwa ili yale mabadiliko ya bei ya uzalishaji na malighafi yaweze kumnufaisha vilevile mwananchi ambaye ndiye mtuamiaji. Nina imani kwa kufanya hivi tutatimiza azma ya Serikali ya kumhudumia na kumsaidia mwananchi wa kipato cha chini.

Mheshimiwa Spika, kujenga viwanda ni jambo moja lakini kuviendesha ni jambo lingine ambalo ni gumu zaidi. Nitoe mfano wa kiwanda kinachozalisha viuadudu pale Kibaha. Kiwanda hiki kilianza kujengwa mwaka 2010 kikakamilika 2015 na kikaanza uzalishaji 2016. Kiwanda hiki ni cha pekee Afrika na kina uwezo wa kuzalisha viuadudu au viatilifu vinavyoua viluilui vya mbu kiasi cha tani milioni sita kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini navyoongea na wewe kuanzia kilipoanza kufanya kazi mwaka 2016 hadi leo kimezalisha tani laki nne tu na hakuna wanunuzi. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba tarehe 22 Juni, 2017

Mheshimiwa Rais alipotembelea viwanda Kibaha alikitembelea kiwanda hiki na alifurahishwa sana na kiwanda hiki kwa sababu ndiyo njia pekee ya kumaliza malaria nchini. Alitoa maagizo kwamba kila halmashauri inunue dawa hii iweze kutumika kuuwa viluilui vya mbu na tuangamize malaria hapa nchini. Tangu kipindi kile katika ya halmashauri 81 ambazo walichukua dawa hii ni halmashauri 25 tu ndizo ambazo zimelipa, nyingine hawajalipa kiwanda kinaendelea kudorora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dawa hii ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kama hamuifahamu kazi yake inashambulia viluilui vya mbu katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo maji yamesimama na kuhakikisha kwamba mbu hawawezi kuzaliwa. Nafikiri hii ndiyo njia pekee ya kumaliza malaria badala ya kutumia fedha nyingi kununua dawa kwa ajili ya malaria. Dawa hii ni nzuri sana, kwanza kabisa ni environmental friendly, yaani siyo kama dawa nyingine mfano DDT na nyingine tunazotumia kiasi kwamba unaweza hata ukainywa. Watengenezaji wali- demonstrate mbele ya Mheshimiwa Rais kwa kunywa ile dawa, haina hata madhara hata ukiinywa lakini ni sumu kwa viluilui vya mbu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa makusudi kabisa imetenga fedha nyingi kwa ajili ya huduma ya dawa na afya za Watanzania kutoka bajeti ya shilingi bilioni 30 mpaka shilingi bilioni 200 kwa ajili ya dawa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba malaria inapigwa vita nchini. Sasa tunachoangalia ni watu tumeangukia, ndiyo tunahangaika kutibu malaria hatutaki kuangalia ni wapi tumejikwaa na tutapojikwaa ni kung’atwa na mbu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kama kweli tunataka kusaidia viwanda vyetu vya ndani kiwanda ambacho kimejengwa kwa ushirikiano au kwa msaada kati ya Cuba na Tanzania ambacho hadi sasa tayari wenzetu wa Angola, Nigeria wameshaanza kupata hamu na kuleta order kwa ajili ya dawa hii, tusaidie kiwanda hiki kizalishe dawa na bajeti ya Wizara ya Afya itengwe kwa ajii ya kulipia dawa hizi kwa sababu lengo letu ni kuangamiza mbu si kuendelea kila siku Watanzania wanaugua tunahangaika kuwatibu kwa gharama kubwa. Niombe sana Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikiane na Wizara ya Afya ili waweze kununua dawa hizi, Watanzania wapewe elimu ya kuzitumia na hatimaye tuangamize mbu na Tanzania iwe free from malaria. Inawezekana, kiwanda tunacho, tutachekwa kama tutaendelea kuugua malaria na wakati tulishajipanga hadi kuweza kujenga hiki kwa gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki hakijasimamiwa vizuri, kiko chini ya NDC, lakini hadi sasa hakina hata Bodi ya Wakurugenzi sasa kinajiendeshaje? Kina wafanyakazi, uzalishaji ni duni na hakuna anayekiangalia ipasavyo matokeo yake tunakwenda kwenye hasara na tunatoka sasa nje ya azma na sababu ya Tanzania ya viwanda. Ni wazi kama kitasimamiwa kina uwezo mkubwa sana wa kuuza bidhaa hii ndani na hata nje ya nchi yetu na kikailetea Serikali mapato makubwa ya kigeni kwa sababu kiko pekee Afrika na dawa inayotengeneza ni pekee ambayo inakwenda kulenga mbu na kumwangamiza na kuhakiksha kwamba malaria haitaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na kuhimiza ujenzi wa viwanda vilevile tushiriki katika kuhakisha viwanda hivi tunavisimamia, tunavisaidia ili viweze kuleta tija na hatimaye tuweze kufikia malengo makubwa ya Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwaasa wafanyabiashara wenzangu Tanzania, kama nilivyosema lengo kubwa la biashara mbali ya kulipa kodi na kupata faida ni kumhudumia Mtanzania. Tuna wajibu wa kuhakikisha tunapopeleka bidhaa katika masoko ya Mtanzania tunamlenga Mtanzania apate nafuu katika bidhaa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameshanyoosha mkono kwa wafanyabiashara, ameamua kutuunga mkono na kutusaidia na hata amekuwa akitoa maamuzi ya papo kwa papo kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania. Ametaka wafanyabiashara wa Tanzania tufanye biashara, tuzalishe, tujenge viwanda na tutumie soko la ndani na fedha za ndani kuboresha viwanda vyetu. Sasa kutokupeleka azma hiyo kwa wananchi na kuwafanya wananchi wakawa wanatapatapa wapate wapi mahitaji ni sawasawa na kuiudhi Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimalizie kwa kuomba tujitahidi twende sambamba na azma ya Mheshimiwa Rais na Serikali yetu. Naunga mkono hoja tuendelee kujenga nchi yetu ya viwanda.