Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekaa najiuliza swali moja, hivi hii Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo Tanzania ya Viwanda au ilikuwa ni Serikali ya Awamu ya Nne? Kwa sababu kinachofanyika sasa hivi, mwaka 2014/2015 katika bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge wenzetu walikuwepo humu waliipitisha, asilimia 82 ya bajeti ilipelekwa kwenye viwanda na vikaboreshwa. Leo 2015/2016 bajeti ya shilingi bilioni 35.3 tumepeleka shilingi bilioni 1.6 sawa na asilimia 5. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hiyo, mwaka 2016/ 2017 tumepeleka 8% ya bajeti nzima. Mwaka 2018 mpaka Machi, taarifa tuliyopewa kwenye Kamati tumepeleka asilimia 9.4 tu yaani hakuna mwaka ambao tumepeleka angalau asilimia 50 ya bajeti ya viwanda halafu tunajinasibu kwamba tunaenda kwenye Serikali ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala linanipa wasiwasi na ndiyo maana ukiona mtu anajitetea sana, ujue kuna maovu nyuma yake. Ndiyo maana ukiangalia viongozi mbalimbali wa Serikali wana matamko tofauti tofauti juu ya ni viwanda vingapi vimeanzishwa Tanzania mpaka leo hii?

Mkuu wa nchi anasema tumeanzisha viwanda zaidi ya 3,060, Waziri kwenye hotuba yake anasema kwamba ameanzisha viwanda 1,287, kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wanasema viwanda viko 50. Kila mtu anaongea statement yake, Serikali moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima ujichanganye kwa sababu Watanzania tumewaaminisha tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda. Laiti kama Watanzania wangegundua kwamba viwanda wanavyoahidiwa kwenye kampeni ni vya kutengeza juisi, zile blender, ni viwanda vya cherehani, sijui kama leo tungekuwa tunaongea haya maneno. Leo tumebadilishiliwa story tunaambia kwamba viwanda ni aina yoyote, vya kati na vidogo. Sawa, basi hivyo viwanda vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye ripoti ya CAG, SIDO wanaweza kutoa mikopo kwa asilimia 40 tu ya pesa ambazo walikuwa wame-propose kwamba wanatoa mikopo. Watu wanaoahidiwa watapewa mikopo kwa SIDO ndio hao wenye viwanda vya kati na viwanda vidogo lakini pesa hawapelekewi. Mheshimiwa Waziri anajitapa hapa ameanzisha viwanda vipya. Jamani, wengi hapa sisi ni wazazi. Hivi kweli mtoto wako hata kama una watoto wengi kiasi gani, mtoto wako mmoja akifa kwa kifo ambacho umesababisha wewe mwenyewe mzazi utajisikiaje? Viwanda vinakufa vidogo na vya kati, pesa hatupeleki halafu tunajinasibu kwamba tunatengeneza Serikali ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika bajeti ya mwaka 2018, hiyo 8% ninayosema imepelekwa siyo fedha za ndani, ni fedha za wafadhili, fedha ambazo tunapewa na watu wengine. Uangalie seriousness ya Serikali katika kukuza uchumi wa viwanda, wewe mwenyewe utaona kuna changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, ili viwanda viweze kukua, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba lazima tukuze malighafi, lazima tuhakikishe tunaboresha pamba, tumbaku na barabara. Shinyanga ni wakulima wakubwa wa pamba. Sisi mpaka sasa hivi tuna- export pamba tani 700,000. Yes, tunauza marobota 700,000 lakini tuna-import marobota ya nguo 2,000,000 kuleta Tanzania. Mbona tunafanya biashara kichaa? Kwa nini Serikali isiwekeze kwenye malighafi ili kukuza viwanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namweleza Mheshimiwa Waziri, hivyo viwanda anavyovitaja kwenye kitabu chake wanampigia makofi, anapiga nao picha, anatuma kwenye mitandao, hao watu wanamwangalia waone yeye ana commitment gani kukuza viwanda? Wale watu wamewekeza Tanzania lakini Waziri unathubutu kukaa na Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Miundombinu na Wizara ya Kilimo kuangalia utarahisisha vipi uzalishaji kwenye hivi viwanda? Au tunafanya majaribio ya kusema tumeleta viwanda na baada ya miaka mitano viwanda vimeshindwa kufanya kazi au viwanda vyote vimefungwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi viwanda anavyotuaminisha leo Mheshimiwa Waziri, hebu jiulize swali, vinaajiri Watanzania wangapi? Juzi nimesikia Mheshimiwa Waziri anasema kwamba cherehani tano ni kiwanda. Mheshimiwa Waziri tusifanye mchezo na Watanzania, wanatutegemea sisi Wabunge na Serikali kuamua hatima ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwangu Kahama, Shinyanga na Mikoa ambayo kimsingi ilikuwa imekaa strategic kibiashara, nikikueleza tangu Serikali yenu imeingia madarakani, zaidi ya asilimia 70 ya wafanyabiashara waliokuwa wanamiliki maduka na biashara wameshapokonywa mali zao na Serikali. Watu wana mikopo Mheshimiwa Waziri. Wewe unachekelea kuleta viwanda vipya, una mkakati gani kuhakikisha viwanda ambavyo vilikuwepo ambavyo kimsingi vilikuwa vinalipa kodi na vinaendesha Serikali unavi-maintain? Una mkakati gani wa kuhakikisha hawa watu pamoja na kutusaidia kuendesha Serikali, wanaendelea kuwepo kwenye circular ya uchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa nakaa namfikiria Mheshimiwa Waziri, sijui anaposema kwamba tuna viwanda 3,000 anakuwa ana-project nini? Kwa sababu kama mwisho wa siku Shinyanga pale kuna Kiwanda cha Nyama hakina uwezo wa kuajiri hata watu 2,000. Shinyanga leo maji na barabara ni changamoto, ng’ombe ndiyo kwanza mmekazana kupiga chapa mnakusanya ushuru wa Sh.5,000, umeme ndiyo kabisa, labda wanunue na power bank pale kwenye kile kiwanda, hali ni mbaya, lakini Mheshimiwa Waziri anajinasibu anasema viwanda vinaendelea, tunafanya vizuri, tunafanya vizuri wapi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka commitment ya Serikali, tutafanyaje kuhakikisha wawekezaji wa kati na wadogo ambao ni wafanyabiashara kwa Tanzania hii na ndiyo walezi wa Tanzania hii, wanarudi kwenye hali yao ya kiuchumi kuweza kuendesha nchi hii? Nataka commitment ya Serikali juu ya huu utaratibu wenu, mtu akiamka asubuhi, TRA inapanga leo tunatoza kodi kiasi hiki, kesho asubuhi wanasema kiasi hiki, nini commitment ya Serikali? Watu wanafunga biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa leo, huyo huyo ambaye ni sehemu ya Serikali, anasema mnaofunga maduka, fungueni, njooni mezani tuzungumze, tunaweza tuka-negotiate bei ya kulipa kodi TRA.

TAARIFA . . .

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, halafu naomba kitu kimoja, tukiwa tunawashauri muwe mnatusikiliza kwa sababu Tanzania nzima haiwezi kuja hapa kuongea, sisi ni Wawakilishi wa wananchi. Tena kwa taarifa yako, kule kijijini njoo kwangu watu wanapiga chapa ng’ombe mpaka Sh.7,000 siyo Sh.5,000, ninyi mmekaa hapa sisi tunatoka kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu suala la kiwanda, mimi kwa uelewa wangu, kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania, anapokuja kuwekeza Tanzania anapewa kitu kina tax incentive. Akipewa incentive, maana yake kwa kipindi cha muda fulani yule mwekezaji hatalipa kodi mpaka ambapo ule muda wa incentive uwe umeisha. Kama hiyo haitoshi, kuna kitu kinaitwa operational cost, yule mwekezaji yuko pale hana miaka miwili, amekuwa anafanya operation pale na halipi kodi kwa sababu anasema costs zake za uzalishaji hazijalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali wanatujia hapa na mazingaombwe eti wanatafuta mbia mpya, what about the incentive? Vipi kuhusu ile tax holiday mliowapa wale wawekezaji? Jamani nyie si mnajisema kwamba ninyi ni Wataalam, ni wataalam wa nini basi? Tusifanye siasa kwenye maisha ya Watanzania. Siasa hizi zitakuja kutuadhibu, makaburi yetu yatapigwa fimbo na wajukuu zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusijifiche nyuma kwa kusema kwamba Serikali inatafuta mbia. Mheshimiwa Waziri hata standard gauge miujiza hii hii ilifanyika. Tumeacha mkopo wenye riba ya asilimia 1.2 tumeenda kuchukua mkopo wenye asilimia 4. Unakaa unasema umekaa na wataalam wanakokotoa mimi sijui mahesabu au biashara, lakini kwa uelewa wangu tu wa kawaida, siwezi kufanya biashara ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali iwasaidie Watanzania, itengeneze miradi. Wakae pamoja, naamini Balaza la Mawaziri ni moja, wamsaidie Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara tutengeneze miundombinu kwa ajili kusafirisha malighafi na tuboreshe zao la pamba. Zaidi ya Watanzania milioni 16 wa Lake Zone wanalima pamba. Mheshimiwa Rais anasema hao ndiyo wapiga kura wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kilimo chetu tunategemea pamba. Hebu tuboreshe zao la pamba ili tuweze kufungua viwanda vya nguo na kufungua viwanda vya mafuta. Leo kelele za mafuta zisingekuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikitembea tu kidogo kilometa moja kutoka nyumbani, naona maua ya pamba yametanda kila mahali, leo tuko busy tunanunua ndege, tunajenga flyover, Tanzania siyo Dar es Salaam, Tanzania ina Mikoa zaidi ya ishirini na kitu. Tanzania siyo Dar es Salaam.