Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji. Nianze moja kwa moja kwa kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba aliyetufikisha hapa ni yeye mwenyewe Waziri kwa sababu mara nyingi anapoongea na kutaka kuli-address Bunge au hata ku- address Taifa amekuwa akitumia neno moja anasema mimi ni mzee wa sound. Hili jambo linamharibia yeye, lakini pia linatuharibia na sisi kama nchi. Hata hivyo wanaotakiwa kumsaidia nao wanapata akili ile ile kwamba tunatakiwa tupige sound ili tuweze kufika mahali fulani, sasa athari zake ndiyo hizo ambazo tunaziona leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa tu mifano michache, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara lakini pia ni Waziri Kivuli kutoka kwenye Serikali yetu ambayo tunategemea Mungu akitujaalia tutakuja kuiongoza hii nchi, nitakuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na sitegemei kama nitafanya kama ambavyo kaka yangu Mheshimiwa Waziri hapa anafanya kwa sababu kwa vyovyote vile tunataka kulisogeza hili Taifa letu mbele. Ndiyo maana juzi wakati ninatoa mchango wangu nilijaribu kuwakumbusha ndugu zangu Wabunge kwamba lazima tuangalie kwanza uzalendo na kulitetea Taifa letu ili tuweze kujua tunakwenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo ambayo sasa hivi kaulimbiu yake ni masuala ya viwanda kwamba tutakapofika mwaka 2020/2025, basi nchi yetu iwe ya viwanda. Lakini nimwambie tu Mheshimiwa Waziri kwamba ameanza vibaya jukumu hili. Tukiwa kwenye Kamati tuliletewa taarifa kwamba mpaka sasa Tanzania kuna viwanda 53,050 viwanda hivyo ambavyo Tanzania tunavyo mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Jimboni kwangu sina kiwanda kile ambacho kipo wananchi wanakifahamu kwamba hiki ni kiwanda na ile tafsiri ya viwanda iliyozoeleka kwenye mitaa yetu, lakini tumeona wamezidi kuwapa jukumu pia sasa hivi kutoka TAMISEMI wamekwenda kuwapa majukumu Wakuu wa Mikoa na wengine kwamba kila Mkoa lazima wamhakikishe wamepata viwanda 100. Wanachokifanya sasa hivi ni kwamba Mkuu wa Mkoa anaamua, anatafuta watu 25 wenye uwezo wa kuwa na cherehani nne, nne halafu analeta taaifa kwamba tumefanikiwa kupata viwanda 100. Sasa hii hatuwezi kwenda vizuri. Tunachojaribu sisi kuangalia ni vile viwanda vya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuomba ile taarifa kwamba nchi yetu ina viwanda 53,000 na mimi nilitamani nivijue ili kama inawezekana basi niweze kufahamu Jimboni kwangu kuna viwanda vingapi, lakini bahati mbaya kabisa na Mheshimiwa Naibu Waziri nilimkumbusha kwenye kikao chetu cha mwisho cha Kamati mpaka tunaingia hapa hiyo taarifa sijaipata, sijui kama wajumbe wenzangu, Mwenyekiti au Makatibu wa Kamati kama walipata hiyo taarifa inayoonesha Tanzania tuna viwanda 53,000 kwa sababu nilitaka tuvifahamu kwa majina ili tuweze kuwasaidia ndugu zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tena sasa kiti chako watuambie hizo taarifa, walisema ni document kubwa sana tukaomba basi tupate in software ili iweze kutusaidia kuvitambua hivyo viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wanapoongelea habari ya viwanda, ukienda kwenye kitabu chao cha hotuba, ukienda ukurasa wa 13 kwenye taarifa ya Mheshimiwa hapa waziri anasema miradi mipya ya viwanda, sasa sehemu ambayo sijaielewa na nitaisoma kidogo kama alivyoelezea

yeye; kuanzia Julai, 2017 mpaka Machi, 2018 jumla ya miradi 243 yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 4,169.11 inatarajiwa kuajiri watu 49 ilikuwa imesajiliwa, wanaiongeza hiyo wanasema kwenye miradi mipya ya viwanda. Mimi nilitegemea kama Bunge au kama sisi Watanzania tulikuwa tuna interest ya kusikia bada ya kusajili nini kimefanyika, usajili tu peke yake haitusaidii, kwa hiyo, tumeleta hapa habari ndefu sana lakini kimsingi tunataka tusikie mwishoni nini kimefanyika baada ya usajili huu. Hii ndiyo maana tunasema tunakwenda mbele na tunarudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kuangalia pia kwenye kitabu chao hiki hiki, tunajaribu kuongelea hapa wanasema viwanda mama na miradi ya kielelezo. Tumeona hapa wabunge wengi sana wanaongea habari ya Mchuchuma karibia asilimia 50 ya Wabunge walioongea kuchangia kwenye hii Wizara wanaongea habari ya Mchuchuma. Huko Mchuchuma tunakoongea sasa hivi pesa ya Mchuchuma na Liganga pesa iliyotengwa ni karibia shilingi bilioni 10 ambayo inakwenda kufanya nini kimsingi bado haijasemwa moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hii ni nchi ambayo kwa vyovyote ili tuweze kwenda sawa sawa lazima tuangalie wenzetu walivyopita waliopita walikuwa wanafanya nini kama ambavyo Mheshimiwa Mariam Ditopile pale alijaribu kushauri kwa sababu hizi regime lazima zipokee kijiti kutoka kwenye regime iliyopita. Tumeona sasa hivi kulikuwa kuna utaratibu wa Mtwara corridor, Serikali ya Awamu hii ya Tano imesahau kabisa habari ya Mtwara corridor na hii inajithibitisha wazi wazi tunapokwenda kuongea habari ya Mchuchuma, tunakuja hapa tunaita Mradi wa Mchuchuma na Liganga ambao ni mradi mama na mradi kielelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kwenda kuchimba chuma, nchi za Ulaya pamoja na china walipofanya mapinduzi ya kiviwanda wao walitegemea sana chuma. Chuma ndio kiwanda mama ili uweze kujenga kitu kingine chochote unahitaji kupata chuma. Unaambiwa pale
Mchuchuma na Liganga tukiamua ile kuchuma chuma yetu tuna uwezo wa kujitosheleza chuma kama sisi wenyewe kama nchi, lakini pia tuna uwezo wa kuichukua hii chuma tukaipeleka nchi za nje kwenda kuuza tukajiingilia sisi forex matokeo yake sasa hivi pesa nyingi za kigeni Serikali hii imeamua kuzitumia kwenda kununa chuma nje kwa ajili ya kuja kufanya miradi mikubwa hapa kwetu badala ya kuwekeza kwetu baada ya miaka mitano au 10 mbele tukahakikisha na sisi tunapata chuma hapahapa nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kuisikitisha kabisa ni kwamba ili chuma iweze kufika bandarini na tunategemea bandari itakayosafirisha chuma ni Bandari ya Mtwara hakuna mpango mkakati mzuri unaoonesha namna ya kusafirisha chuma hii. Bado tunataka turudi miaka ya 40 kwa kusafirisha chuma kutoka Mchuchuma na Liganga kuleta kuileta Bandari ya Mtwara kwa kutumia barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara za Mtwara, Songea tumezipata kwa shida kubwa sana, leo hii tunataka kurudi kulekule badala ya kufikiria kujenga Reli, ambao mkakati wake hauonekani. Sasa hivi karibia mwaka wa 20 kule kuna watu walioekewa X kuonyesha kwamba kunatakiwa kupita reli inayotoka Linganga na Mchuchuma hiyo Reli inakwenda mpaka bandarini Mtwara imepita Jimbo la Mtama, imepita baadhi ya maeneo la Jimbo Ndanda, imepita Songea, Tunduru na kuelekea kote mpaka kufika Liganga na huko Mchuchuma lakini Serikali haijaonesha kwa namna yoyote jinsi gani inataka kufanya kazi kwenye hii Reli ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii Reli ya Kusini kihistoria ilikuwepo toka mwaka 1949 lakini mara tu baada ya uhuru Reli ya Kusini iling’olewa. Tulitegemea leo tunakwenda kuendeleza ile Reli ya Kusini ili iweze wale wananchi pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye kitabu cha Kamati hapa, matatizo yaliyopo kwenye hii na ninaomba Mheshimiwa Waziri akasome ili kuboresha kwenye majibu yake atakapokuja hapa. Wenyewe wanasema kwenye ukurasa wa sita na Kamati inaishauri Wizara. Inasema hivi, upatikanaji wa fedha kutoka Hazina kwa kiwango kikubwa unaonyesha kuwa Serikali inapanga matumizi makubwa yasioakisi uhalisia wa vyanzo vya mapato, hali hii imeathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ushauri wa Kamati, na Mheshimiwa Mwijage naomba hii uingalie sana, ndugu zetu wa Wizara ya Fedha hawana nia njema na wewe. Hawana nia njema na Naibu wako Waziri kwa sababu ndio wanaokwamisha. Haiwezekani bajeti iliyopitishwa kwenye pesa za maendeleo wawape nyinyi asilimia tisa tu, na wakati mwaka uliopita 2015/16 waliwapa asilimia tano na bado tunasema nchi yetu tunataka kuisogeza kwenda kuwa nchi ya viwanda. Nchi ya viwanda inapewa pesa za maendeleo, Wizara inayosimamia masuala haya asilimia tisa Wizara inayosimamia maswala haya asilimia tano. Kwa hiyo, katika hii miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano pesa pekee ambayo imepata kwa ajili ya maendeleoe kwenye Wizara yako ni asilimia 14 pekee. Ni kweli tuna nia ya kutekeleza hiyo Ahadi ya viwanda kwa wananchi? Na lazima watu tuwaambie ukweli kwa sababu tusipofanya hivyo hatutaweza kufika kokote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeendelea kwenda mbele, kwenye changamoto zilizopo wanasema hivi kumekuwa na ucheleweshwaji wa fedha za maendeleo, jambo linalokwamisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati na hatimaye kupanda kwa gharama hizo mwaka hadi mwaka. Hayo ndio matataizo na umeangalia hapa Wizara zote wamejaribu kuongelea suala hilo hilo. Ukienda Wizara ya Maji kuna matatizo ya ucheleweshwaji wa pesa, ukienda Wizara ya Nishati na Madini yaani ni kote kuna matatizo ya ucheleweshwaji wa pesa unaofanywa labda kwa makusudi kabisa na Waziri kwa maana ya kutokutaka kuwasaidia wenzie ili ikiwezekana yeye ndio aonekane anafanya vizuri kuliko Mawaziri wote, jambo hili msipolikemea haraka katika vikao vyenu vya Baraza la Mawaziri niwaambie Hazina Wizara ya Fedha inawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyofahamu kwa uelewa wangu mdogo tuu wa masuala ya mahesabu mimi ni mtaalam wa hesabu pia, kwamba mara baada ya kupitisha bajeti kinachofata kunakuwa kuna cash flow hazina wanatakiwa watoe pesa kutokana kwenye cash flow kwenye matukio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 10 wanatakiwa wawe wamepata shilingi milioni mbili kwa ajili ya kugharamia shughuri fulani. Lakini sasa hivi kuna utaratibu mpya hata sijui hata unapotokea. Bunge likishapitisha hapa kuna watu wengine nawasikia hapa kwenye taarifa wanasema kutoka juu ya Mheshimiwa Waziri mwenyewe hapa kuna sehemu ameandika wakati anajadili hilo suala la Liganga na Mchuchuma yaani ni robo tu ya ukurasa kwenye kitabu chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwishoni kabisa anamalizia kwamba huu Mradi wa Liganga na Mchuchuma unakwenda vizuri anasema; taarifa ya awali ambayo inatakiwa kutolewa maamuzi na mamlaka husika. Sasa mamlaka anayopewa Waziri na Bunge hili halafu naye anatafuta mamlaka nyengine husika kwa nini hiyo sasa isije hapa ikajibu maswali ya Wabunge kwamba Mchuchuma na Liganga itaanza kufanya lini shughuli zake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nikuombe jambo moja, mama yetu Mheshimiwa Lulida hapa ameongea kuhusu viwanda vya korosho kule Mtwara ambavyo sisi tumeshakata tamaa moja kwa moja wa sababu hatuoni juhudi yoyote ile ikifanywa ili kuweza kufanya, kwa hiyo tunakuomba sana ujitahidi ili vile viwanda ziweze kuanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine jaribu kufungamaana na Wizara ya Kilimo, kwa sababu ili uweze kufanya kazi vizuri lazima ushirikiane na Wizara.