Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa maendeleo katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji hauendani kabisa na kaulimbiu ya Tanzania ya viwanda. Utekelezaji wa bajeti ya viwanda licha ya ukweli kwamba suala la viwanda lilikuwa halipigwi upatu na wala halikuwa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Nne, mara tu baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika Wizara hii umeyumba sana licha ya kwamba ni Serikali inayojenga uchumi na viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ilianza utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Utekelezaji kwa kutoa asilimia tano tu ya fedha zilizokuwa zimetengwa kutekeleza miradi ya maendeleo. Katika fedha hizo hakukuwa na hata senti moja ya fedha za ndani. Ni vizuri Serikali ikatoa fedha za kutosha ili kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuporomoka vibaya kwa sekta ya viwanda vidogo na vya kati, ukweli ni kwamba viwanda vidogo ndiyo chimbuko la mapinduzi makubwa ya viwanda. Sekta hii imekuwa haipewi kipaumbele na Serikali jambo ambalo limesababisha sekta hii kuporomoka vibaya na kufifia kwa ndoto za kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sekta ya viwanda vidogo vidogo ni dhaifu na imeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa. Sekta hii ya viwanda vidogo vidogo haikui kwa kiwango cha kuridhisha. Kumekuwa na utekelezaji mdogo sana wa bajeti za maendeleo kwa viwanda vidogo vidogo katika ngazi zote za Serikali. Ni vizuri viwanda vidogo vidogo wapewe huduma za mafunzo ya kuridhisha. Vilevile

hakuna maendeleo ya teknolojia katika sekta ya viwanda vidogo vidogo na vya kati, kwani sekta hii ya viwanda inaporomoka kwa kasi kuliko ukuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya viwanda vidogo vidogo na vya kati ndiyo moyo wa maendeleo ya viwanda hata katika nchi zilizoendelea, lakini Tanzania sekta ya viwanda vidogo ni dhaifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu idadi ya viwanda na masoko nchini, Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikijinasibu mara kwa mara kuwa inajenga uchumi wa viwanda na imekuwa ikitoa takwimu mbalimabli zikionesha idadi ya viwanda vinavyoanzishwa nchini kwa lengo la kutoa taswira nchi inaendelea vizuri kiviwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji hajawahi kuwasilisha kwenye Bunge lako tukufu mpango wa ujenzi wa viwanda na uzalishaji masoko ya bidhaa utakavyofanyika. Aidha, yapo maelekezo yaliyotolewa kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa kila Mkoa unajenga viwanda 100 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haijaelezwa ni viwanda vya namna gani vinaenda kujengwa na kwa tafiti zipi za masoko ya bidhaa zitakazozaliwa na viwanda husika; japokuwa Serikali imeeleza kwenye mpango wa miaka mitano kuwa itajikita kwenye uchumi wa viwanda na kutengeneza ajira? Vilevile ongezeko la kodi na kubadilika kwa ghafla kwa mifumo ya usimamizi wa biashara inayofanywa na Serikali yameathiri ukuaji wa biashara nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pato la Taifa kuonekana kukua, mazingira ya biashara nchini siyo rafiki kwa uwekezaji na maendeleo ya biashara. Kutokana na hali hiyo, kuonekana dhahiri kuwa shughuli za kiuchumi ni dhaifu, hivyo kutopelekea kuzalisha ajira na kupunguza umasikini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kumekuwa na ongezeko kubwa la mikopo isiyolipika kwenye mabenki, jambo ambalo linaathiri mazingira ya ufanyaji biashara kwa sababu udhaifu uliopo katika mfumo wa sasa wa kodi na maelekezo ya kiutawala yasiyoangalia maslahi ya wafanyabiashara, hii inapelekea wafanyabiashara kushindwa kulipa mikopo kwenye mabenki ya ndani, hivyo kuathiri mazingira ya biashara katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu suala la kodi na urasimu yanavyoathiri biashara nchini. Serikali inawahimiza wafanyabiashara nchini kulipa kodi ya maendeleo (jambo ambalo ni jema) lakini haijaweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa biashara hizo. Ukweli ni kuwa mazingira ya kuanzisha biashara nchini ni magumu. Mfano, kuanzisha biashara ya kawaida unaweza ukatakiwa kupitia kwenye mamlaka na wakala zaidi ya tano na sehemu zote hizo kuna gharama ambazo lazima uzilipe kama mfanyabiashara ili kupata vibali au leseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapato (TRA) siyo rafiki kwa wafanyabiashara. Hii ni kutokana na maafisa kuambatana na vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa ukusanyaji na ufuatiliaji wa kodi, jambo ambalo linatia hofu wafanyabiashara na kuamua kufunga biashara zao. Ni vizuri Serikali isijikite zaidi kwenye ukusanyaji wa kodi bila kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi ya rasilimali ya makaa ya mawe na chuma katika maendeleo ya viwanda; Shirika la Maendeleo la Taifa lilishakamilisha tathmini ya kufahamu wingi na ubora wa makaa ya mawe, pamoja na chuma cha Liganga na kubaini kuwa tuna makaa ya mawe ya kutosha, kwa kuwa tathmini ya mazingira ilishafanyika na Serikali kueleza kuwa ujenzi wa miradi hiyo ulitarajiwa kuanza mwaka 2016 na uzalishaji kuanza mnamo mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itumie chuma cha Liganga katika kujenga reli ya standard gauge badala ya kutumia vyuma vya Uturuki, kwani tuna chuma cha kutosha kwa matumizi ya ndani na akiba ya kuuza nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea kuchelewa kulipa fidia ili kupisha miradi ya biashara na viwanda, kuna athari kubwa kiuchumi. Kwanza muda unavyozidi kwenda ndiyo thamani ya ardhi inazidi kupanda. Hivyo kuchelewa zaidi ni kuongeza kiwango cha fidia kitakacholipwa kwa wanaodai. Vilevile huu ni unyanyasaji mwingine wa Serikali dhidi ya raia wake, lakini pia ni kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya viwanda na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kazi rahisi kuanzisha viwanda kama ambavyo Serikali hii imekuwa ikisema na kutangaza kwenye vyombo vya habari. Pamoja na gharama kubwa za kuanzisha na kuviendesha hivyo viwanda, bidhaa zitakazozalishwa ili kuingia kwenye soko na kukubalika katika jamii ya watumiaji huwa mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ikaanzisha viwanda vya uunganishaji kama wenzetu wa Kenya walivyofanya au kama inavyofanyika kwa matrekta ya ASUS yanayounganishwa hapa Tanzania, lakini kiwanda mama kipo nchi za nje. Kwa njia hii tutakuwa tumeepuka gharama kubwa ya matumizi ya nishati ya umeme na gharama ya kutangaza bidhaa husika na hivyo bidhaa husika zitakuwa shindani katika soko la ndani na nje.